AN-NUUR 
Na.188 Shawwal 1419, Februari 12 - 18 , 1999 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Kuhujumiwa Waislamu kielimu:
Mzazi adai mwanafunzi Adam Rashid kafelishwa
 
  • Ofisi ya Jiji yashangaa kwanini ameachwa
  • Adaiwa kuwasaidia ‘vilaza’ majibu
IMEFAHAMIKA kwamba wazazi kadhaa Waislamu wamekuwa wakipeleka malalamiko yao kwa Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi kutokana na kutokuridhishwa kwao na matokeo ya mtihani wa darasa la saba. 

Katika malalamiko yao baadhi ya wazazi wamedai kwamba watoto wao wamehujumiwa. Egemeo la madai yao ni kwamba watoto wao wamekuwa wakifanya vizuri darasani lakini wameachwa wakachaguliwa watoto ambao uwezo wao ulikuwa mdogo sana. 

Katika barua yake kwa Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi, mzazi Ramadhani Rashid ameeleza kwamba baada ya kuona mtoto wake hakuchaguliwa na kwa kujua uwezo wa mtoto wake alifuatilia suala hilo Ofisi ya Elimu ya Jiji. 

Huko anasema kwamba alielezwa na mtu mmoja anayeitwa Kihiyo kwamba mtoto wa mwisho kuchaguliwa katika shule ya msingi Rutihinda alipokuwa anasoma mtoto wake ni yule aliyekuwa na alama 105. 

Alipotaka kujua alama alizopata mtoto wake alionyeshwa matokeo rasmi yaliyoonyesha kwamba mtoto wake Adam kapata jumla ya alama 108 (Lugha 40, Hisabati 35 na maarifa 33). 

Kwa maelezo ya Bw. Ramadhani Ofisa huyo hakuamini kwamba mtoto huyo Adam hakuchaguliwa kwa alama hizo; hivyo akaleta orodha ya waliochaguliwa wakaangalia pamoja. Hata hivyo jina hilo halikuonekana. 

Hiyo ilikuwa Januari 18. Ofisa huyo wa Elimu ya Jiji alimtaka mzazi huyo ampe muda afanye uchunguzi na arejee Januari 25, 1999 kuchukua jibu. 

La kushangaza Bw. Ramadhani anasema alipofika aliambiwa kwamba yale aliyoonyeshwa awali hayakuwa "Official Results" (yaani matokeo rasmi). 

Alipohoji zaidi wakaleta dai jingine kwamba mtoto wake ni miongoni mwa waliofutiwa matokeo kwa kuonyeshana majibu. 

Katika kuhoji zaidi Afisa Elimu wa Jiji alitoa maelezo kwamba pamoja na kuwepo kuibiana lakini ilifanyika tathmini ambapo wale watoto ambao walikuwa wakifanya vizuri darasani walichaguliwa lakini wale ‘vilaza’ waliachwa japo walifanya vizuri (kwa kuibia). 

Kwa maelezo hayo ya Afisa Elimu kwamba ilifanywa tathmini wanafunzi ‘strong’ (kama alivyotumia neno hilo) wakachaguliwa wale "weak" wakaachwa; "Mbona wamechaguliwa wanafunzi "weak" wapatao 37 katika shule ya msingi Rutihinda ambao wote walikuwa nyuma kimaendeleo kwa mtoto Adam na yeye Adam kuachwa" anahoji mzazi Ramadhani Rashid. 

Mzazi Ramadhani ameiomba mamlaka husika iingilie kati suala hili ili haki ya mtoto wake Adam ambayo imehujumiwa irudishwe. 

Mzazi huyo ametahadharisha kwamba katika kulishughulikia suala hili busara itumike na pasiwepo na kuoneana haya au kulindana. 

Gazeti hili liliwasiliana na Idara ya Elimu ya Msingi katika Wizara ya Elimu ambapo msemaji mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mwigio aliliambia gazeti hili kwamba ni kweli malalamiko hayo yamefika Wizarani na Wizara inawasiliana na Tume ya Jiji kutafuta ukweli. 

Kesi kama hizi ni nyingi, hata hivyo ni wazazi wachache tu wanaochukua hatua za kufuatilia. 

Akijibu risala ya Waislamu ambayo ilikuwa imejaa malalamiko likiwemo lile la kudhulumiwa katika Elimu, Mh. Rais Benjamin William Mkapa pamoja na kutoa ahadi ya kuyashughulikia malalamiko hayo, aliwataka Waislamu wamsaidie kwa kuyafanyia utafiti wa kisayansi. Hiyo ilikuwa Januari 19 mwaka huu wakati wa Baraza la Eid el Fitr. 

Naye Mbunge wa Kigamboni Mh. Kitwana Kondo alihoji Bungeni hivi karibuni alihoji ni vipi watoto Waislamu ambao wapatao asilimia 71 ya watahiniwa wote wa Dar es Salaam wachaguliwe asilimia 21 wakati wale waliokuwa 21% walichaguliwa 79%. 

Wakati huo huo, wakati tukienda mitamboni kijana aliyejitambulsha kwa jina la Abdallah Kassim amelalamika kwamba ameshindwa kuelewa ni kwanini hakuchaguliwa wakati alikuwa akiongoza katika darasani. Amesema kwamba katika mtihani wa muhula wa kwanza alikuwa wa kwanza. 

Mwanafunzi huyo amedai kwamba yeye na wanafunzi wenzake Waislamu ambao pia walikuwa wakifanya vizuri hawakuchaguliwa. Aliwataja marafiki zake hao kuwa ni Adam Shaaban, Salma Swaleh, Aisha Mohamed na Amin Juma. 

Aidha, amedai kwamba wanafunzi wote kumi na tisa waliochaguliwa walikuwa wakipata alama za chini kabisa ikilinganishwa na wao. Amesema amemwambia mwalimu mkuu na ameahidi kulishughulikia. 

Aidha amedai kwamba wamemuona Afisa Elimu na akawaelekeza kwa Bw. Kihiyo wa Tume ya Jiji. 

Juu 
 

YALIYOMO 
  

Tahari 
Tusirudishane nyuma 

Mwaka mmoja wa mauaji ya Mwembechai: Waliouawa ni wanne
Na Mwandishi wetu

Waasisi wa TAA waibuka kupigania haki zilizoporwa

Kuhujumiwa Waislamu kielimu: Mzazi adai mwanafunzi Adam Rashid kafelishwa

Maoni yetu: Tuondoleeni wenye mikono ya damu

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: MULTIPARAPHILIASIS

Askari wa Tume ya Jiji wapora mkaa

Kuchangia Radio Kheri Broadcasting Station

Yesu Kristo na Yohana Mbatizaji
Na BERNARD B. MWENDA

Wakereketwa CCM wawakosha wauaji wa Mwembechai
Na Idd Kikong’ona, Morogoro

Ufugaji holela wa nguruwe waikumba Dodoma
Na Abu Zubeir, Dodoma

Watembelea na kusaidia wagonjwa Arusha

Mkuu wa wilaya awatimua Masheikh ofisini kwake
Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Kutoka magazeti ya zamani

Sayansi na Teknolojia 
[Windows: Mambo Mazuri ya Kuyajua] 

Masomo ya Kiislam 

Barua za Wasomaji 

Mashairi

Chakula na Lishe 
[Kauli hii ya serikali itatumaliza Watanzania kwa njaa] 

Kumbukumbu ya mauaji Mwembechai 
[Maazimio ya Maimamu Dar]
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita