AN-NUUR 
Na.188 Shawwal 1419, Februari 12 - 18 , 1999 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Kutoka magazeti ya zamani
  
Mawaziri wa Jamhuri mpya nchini watangazwa

Mwafrika Na. 1,224 Jumanne Aprili 28, 1964 

 
RAIS wa Jamhuri ya Tanganyika na Unguja, Mwalimu Julius Nyerere jana alitangaza majina ya Mawaziri watakaotumikia Jamhuri hiyo. 

Mawaziri hao ni kama ifuatavyo: 

Rais: Mwalimu Julius Nyerere. 

Makamu wa Kwanza na Mambo ya Unguja: Sheikh Abeid Karume. 

Makamu wa pili: Bw. Rashid Kawawa ambae pia atakuwa Waziri wa Ulinzi na Ujengaji wa Taifa. 

Mwalimu Nyerere pia atasaidiwa na Mawaziri watatu wa Nchi katika Wizara ya Mipango; nao ni Bw. N. Swai, Sheikh Abdulrahaman Mohamed Babu na Bw. Amir Jamal. 

Kadhalika Makamu wa Rais wa Kwanza atasaidiwa na Waziri mmoja wa Nchi nae ni Sheikh Aboud Jumbe. 

Makamu wa Pili wa Rais nae atasaidiwa na Mawaziri wawili wa Nchi; hao ni Bw. Lawi Sijaona na Bw. Bonke Munanka. 

Mawaziri wengine ni kama hivi: 

Kilimo, Misitu na Wanyama: Bw. Saidi Maswanya. Biashara na Ushirika: Bw. J. Kasambala. Njia na Majengo: Bw. George Kahama. Fedha: Bw. Paul Bomani. Mambo ya Nje: Oscar Kambona. Mambo ya Ndani: Bw. Job Lusinde. Ardhi na Maji: Alhaj Tewa Said Tewa. Viwanda na Migodi: Bw. Kassim Hanga. Elimu: Bw. Solomon Eliufoo. Afya: Bw. Derek Bryceson. Leba: Bw. Michael Kamaliza. Maendeleo na Mila: Sheikh Amri Abedi. Serikali za Mitaa na Nyumba: Bw. Austin Shaba. Sheria: Bw. Hassan Moyo. Habari na Kutalii: Bw. Idirisa Abdulwahid. 

Majina hayo yalitangazwa katika mkutano wa waandishi wa habari, nae baadae Mwalimu alijibu maswali. 

Alipohojiwa kama wafungwa wa siasa walioko Unguja wataachiliwa, Mwalimu alijibu kwamba hata Tanganyika kuna wafungwa wa siasa. 

Alisema pia kwamba ni matumaini ya viongozi wa Jamhuri mpya kuwa muungano huo utakuwa ni kishawishi cha kuleta, sio tu shirikisho la Afrika ya Mashariki, lakini pia Umoja wa Afrika nzima. 


Ukatili usio kifani...
Mgambo wavamia waumini

KILIMANJARO LEO TOLEO LA NOVEMBA 1983 

Na A. Sekajingo  

WANAMGAMBO watatu wa huko Kindi, Kibosho Mashariki katika Wilaya ya Moshi Vijijini wamehukumiwa kulipa faini ya jumla ya Sh. 3,000/- kwa kuvamia na kuwapiga waumini wa madhehebu ya ‘Assemblies of God’ walipokuwa Kanisani wakiabudu. 

Akitoa hukumu hiyo, hivi majuzi, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Kindi, Ndugu E. Massawe, alikieleza kitendo cha walinzi hao wa mgambo kuwa ni cha ‘ukatili usio na kifani’. 

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani wanamgambo hao Sebastian Mikari (45), Aloyce Eugen (25) na Joseph Mohamed (36) walikivamia kikundi cha waumini hao wakiwa na Mchungaji wao, Paulo Mboya usiku wa Septemba 9 na kuwalazimisha ‘kuruka kichura’, kubebana na kufanya mazoezi mengine magumu ya kijeshi. Waliwabebesha mawe mazito na kutishia kuwauwa. 

Ilidaiwa pia kuwa waumini hao walimwagiwa maji baridi ya bomba, kupigwa na boriti na kulazimishwa kunywa pombe kinyume na imani ya dini yao. Visa hivi viliendelea hadi asubuhi kuanzia saa tano usiku. 

Hakimu pia aliamuru washitakiwa kutotenda kosa lolote katika kipindi cha mwaka mmoja na kulipa fidia ya juma ya Sh. 1,000/- kwa waumini wawili - Sebastian Peter na Stephen Koyanga ambao waliwaumiza na kusababisha majeraha makubwa miilini mwao. 

Katika hukumu yake, Masawe alisisitiza kuwa kwa kuwafuata waumini hao walipokuwa wakiabudu Kanisani mwao na kuwatoa nje na kuwatesa, wanamgambo hao walifanya kosa kubwa sana. 


Kesi ya maasi imeanza

Mwafrika Na. 1,224, Jumanne Aprili 28, 1964 

SIKU moja kabla ya maasi ya askari jeshi kutokea baadhi ya askari fulani walijiunga katika kikundi. Kikundi hicho wakakiita kikundi cha ‘wagombea uhuru’. Kisha wakati wa saa 11 jioni walitoka kwenye kambi yao wakaenda kwenye kichaka karibu na Mbezi wakafanya mpango wa kuwakamata maofisa wao wa Kizungu na hatimaye kuwasafirisha hadi makwao. Korti ya kijeshi iliambiwa leo. 

Mkurugenzi wa mashitaka katika Jamhuri ya Tanganyika, Bwana Wilbert Chitepo alipokuwa anafungua mashitaka ya uasi yanayowakabili askari jeshi 19, aliiambia korti hiyo kwamba kikundi hicho baada ya kukubaliana juu ya mpango huo kilirudi kambini kwao. Kukiwemo baadhi ya washitakiwa kikundi hicho kilianza kuwashawishi askari wenzao washiriki katika mpango wao. 

Bw. Chitepo aliendelea kueleza kuwa zilipotimu saa sita za usiku wa siku hiyo (Januari 19) walianza kutimiza mpango wao baada ya wale askari waliwashauri kukubali. 

Mbele ya Jaji Mkuu wa Tanganyika, Justice Ralph Windham walikuwa wamesimamishwa askari hao 19 ambao wanashitakiwa kwa makosa ya kufanya maasi mnamo Januari 20. Askari hao waliingizwa kortini humo wakiwa wamevaa mavazi yao ya kijeshi baada ya kusomewa mashitaka waliyakanusha. ‘Sikubali mashitaka bwana mkubwa’, ndivyo ilivyokuwa kila mmojawapo alivyokuwa akisema. 

Washitakiwa wote wanatetewa na Mabwana Adrian Roden, Homi Udvandia na N. M. Kassam. Kwa upande wa Jamhuri ni Mabwana W. Chitepo, A. Troup na Fredick Rutakyamirwa. Baada ya maelezo ya mashitaka kutolewa na Bw. Chitepo kesi iliahirishwa mpaka leo (Jumanne) saa tatu asubuhi. 

Mapema wakati akiendelea kutoa maelezo, Bw. Chitepo alisema kuwa katika kuutimiza mpango wao walianza kukamata maofisa wao waliokuwa kazini siku ile kati yao alikuwa ni ofisa anayesimamia stoo ya silaha. Baada ya kumkamata walimfungia stoo na wakatoa silaha. Kwa kuwa walikuwepo maofisa wengine ambao walikuwa wamo majumbani mwao karibu na kambi, askari hao walifanya ujanja wa kuwakamata kwa urahisi. Walizimisha taa zote kambini na wakaanza kupuliza tarumbeta. Kusikia tarumbeta inapigwa maofisa wakaja kutazama kuna nini. Wakawatia nguvuni na wakawafungia mahali fulani. 

Bw. Chitepo aliendelea kuwa baada ya hapo walijigawa katika vikundi. Wakaja mjini wakawakamata maofisa wa vituo vya polisi kwa kuwatishia na bunduki, kisha wakateka ofisi za Posta, T.B.C., Uwanja wa Ndege na mwisho Jumba la Serikali. 

Walitembeatembea katika mabarabara ya mji wakawa wanawatisha watu. Walinyang’anya magari ya watu kwa nguvu na wakawatishia wakuu wa vituo vya mafuta ya petroli wakiwa wanajaza mafuta bure katika magari yao. 

Bw. Chitepo aliielezea korti kuwa hasara iliyopatikana kwa kutokana na vituko vya askari hao haiwezi kukadirika. Akasema watu waliuliwa na maduka ya matajiri yakavunjwa na mali nyingi ikaibiwa. 

Bw. Chitepo aliendelea kuwa kutokana na vituko vya askari hao taifa zima lilikuwa na hofu kubwa wakati wa siku hiyo. Mpaka saa za jioni, akaendelea, askari hao hawakuweza kuacha uasi huo na ilionekana kana kwamba nia yao ilikuwa ni kuiangusha serikali. 

Kosa lastahili kifo 

Akasema Bw. Chitepo ‘askari hao walikuwa ni walinzi wa kuilinda serikali. Kosa walilolitenda ni kubwa sana ambalo linastahili adhabu ya kifo. Watu hawa 19 walishiriki katika maasi na wakalitia taifa katika aibu’. 

Bw. Chitepo alimwambia Jaji Mkuu Windham kwamba askari hao mapema walipojigawa katika vikundi huko kambini, kundi la watu kati ya 22 na 23 liliamuriwa kwenda kwenye Jumba la Serikali. Walipokwenda huko wakamtafuta Rais lakini hawakumuona. Hapo baadhi yao wakaendea kumkamata Bw. Kambona kwenye nyumba yake. 

Hawawezi kumwachia 

Kufika huko wakamkuta na kumkamata. Akapelekwa kwenye Jumba la Serikali. Huko wakamwambia kwamba maofisa wote wamekwishakukamatwa. Wakasema hawataweza kumwachilia ikiwa hakuwatimizia madai yao. Wakamchukua kambini kwao na kumueleza madai yao hayo. 

Bw. Chitepo alisema kwamba madai hayo yalikuwa kwamba maofisa wote wasafirishwe makwao. Kianzio cha mshahara kiwe shs 250. Askari wanapomaliza mafunzo apewe mshahara wa Shs 260 na nyongeza iwe Sh 5 kila mwaka. 

Isitoshe waendapo livu wapewe waranti ya serikali na mavazi yao yageuzwe. Bw. Kambona, akasema, aliwaambia wawachague watu wanaowaamini waende kwa Rais wakajadiliane juu ya madai yao. Wote wakasema ‘sote twende ni waaminifu’. Hatimaye walimteua Bw. Havana na Sajini Francis Hingo ambaye Bw. Chitepo alisema ndiye aliyekuwa kiongozi wa madai yao. 

Walikwenda hadi State House. Bw. Kambona akaingia ndani kisha baadaye akatoka na kuwaambia kuwa Rais amekubali madai yao. Bw. Chitepo akasema askari walikubali na wakaondoka. Bw. Kambona aliporudi kambini aliwachagua Wazungu akakubaliana nao wasafirishwe makwao. 

Lakini, akasema, alipowashauri kwamba maofisa hao waruhusiwe kubadilisha nguo zao, wakakataa. 

Akarudia upande wa vile vikundi ambavyo alisema vilikuwa vikitembeatembea barabarani. Bw. Chitepo alisema kuwa katika maduka yaliyovunjwa upo ushahidi utakaothibitisha kwamba baadhi ya washitakiwa ndio walioyavunja wenyewe na kuwaambia watu waanze kuiba vitu. 

Kamuua Mwarabu 

Kisha akaielezea Korti jinsi askari hao walivyomuua Mwarabu mmoja pamoja na jamii yake baada ya Mwarabu huyo kumpiga risasi askari mmoja wakati alipokuwa anatetea duka lake. 

Mpaka wakati wa jioni, akasema askari hao walikuwa wangali wanaendelea kufanya vitendo vibaya, Bw. Chitepo akaielezea korti jinsi baada ya siku mbili askari hao walivyokataa kuachilia silaha wakati walipoombwa kufanya hivyo na wakuu wa serikali. 

Akamaliza maelezo yake kwa kusema ‘washitakiwa walijichukulia silaha wao wenyewe, wakawakamata maofisa wao, na wakashiriki katika maasi. Kushiriki katika mojawapo ya makosa haya kwa mtu ambaye ni askari jeshi anastahili adhabu ya kifo kwa mujibu wa sheria ya korti za kijeshi’. Kesi itaendelea leo. 


Bw. Hanga kaenda Nairobi

Ngurumo Na. 1,566 Jumanne, Mei 20, 1964 

BWANA Kassim Hanga, Waziri wa Viwanda, Madini na Umeme katika Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar, jana usiku aliondoka Dar es Salaam kwa ndege kuelekea Nairobi, ambako atahudhuria kufunguliwa kwa Baraza Kuu la Afrika Mashariki leo. 

Bwana Hanga alipoondoka jana, alifuatana na Bwana A. J. Nsekela wa Wizara yake. Wajumbe wengine wanaouwakilisha Muungano wa Jamhuri ni Waziri wa Bwana Bomani, Waziri wa Leba, Bwana Kamaliza, Waziri wa Mambo ya Nchi katika Ofisi ya Rais, Bwana Amir Jamal, Waziri wa Uchukuzi na Kazi, Bwana Kahama, ambaye amefuatana na Waziri Mdogo katika Wizara ya Leba, Bwana Baghdelleh. 


Jen. Amin atua Mwanza

Uhuru, Na. 2,849 Jumanne, Oktoba 30, 1973, bei senti 25, Kenya senti 30 

Na Joe Masanilo, Mwanza

JENERALI Idi Amin wa Uganda aliwasili mjini Mwanza juzi mchana na kufanya mazungumzo ya saa tatu hivi na Mwalimu Nyerere pamoja na Rais Kaunda wa Zambia na Rais Mobutu wa Zaire katika Ikulu ndogo. 

Hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusu mazungumzo hayo isipokuwa inaaminika kwamba licha ya mambo ya ujirani mwema, Jenerali Amin aliwaeleza viongozi wenzake juu ya hali ilivyo katika Mashariki ya Kati. 

Jenerali Amin alifanya ziara katika nchi kadhaa za Kiarabu mara tu vita vilipozuka hivi majuzi. 

Zaire, Tanzania na Zambia zimekwishavunja uhusiano na Wayahudi kwa sababu ya siasa zao za uchokozi kwa Waarabu. 

Ingawa kuwasili kwa kiongozi huyo wa Uganda hakukutangazwa mapema, wananchi wengi walikuwepo barabarani kumsalimu wakati akitoka kiwanja cha ndege baada ya kupokewa na Mwalimu Nyerere. Makundi ya watu yaliongezeka barabarani na kiwanjani wakati Jenerali huyo alipokuwa akiondoka juzi hiyo hiyo jioni kwa ndege ya jeshi. 

Kabla ya kufika kwake, Mwalimu Nyerere na wageni wake walifanya mazungumzo ya faragha na viongozi wa wapigania uhuru wa Angola, Bwana Holden Ruberto na Bwana Augustino Neto. Bwana Roberto mwenye maskani yake huko Kinshasa, Zaire aliwasili mapema asubuhi na Bwana Neto alifika na ndege maalum kutoka Dar es Salaam saa tano asubuhi. 

Juu 
 

YALIYOMO 
  

Tahari 
Tusirudishane nyuma 

Mwaka mmoja wa mauaji ya Mwembechai: Waliouawa ni wanne
Na Mwandishi wetu

Waasisi wa TAA waibuka kupigania haki zilizoporwa

Kuhujumiwa Waislamu kielimu: Mzazi adai mwanafunzi Adam Rashid kafelishwa

Maoni yetu: Tuondoleeni wenye mikono ya damu

MARADHI YA KISAIKOLOJIA: MULTIPARAPHILIASIS

Askari wa Tume ya Jiji wapora mkaa

Kuchangia Radio Kheri Broadcasting Station

Yesu Kristo na Yohana Mbatizaji
Na BERNARD B. MWENDA

Wakereketwa CCM wawakosha wauaji wa Mwembechai
Na Idd Kikong’ona, Morogoro

Ufugaji holela wa nguruwe waikumba Dodoma
Na Abu Zubeir, Dodoma

Watembelea na kusaidia wagonjwa Arusha

Mkuu wa wilaya awatimua Masheikh ofisini kwake
Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Kutoka magazeti ya zamani

Sayansi na Teknolojia 
[Windows: Mambo Mazuri ya Kuyajua] 

Masomo ya Kiislam 

Barua za Wasomaji 

Mashairi

Chakula na Lishe 
[Kauli hii ya serikali itatumaliza Watanzania kwa njaa] 

Kumbukumbu ya mauaji Mwembechai 
[Maazimio ya Maimamu Dar]
 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita