AN-NUUR 
Na.188 Shawwal 1419, Februari 12 - 18 , 1999 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Yesu Kristo na Yohana Mbatizaji
 

NIMESOMA katika gazeti lako la Ijumaa Januari 8, mwaka huu, ukurasa wa 15 ulioandikwa na Bwana Muhibu Said akianzia na kichwa cha habari "Je Yesu alibatizwa?" Kwa kweli nilifurahishwa kuona Bwana Muhibu Said amekuwa na ufuatiliaji wa Biblia takatifu na amejaribu kuelezea ubatizo na mambo mengine kadhaa ya dhambi kwa wanadamu jinsi yalivyo. Ungana nami Bernard B. Mwenda katika kujibu hoja zake. 

Kutokana na hayo, nimeonelea niweze kutoa ufafanuzi mzuri zaidi kuhusu ubatizo wa Yesu Kristo na pia kuelezea makuzi ya Yohana Mbatizaji na Yesu Kristo hadi kufikia hatua hiyo ya ubatizo wa Yesu. 

Kwanza kabisa, kabla sijaanza kuelezea mada yenyewe au kichwa cha somo, napenda kuwaelimisha wasomaji na Bwana Muhibu Said kuwa Biblia ni maandiko matakatifu ya Mwenyezi Mungu na kila lilioandikwa katika Biblia hatuna budi kulichukua kama lilivyo na kulitendea kazi. 

Kumbukumbu 4:2 Msilisogeze neno niwaamurulo wala msipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana Mungu wenu, niwamuruzo. Kumb. 12:32 Neno niwaagizalo lolote liangalieni kulifanya, usiliongeze, wala usilipunguze. Tunaona kuwa iwapo tunapunguza Mungu atatuondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima Ufunuo 22:18. 

Kutokana na maandiko hayo, tunajifunza kuwa tunatakiwa kuliamini neno la Mungu kama lilivyo ili Mungu azidi kutufunulia tunachokifahamu na shetani ataingilia kati na kutuvuruga kabisa. 

Baada ya hayo sasa tuingie kwenye somo letu na tuanze kuangalia kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji na Yesu Kristo. Luka 1:13 "Lakini yule Malaika akamwambia. Usiogope Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elizabeth atakuzalia mtoto mwanamume na jina lake utamwita Yohana". 

Hapa tunaona jinsi kuzaliwa au kutabiriwa kwa Yohana Mbatizaji kulivyotokea. Tujiulize. Je! Wakati huo Yesu alikuwa wapi au aliuwa hayupo? Luka 1:26 "Mwezi wa sita, malaika Gabriel alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya jina lake Nazareti 27 kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu jina lake Yusufu, wabari ya Daudi na jina lake bikira huyo ni Mariam". 

Hapa tunaona kuwa malaika alienda kwa Mariamu na iwapo utasoma mpaka mstari wa 28 anataarifiwa Mariamu kuwa atapata mimba atazaa mwana. Luka 1:31 Tazama utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamme na jina lake utamwita Yesu". 

Hapa Mariamu amezidi kuelezewa jinsi itakavyokuwa kwake katika kuzaa mwana. Je wakati huo Elizabeth alikuwa wapi; wakati Mariamu anaambiwa habari hizi. Je, Elizabeth alikuwa alisha zaa siku nyingi? Hasha, tuone Mariamu anavyoendelea kuambiwa na malaika Gabriel katika Luka 1:36 Tena tazama jamaa yako Elizabeth naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake, mwezu huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa". 

Hapa tunazidi kufunuliwa kuwa Mariamu anaambiwa kuhusu kushika kwake mimba na anaambiwa pia Elizabeth ana mimba ya miezi sita. Hapa bila mashindano tunaona wazi kabisa kuwa Yesu Kristo na Yohana Mbatizaji walipishana miezi sita tu katika kuzaliwa au katika kutunga mimba. 

Kutokana na hayo, sasa tunaweza kufahamu kuwa wakati Yohana anabatiza ule ubatizo wa toba tayari Yesu Kristo alikuwa na umri wa mtu mzima na pia alibatizwa na Yohana Mbatizaji. Marko 1:19 Ikawa siku zile Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya akabatizwa na Yohana katika Yordani. Mathayo 3:13, Mathayo 3:16, Luka 3:21 Maandiko yote haya yanatuthibitishia ya kuwa Yesu Kristo alibatizwa na Yohane Mbatizaji. 

Tuje sehemu nyingine sasa! Kwa nini alibatizwa wakati maandiko yanasema kuwa Yesu Kristo hakuwa na dhambi kwa kuzaliwa na kutenda? Mathayo 3:15 Yesu akajibu akamwambia kubali hivi sasa (kunibatiza) kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali". 

Hapa tunaona kuwa Yesu Kristo ni kielelezo. Hangeweza kusema tubatizwe yeye akiwa mwalimu wetu bila kutupa kielelezo. Sisi tunaomfuata Yesu Kristo tunapokuwa tumebutu dhambi zetu kwa kumaanisha kuziacha na kubatizwa, kule kubatizwa sasa kunakuwa ni kuitikia wito, na pia kuonyesha kivitendo kuwa uamuzi wangu unatoka moyoni au ni wa kufa na kupona. 

Hata hivyo, Yesu Kristo amefanya vielelezo vingi ambavyo tunatakiwa kuvifanya na pia vingine vya kutuonyesha watu wa Mungu siku za mwisho tutakavyofanyiwa. Kufufuka kwa Yesu Kristo pia ilikuwa ni kutueleza kuwa watu wa Mungu siku za mwisho watafufuka katika wafu na kupaa kwenda mbinguni. 1Wathesalomine 4:14-17 Hivyo ni hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye ... sisi tulio hai, tutakaosalia hai wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha lala mauti ... nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai tuliosalia tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana hewani ... 

Kutokana na hayo yote sasa kila mmoja anatakiwa kutenda mapenzi ya Mungu yeye binafsi bila kuangalia mwanadamu mwingine kwa sababu roho itendayo dhambi ndiyo itakayohukumiwa. Ezekiel 18:20 Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa, mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatachukua uovu wa mwanae... " 

Galatia 6:5 Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe". Tukitaka kumpendeza Mungu tusiwaangalie wanadamu walioshindwa, bali tuangalie maandiko yanasemaje na tuyafuate kama yalivyo kama nilivyoeleza hapo awali. Pia hatutakiwi kuyachagua maandiko, kwamba hapa sawa, hapa si sawa pia nasi tutafananishwa na hao walioshindwa kuyafuata kabisa. 

Tukisoma kuwa Mungu yupo, tuamini kuwa Mungu yupo. Tukisoma kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu tuamini hivyo, tukisoma kuwa Yesu ni Mungu inabidi tuamini hivyo, tukisoma kuwa Yesu alikuja kutafuta na kuokoa kilichopotea tunatakiwa tuamini hivyo kuwa Yesu ni mwokozi wetu. 

Kumaanisha kuziacha na kumwomba Yesu atusaidie kushinda dhambi tunatakiwa kufanya hivyo. Pale tunapoona mashaka tuwaulize wale wanaohusika na hicho kitabu wanaoamini wokovu na wanaoamini nguvu ya Roho Mtakatifu akika watatusaidia. Si wote wasemao Bwana, Bwana wataurithi ufalme wa Mungu. 

Bwana Mungu akubariki sana Bwana Muhibu Said na wasomaji wote pia. 

Ni mimi mwenye tumaini la kuja kwake Bwana Yesu kuwanyakua watakatifu wa Mungu. 1 Wakoritho 15: 50 - 54. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
  

Tahari 
Tusirudishane nyuma 

Mwaka mmoja wa mauaji ya Mwembechai: Waliouawa ni wanne
Na Mwandishi wetu

Waasisi wa TAA waibuka kupigania haki zilizoporwa

Kuhujumiwa Waislamu kielimu: Mzazi adai mwanafunzi Adam Rashid kafelishwa

Maoni yetu: Tuondoleeni wenye mikono ya damu

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: MULTIPARAPHILIASIS

Askari wa Tume ya Jiji wapora mkaa

Kuchangia Radio Kheri Broadcasting Station

Yesu Kristo na Yohana Mbatizaji
Na BERNARD B. MWENDA

Wakereketwa CCM wawakosha wauaji wa Mwembechai
Na Idd Kikong’ona, Morogoro

Ufugaji holela wa nguruwe waikumba Dodoma
Na Abu Zubeir, Dodoma

Watembelea na kusaidia wagonjwa Arusha

Mkuu wa wilaya awatimua Masheikh ofisini kwake
Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Kutoka magazeti ya zamani

Sayansi na Teknolojia 
[Windows: Mambo Mazuri ya Kuyajua] 

Masomo ya Kiislam 

Barua za Wasomaji 

Mashairi

Chakula na Lishe 
[Kauli hii ya serikali itatumaliza Watanzania kwa njaa] 

Kumbukumbu ya mauaji Mwembechai 
[Maazimio ya Maimamu Dar]
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita