|
|
| Vipi
umoja wetu uwe hatari ?
MOTO ni kitu muhimu sana katika maisha ya kila siku ya binadamu. Tunakoka moto kupikia, kuchemshia maji ya kunywa, kuota wakati wa baridi, kupatia mwangaza penye giza na matumzi mengine mengi yenye manufaa kwetu. Lakini pia ni kweli kabisa kuwa moto huo huo unaweza kuwa kitu cha hatari sana kwetu kama haukutumiwa vizuri. Pakipatikana mtu kati yetu, ambaye kila aonapo moto, anapiga kelele "hatari jamani", tutakuwa hatuna budi kumfikiria huyu mwenzetu kuwa labda mwoga sana wa kupindukia au mawazo yake yana kasoro fulani. Labda kila akiona moto anadhani ataungua au ataunguliwa na mali yake. Kwa kuwa kama ana mawazo au fikra nzuri, kwanini anapoona moto hafikirii kuwa labda patapikwa au pana uhunzi? Siku nyingi zilizopita, wahenga walituambia kuwa umoja ni nguvu. Kwa yeyote mwenye akili timamu falsafa hii ya wahenga haipingiki. Kwa taifa lililo bora, kitu umoja ni jambo la kufaa sana. Lakini ni lazima tukubaliane kuwa umoja ulio bora sharti uanzie majumbani mwetu. Umoja wa familia ndio msingi madhubuti wa umoja wa ukoo mzima. Na kuwa umoja wa koo zote ndio uimarishao umoja wa kabila zima. Hali kadhalika, umoja wa makabila yote ndio uzinduao umoja wa Taifa. Wako wenzetu ambao fikra zao ni chafu. Wao wakisikia tu kuna umoja wa Wandengereko, tayari wamekwishapiga kelele "hatari hiyo, si ukabila huo!" Na wakisikia kuna umoja wa Waislamu. "Loo, salale! Hiyo ndio kabambe, huo si ndio udini wenyewe". Inakuwa dhambi kwa Wandengereko kuwa pamoja au dhambi kwa Waislamu kuwa pamoja. Hata kama kuwa pamoja kwao ni kwa maslahi yao. Yale yale ya yule mwenzetu ambaye yeye kila akiona moto, wimbo wake ni ule ule "hatari". Umoja wa Tanzania ulikuwako, upo na utaendelea kuwapo. Ukabila ulikuwapo, upo na utaendelea kuwapo. Udini ulikuwapo, upo na utaendelea kuwapo. U-Yanga na U-Simba, vyote hivyo vilikuwapo, vipo na vitaendelea kuwapo. Na si hatari yoyote, na wala havikuzuiwa, wala havizuii na wala havitazuia Umoja wa Taifa letu zuri hili. Kwa mtazamo mzuri, vyote hivyo vinaonekana kama matofali ya kujengea umoja wetu kwa ujumla. Umoja wa Wandengereko hauzuii Umoja wa Madaktari wala Umoja wa Waislamu. Kama vile Umoja wa Wakristo usivyozuia Umoja wa Yanga au Simba. Hii "hatari", "hatari" ya nini? Na inatokea wapi na kwa sababu gani? Iko haja kwa Watanzania ya kukataa kutawaliwa kiakili. Hawa akina "hatari", "hatari" mawazo yao nayo ni hatari vile vile na ajenda zao ambazo nazo pia ni hatari. Kwetu sisi Waislamu, umoja na udugu wa Waislamu ni kitu azizi na muhimu sana. Katika Qur’an na Sunnah, Waislamu tunahimizwa sana kuwa pamoja na kushikamana. Kiasi cha kuambiwa kuwa kila Muislamu ni ndugu ya Muislamu mwingine. Katika hilo, hatukuwekewa mipaka ya nchi, rangi ya mwili wala jinsia. Kwa hiyo kwa Waislamu ni aina ya ibada. Ukiwazuia Waislamu kuwa na umoja wao, ni sawa na kuwazuia wasifanye moja ya ibada zao, na hilo haliwezekani, maana halitakubalika. Katika kufuata misingi ya Qur’an na vigezo alivyotuachia mpendwa Mtume wetu Muhammad (s.a.w.), Waislamu wa Tanganyika tukajiunga na wenzetu wa Zanzibar, Kenya na Uganda katika East African Muslim Welfare Society, tukawa na umoja wetu wa Afrika Mashariki nzima. Kwa hakika kwangu mimi, hilo lilikuwa tofari zuri mno sana la kuundia Shirikisho la Afrika Mashariki. Lakini lahaula, akina "hatari" hawakuona nionavyo mimi, katika ajenda zao kali wakaona bora wapitishe fitna umoja huo uvunjwe. Wenye meno makali wakazitafuna tafuna kamba za mshikamano wetu, wakazikata kata tukaparaganyika kama walivyotaka wao. Hayakutosha, ikatafutwa mbinu, tukaundiwa BAKWATA. Hii Bakwata ikaundwa katika mfumo wa U-Pope. Akapachikwa Sheikh Mkuu, akapewa kigari na ruzuku kidogo, naam, mvurugano na mtafaruku kati ya Waislamu ukapatikana. Ili mradi ikawa huyu Bakwata na yule si Bakwata. Na hivyo ndivyo ilivyokusudiwa. Wagawanye uwatawale, wagombanishe uwadhibiti. Na sisi tukakubali kuwacha mila, desturi na maadili ya Uislamu, basi ndiyo hivyo tena yanatukuta yakutukuta. Ninaposema waanzilishi wa Bakwata si Waislamu, nina maana ya kuwa waliozalisha wazo hilo si Waislamu, ila tu waliwatumia Waislamu wenzetu ili iwe kiini macho. Waislamu hatuna mfumo wa kuwa na Pope, Askofu Mkuu, Askofu na sijui Padre. Hatuna hayo. Waislamu tuna Imamu ambaye ni kiongozi wa swala. Tuna Sheikh wa Community. Tuna Alim wa chuo. Tuna Ulamaa (Scholar) na vitu kama hivyo. Na wote hao hawatawazwi, huchaguliwa na watu kwa kukubalika tu, kutokana na ilmu zao za kidini na wala hawatangazwi bombani. Ukiutazama tu mfumo wa Bakwata, mwenye macho haambiwi tazama. Hata hivyo, mimi naamini kuwa walioshikilia Bakwata hivi sasa ni Waislamu wenzetu na Waislamu kwelikweli na kuwa wanamtanguliza Allah (s.w.) mbele kuliko wao wenyewe na kuwa wanazo jitihada za kuikomboa Bakwata kutoka mikono ya serikali na kuiweka katika mikono ya Waislamu wenzao wa Tanzania ili iweze kutumika kwa manufaa na maslahi ya Waislamu, Insha-Allah! Kinacho nikhofisha, hivi sasa ni migogoro ya mara kwa mara kati ya viongozi wa Bakwata, wao wenyewe kwa wenyewe. Na mara nyingine, na viongozi wengine wa Kiislamu au wa taasisi nyingine za Kiislamu. Jambo ambalo linanistua sana ni kuwa katika karibu kila mgogoro au mzozo, jina la Sheikh Yahya halikosekani. Mimi sijui kama anapakaziwa tu au kama ni kweli, Allahu ya Alam! Sheikh Yahya Hussein mimi ni kaka yangu, tena namuheshimu sana, lakini napenda kumnasihi akumbuke dhulma alizofanyiwa, yeye mwenyewe, mnamo mwaka wa 1949, pale katika shule ya Wavulana ya Sekondari, Mtaa wa Kitchwele na akina Mwalimu Misana, Mrs Hucks na Mr Mundy. Na atambue kuwa dhulma zile ndizo hizo hizo zinazotukabili hivi sasa ingawa hivi sasa sura za wahusika zimebadilika. Akishatambua hivyo, basi azielekeze nguvu zake katika kupambana na dhulma zinazotukuta Waislamu wa Tanzania hivi sasa.
|
YALIYOMO
Tahariri Onyesheni ushujaa wa Badri Daniel kuwatimua waumini Msikitini Waislamu Moshi: Wadai kulishwa nguruwe, vibudu Dondoo za Kisakolojia
Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897) - 2 MASHAMBULIZI YA MAREKANI NCHINI IRAQ Njia bora zitakazotusaidia kuwalea
watoto
Ijue Madrasatul-Qaadiriya Sokoni
I Arusha.
Tutafute kwanza ufalme wa Allah (s.w.)
Chuo cha Kilimo Ukiriguru kupata
Msikiti mpya
Huduma za maji Kondoa haziridhishi
Mnyororo wa imani
Je, Yesu alibatizwa?
Kufuatia Waislamu kuritadishwa Merela Morogoro: Masheikh wa mjini watupiwa lawama Abiria walaani kumwagiwa pombe Kondoa Sheikh Bafadhil ateuliwa
kudhamini waandishi wa habari Morogoro
Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|