|
Mashairi
Ni urithi wa shetani
Nakamata tena peni, karatasi mkononi,
Nakereketwa moyoni, kutulia sitamani,
Niweke upembezoni, niwakemee wahuni.
Pombe zote duniani, ni urithi wa shetani.
Sikubali abadani, ufuasi wa shetani,
Urithiwe sitamani, kunifanya punguani,
Wawafaa “hayawani”, walojishusha thamani,
Ni urithi wa shetani, mimi sikubaliani.
Mwatangaza redioni, mabango barabarani,
Safuni magazetini, na kwenye televisheni,
“Wetu urithi jamani”, mwasema bila huzuni,
Ni urithi wa shetani, ni ukweli si utani.
Upumbavu uacheni, musitutie kundini,
Sisi sote si wahuni, ni watu wenye thamani,
Pombe mali ya wahuni, si ya kwetu waumini,
Pombe zote duniani, ni urithi wa shetani.
Walio madarakani, mvinyo wauthamini,
Wakaa maofisini, viwanda kuvisaini,
Wapanda majukwaani, kutwambia “tumieni”,
Ni urithi wa shetani, sisi tunakupasheni.
Nyumba tatu mitaani, pombe hukosi dukani,
Asubuhi na jioni, wengi wako mvinyoni,
Wamekaa vikundini, pombe watia vinywani,
Lajengwa taifa gani, kwa urithi wa shetani?
Wakubwa oneni soni, acheni kuturubuni,
Pombe ina tafrani, asiyejua ni nani?
Yatokomeza amani, watu hawaelewani,
Ni urithi wa shetani, tunasema waumini.
Ajali barabarani, na uzembe makazini,
Kubakana mitaani, vichupi madanguroni,
Kudidimiza uchumi, na kueneza ukimwi,
Pombe ni nambari wani, urithi wa shetani.
Urithi, urithi gani, kututia ulevini?
Asili, asili gani, kujenga umajununi?
Hapa sioni usomi, ila ni upunguani,
Ni urithi wa shetani, nawapasha fahamuni?
Familia majumbani, zavunjika kwa magumi,
Watoto wa mitaani, waongezeka nchini,
Wapata malezi duni, wazolewa na uhuni,
Pombe zote duniani, ni urithi wa shetani.
Nimefika kituoni, na walevi siungani,
Nimefikia mwishoni, nimewajuza kwa peni,
Nimesema kwa makini, wazi wazi hadharani,
Ni urithi wa shetani, hapa ninakuageni.
Idd S. Kikong’ona,
Morogoro.
Msisubiri kampeni
Enyi mlio madarakani, jibuni risala yetu,
Isisubiri ilani, kupatia kura zetu,
Msitufanye majnuni, kuchezea vichwa vyetu,
Msisubiri kampeni, tunayo ajenda yetu.
Mmeunadi uwazi, vipi unakushindeni,
Mlidhani utarazi, sasa shingo kitanzini,
Mlipigwa bumbuazi, risala tulipokusomeeni,
Msisubiri kampeni, tunayo ajenda yetu.
Kwanza mlitukejeli, tunasemea pembeni,
Mwaliko mlipokubali, tukanena hadharani,
Mlipopewa ukweli, Mufti akawakingeni,
Msisubiri kampeni, tunayo ajenda yetu.
Kusema ule ukweli, risala ile si ngumu,
Hamtaki kukubali, Waislamu mewahujumu,
Msitumie dalali, ili dhulumu idumu,
Msisubiri kampeni, tunayo ajenda yetu.
Kuhusu la Mwembechai, ushahidi uko wazi,
Waliodhulumu uhai, hao ndio wachokozi,
Acheni kutulaghai, wawajibishwe viongozi,
Msisubiri kampeni, tunayo ajenda yetu.
Wahukumiwe polisi, waliopiga risasi,
Wafutiwe hiyo kesi, waliokuwa mahabusi,
Ponda asitiwe wasi, apewe uhuru halisi,
Msisubiri kampeni, tunayo ajenda yetu.
Walidhiri kina mama, nasema pia wasiachwe,
wameufanya unyama, lazima waadhibiwe,
Pamoja na adhabu ya kiama, jela pia watiwe,
Msisubiri kampeni, tunayo ajenda yetu.
Wote walipwe fidia, waliopata msikukosuko,
Wakati umewadia, aadhibiwe Paroko,
Katika ile kadhia, yeye alitia choko,
Msisubiri kampeni, tunayo ajenda yetu.
Kuhusu uwiano, msitupunje jamani,
Zingatieni agano, madaraka nao wapeni,
Wasomi sasa tunao, madaraka nao wapeni,
Msisubiri kampeni, tunayo ajenda yetu.
Kuhusu suala la kadhi, mwendeni mzee wenu,
Risala mumkabidhi, mumpe maoni yenu,
Msije shushiwa hadhi, atajificha mwenzenu,
Msisubiri kampeni, tunayo ajenda yetu.
Uislamu haukuacha, kila jambo bainisha,
Sio dini ya mchacha, ni mfumo wa maisha,
Waislamu hawatokacha, sheria kusimamisha,
Msisubiri kampeni, tunayo ajenda yetu.
Msibuni mikakati, mfiche yaliyo wazi,
Msipoteze wakati, enyi wachapakazi,
Hata kwa mihadharati, hamtatutia usingizi,
Msisubiri kampeni, tunayo ajenda yetu.
Batuli Hussein,
S.L.P. 1876,
Morogoro.
|
YALIYOMO
Tahari
Tusirudishane nyuma
Mwaka mmoja wa mauaji ya Mwembechai:
Waliouawa ni wanne
Na Mwandishi wetu
Waasisi wa TAA waibuka kupigania haki
zilizoporwa
Kuhujumiwa Waislamu kielimu: Mzazi
adai mwanafunzi Adam Rashid kafelishwa
Maoni yetu: Tuondoleeni wenye mikono
ya damu
MARADHI YA KISAIKOLOJIA: MULTIPARAPHILIASIS
Askari wa Tume ya Jiji wapora mkaa
Kuchangia Radio Kheri Broadcasting
Station
Yesu Kristo na Yohana Mbatizaji
Na BERNARD B. MWENDA
Wakereketwa CCM wawakosha
wauaji wa Mwembechai
Na Idd Kikong’ona, Morogoro
Ufugaji holela wa nguruwe
waikumba Dodoma
Na Abu Zubeir, Dodoma
Watembelea na kusaidia
wagonjwa Arusha
Mkuu wa wilaya awatimua Masheikh
ofisini kwake
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Kutoka magazeti ya zamani
Sayansi na Teknolojia
[Windows: Mambo Mazuri ya Kuyajua]
Masomo ya Kiislam
Barua za Wasomaji
Mashairi
Chakula na Lishe
[Kauli hii ya serikali itatumaliza Watanzania kwa njaa]
Kumbukumbu ya mauaji Mwembechai
[Maazimio ya Maimamu Dar]
|