AN-NUUR
Na.154 Safar 1419, Juni 19-25, 1998
 
Home 

Links 

Islam Tanzania 

Matoleo ya nyuma 
 
 

Pole ya Mwinjilisti Kusupa ni kejeli 

TOLEO Na. 152 la ANNUUR lilichapisha makala ya Mwinjilisti Kamara Kusupa yenye kichwa cha habari "Poleni Ndugu zangu Waislamu, Ibilisi hana Rafiki". Hili ni jibu la makala hayo. 

Katika makala hii yenye jibu kwa Mwinjilisti Kusupa, sikusudii kujibu kila hoja iliyomo ndani ya makala yake kwa vile baadhi ya hoja zake ni zile zenye kejeli, ufyosi na zisizo kuwa na uzito wala mantiki. Kama ile ya kulinganisha Waislamu na Wakristo kama wakewenza wanaooneana wivu na nyinginezo. Nimewaachia wasomaji wengine watoe mchango wao. 

Makala hii itashughulika na kudhihirisha upogo wa dhana mbalimbali alizonazo Mwinilisti Kusupa juu ya mambo mengi ambayo haelekei kuyafahamu. 

Pia itafafanua mambo kadhaa kwa ajili ya kuwasaidia wasomaji wengine kuelewa vyema dhana za kitaalamu alizojaribu kuzilaumu Mwinjilisti Kusupa. Vilevile itaweka wazi sera ya Waislamu kuhusu madai yao na sera za Kanisa ambalo Mwinjilisti Kusupa anazitumikia. Mwisho kuishauri serikali kuchukua hatua za makusudi kabisa kuwajibika katika kuitikia kilio cha Waislamu ili kurekebisha hali hii isiyo-wiana baina ya Waislamu na Wakristo mkabala na suala la haki zao. 
Na Ustadh A.S. Fundi 

DHANA POTOFU 

Picha ya Ibilisi kama ilivyochorwa na Mwinjilisti Kusupa, namna anavyomgeuza mwanadamu kama kontena na kisha kumtumia kueneza ubaya duniani na kila aina ya udhalimu inawasilisha dhana zinazofundishwa na Makanisa ya Kikristo. Makala ya Mwinjilisti Kusupa haikutufahamisha mafunzo ya Biblia jinsi ya kumwepuka Ibilisi, mwovu na mashawishi wa mwanadamu. 

Wala haikutupa mbinu za kupambana na ayari huyu anayedanganya walimwengu. Ametuacha kwenye mataa kwa kuishia tu kutaja namna anavyoweza kulikalia Taifa na viongozi wake na kuwafanya chombo cha ukiukaji haki za binadamu, kuendesha mauaji ya raia wasio na hatia, kufanya ubadhilifu wa mali ya umma na kusambaza ufisadi wa kila namna. 

Picha hii ya Ibilisi ni dhana potofu kabisa. Picha hii ni picha ya kutukatisha tamaa. Hii ni dhana ya kukata tamaa na kukosa msaada wa Mungu Muumba. Dhana hii inamfanya mtu asijue la kufanya, wala asijue namna ya kumkimbia Ibilisi ili awe mwema, atendee haki raia wake, awe mwadilifu, mkweli na awajibike. Yaonyesha Bibilia haina jibu la kuponya maradhi haya ya nafsi. 

Dhana ya namna hii inatutaka tuamini kuwa Ibilisi ana nguvu za ajabu na za kimiujiza na hawezi kuepukika. Hivyo tukiikubali itatupelekea kuamini kuwa ni Ibilisi aliyemwamrisha Paroko kuitaka serikali idhibiti mihadhara ya Waislamu, na ni Ibilisi aliyemwamrisha Mheshimiwa Yusufu Makamba kutoa amri ya kuuvamia Msikiti wa Mwembechai kwa silaha za moto, na ni Ibilisi aliyemwamrisha Kamanda wa Polisi kutoa risasi za moto kuwapa askari na kisha kutoa amri kwa Makostebo kuwapiga risasi raia Waislamu wasio na silaha. 

Pia ati ni Ibilisi aliyemwamrisha Hakimu kuwanyima dhamana Waislamu lakini awape dhamana Wakristo walioshitakiwa kwa kosa kama la Waislamu. Na mlolongo wa maonevu yote dhidi ya Waislamu. Hii ni dhana potofu kabisa. 

Mafunzo kama haya yakienea na kustawi katika nyoo za watu, itaondoa ile hisia adhimu ya uwajibikaji, ukweli na uwazi ambayo ni sera ya serikali ya wamu ya tatu. 

Ama Qur'an Takatifu ina mafunzo yaliyo wazi kabisa juu ya huyu Ibilisi. Qur'an inasema Ibilisi ndiye huyu shetani alikwisha laaniwa na Mungu Muumba, Allah (sw). Na kwamba ni adui mkubwa wa kutia wasiwasi katika nafsi ya mwanadamu. Lakini Qur'an Takatifu haishii hapo tu, bali inasema kuwa uwezo wa Ibilisi au Shetani haumgusi mtu mwenye imani na Istiqama (msimamo) thabiti. Tunasoma hayo katika Qur'an, sura 16:99 kuwa "Hakika yeye (Ibilisi) hana nguvu juu ya wale walioamini na wanaomtegemea Mola wao". Na kwamba S 

thabiti. Tunasoma hayo katika Qur'an, sura 16:99 kuwa "Hakika yeye (Ibilisi) hana nguvu juu ya wale walioamini na wanaomtegemea Mola wao". Na kwamba Ibilisi ana nguvu juu ya wale wanaomkumbatia na kumfanya ni mwenza wao mpenzi. Qur'an sura 16:600 inasema: "Nguvu zake ni juu ya wale wanaomfanya rafiki (wakamfuata) na juu ya wale wanaomshirikisha (Allah) naye". Lakini pia siku ya kiama (siku ya hukumu), Ibilisi atawakana waliokuwa wanamfuata. Qur'an inasema: "Ibilsi atasema itakapokatwa hukumu (atawaambia wale watakaomng'ang'ania) Allah aliwaahidini ahadi ya kweli ( na ameitimiza), mimi nilikuahidini lakini sikuitimiza (ahadi yangu) wala sikuwa na mamlaka juu yenu (ya kukulazimisheni) isipokuwa nilikuiteni tu nayi makaniitika. Basi msinilaumu bali jilaumuni (nafsi zenu) wenyewe, siwezi kukusaidieni wala ninyi hamwezi kunisaidia". Sura 14:22. 

Kwa nini iwe hivyo naye Ibilisi alikwishapewa ruhusa ya kuwapoteza wanadamu? Jibu ni kuwa Allah (sw) alikwisha sema kumwambia Ibilisi aliyekataa kumsujudia Nabii Adamu zama alipoumbwa (huyo Adamu) kuwa: "Waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu yao, isipokuwa wale wenye kukufuata (kwa hiari zao) katika hao wapotovu". Sura 15:42. 

Maelezo haya yanatosha kutufahamisha kuwa kila mwanadamu anawajbika kwa imani yake na vitendo vyake. Anao uhuru kamili wa kutenda mema au mabaya kwa hiyari yake na dhamira yake ndiyo itakayohukumiwa siku ya Kiama. Wa kulaumiwa hapa siyo Ibilisi bali mwanadamu mwenyewe. 

Hii ndiyo dhana sahihi, na ilienea na kushamiri itamfanya kila mmoja wetu kuwajibika kwa kila ovu alitendalo. Na akitenda jema atapongezwa yeye binafsi, wala sio malaika anaofuatana nao. Hivyo basi viongozi wa serikali na wasimamizi wa vyombo vya dola wanapowadhulumu haki zao Waislamu hawanabudi kulaumiwa waziwazi na moja kwa moja wala sio Ibilisi asiyeonekana. 

Mwinjilisti Kusupa anamlaumu Mohamed Said kwa kuandika makala isiyokuwa na hitimisho na anasema hali hiyo inamfanya msomaji mwenye makini ashindwe kumuelewa mwandishi anakusudia nini au lengo lake ni lipi. Hoja hii ni dhaifu kwani inadhihirisha upeo mfupi wa kuatikali na uchovu wa haraka wa akili kushindwa kufuatilia hatua kwa hatua maelezo sawia kama yanavyosukwa na Mwandishi aliyebobea. 

Mtindo wa uchambuzi wa Mohamed Said wa kuchambua mada kwa kina kirefu na kumwacha msomaji awe huru kutoa majibu au hitimisho analoona ni mnasiba kwa mujibu wa makala aliyosoma, ni mtindo maalum kati ya mitindo mingi ya uandishi. 

Msomaji atakayeshindwa kumwelewa Mohamed Said hawezi kuitwa msomaji makini. Kwani sifa ya msomaji makini ni utulivu wa mawazo na akili, na mwenye uzingativu wa kile anachokisoma. Na ni msomaji wa sifa hizi ndiye awezaye kutoa hitimisho la kweli la makala hiyo au kuweza kutoa majibu sahihi yanayojitokeza katika makala husika. 

Katika fani ya uandishi, mwandishi mweledi yu huru kutumia mtindo anaofikiri kuwa utasaidia kufikisha ujumbe kwa dhamira iliyokusudiwa. Mtindo wa mtiririko wa maelezo unaokwenda hatua kwa hatua hadi mwisho (sequential method) ni mtindo wa kawaida ulio mwepesi kueleweka na msomaji yeyote, ni aina ya kwanza ya uandishi. Aina ya pili ni mtindo wa kuyataja na kuyaeleza matukio kwa mujibu wa nyakati za matukio hayo mwanzo hadi mwisho (chronological method). Aina ya tatu ya uandishi ni mtindo maalumu unaohusisha mambo na matukio au vitu kwa mujibu wa nafasi inayokaliwa na wahusika (special order method). Au ule wa mtindo wa nne, wa kutoa maelezo ya nukta kisha nukta ya pili hadi mwisho, maelezo ambayo huwa ni hoja au sababu za nukta hizo, vivyo hivyo hadi mwisho wa makala (cause and effect method). 

Huu mtindo wa nne ndio anaoutumia Mohamed Said ambao humpa msomaji kila aina ya taarifa na hoja kisha humwacha msomaji mwenyewe achekeche na apembue uzito wa hoja hizo na kutoa hitimisho munasiba. 

Aghlabu huu ndio mtindo unaotumiwa na wataalamu wa fani mbalimbali hasa wanafalsafa wa sayansi ya jamii kila wanapoandika insha za kisomi au taarifa za kiakademia. Lakini kama unamwandikia mwanafunzi wa darasa la saba, kidato cha pili au kidato cha nne huna budi kumwekea hitimisho bayana ili asije changanyikiwa na kupoteza lengo. Na ipo mitindo mingine ya kuandishi katika fani ya fasihi andishi ambayo mwandishi anaweza kutumia. 

Waislamu wanapodai kuwa wamenyimwa elimu, Mwinjlisti Kusupa anasema huku ni kujifananisha na Wakristo wachache waliosoma badala ya kulinganisha na Wakristo wengi wasiosoma. Hili si sahihi. Na hata kama tukijaalia kuwa idadi ya Wakristo ni sawa na idadi ya Waislamu nchini bado hakutokuwa na uwiano sawia wa kiidadi. Bado idadi ya Wakristo waliosoma itakuwa ni kubwa kuliko ya Waislamu walionyimwa elimu. Lakini hali halisi sivyo ilivyo. 

Kwa mujibu wa Idara ya habari na Idara ya Takwimu (1981) na ambazo tayari zilikwisha tolewa na gazeti hili katika safu za matoleo ya nyuma, idadi halisi ya Waislamu nchini, kwa mujibu wa makadirio ya wataalamu ni zaidi ya asilimia 60%. Ambayo idadi ya Wakristo wote ni asilimia 30% na ya wasiokuwa na dini hizi mbili ni asilimia 10% tu. Ukizingatia hilo bado idadi ya Waislamu walionyimwa elimu itapita kwa kiwango kikubwa na asilimia, idadi ya Wakristo wasiosoma na vivyo hivyo idadi ya waliosoma ya Waislamu na ya Wakristo. 

Na hao akina Matonya na Ndyanao wa Ugogoni aliowataja Mwinjilisti Kusupa na wale akina Ole-Parsalau na akina Nabulu wa Umasaini waliokosa elimu idadi yao haiwezi kulingana na idadi ya akina Khamis na Khadijah alionyimwa elimu kwa zaidi ya miaka 35 ya uhuru wa Tanzania. 

Na hasa ukizingatia kuwa mchango wa Waislamu katika kudai uhuru ni mkubwa zaidi ya watu wengineo. Hivyo mlinganyo wa Mwinjilisti Kusupa ni hasi na ni seti tupu kwa maana takwimu zote za rekodi za kielimu serikalini hazimuungi mkono. 

Historia ya maendeleo ya elimu nchini inaonyeshwa na waandishi wengi wataiti kuwa, shule nyingi, vikiwemo vyuo mbalimbali, zilizojengwa na kuendeshwa na Makanisa, ziliweka mazingira yenye mfumo wa maadili ya Kikristo. Ambapo zilikuwa zikiwalazimisha wanafunzi wote humo kufuata ratiba na mfumo wa mitaala bila kujali dini zao. 

Makanisa ya Kikristo yaliweza baadaye, kama wafanyavyo sasa; kuwa yamesaidia kuelimisha kwa ngazi moja au nyingine; idadi kubwa ya watu waliokuja kushika uongozi wa chama na serikali. Dr. Sivalon (1992). 

Mfano mzuri ni Chuo cha "Marian College" kilichojengwa na Kanisa Katoliki ili kuelimisha Masista na wasichana (wateule) hadi kidato cha nne zama hizo. Na Chuo hicho kilipewa kipaumbele sana na Kanisa, maana kiliteua wanafunzi wenye viwango vizuri vya alama katika mitihani yao. Matayarisho ya wanafunzi yalikuwa ya hali ya juu kabisa kiasi kwamba wanafunzi waliofaulu vizuri kati ya mwaka 1961 _ 1965 waliweza kupewa nafasi kama ifuatavyo: Wawili walikwenda kusomesha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tisa walipata nafasi ya kama walimu shule za Sekondari, na miongoni mwao watatu waliteuliwa kuwa viongozi wa mikoa, mmoja ngazi ya taifa, na mmoja kuwa daktari na mwingine akateuliwa kuingia katika Baraza la Maaskofu (TEC). Dr. Sivalon (1992) Uk. 27-28, 34, 40, 43, 44, 49 na 61. 

Wakoloni wakiwemo Wajerumani na Waingereza hawakuyaruhusu Makanisa kujenga na kuendesha shule, hospitali na taasisi za kijamii kwa sababu kama asemavyo Mwinjilisti Kusupa katika hoja yake ya kuyasifu Makanisa. Bali ukweli ni kwamba kama Makanisa ndiyo yalikuwa ya kwanza kufika Tanganyika na kuanzisha shule hayangepinga kuja kwa wakoloni kutawala kwani ndani ya uongozi wa serikali ya kikoloni walikuwamo wakereketwa wa karibu wa Makanisa. Vivyo hivyo usingalitarajia wakoloni kupinga Makanisa kuanzisha shule kwa sababu wote walikuwa na lengo lile lile la "kustaarabisha washenzi". Wakoloni ni Wakristo wakereketwa tangu zama hizo nao ni kama tui na maziwa baina ya wakoloni na Makanisa katika azma zao. 

Mfumo wa mitaala inayohusisha Ukristo na mazingira yanayozingatia utamaduni wa Kikristo uliwaathiri sana Waislamu wachache waliopata nafasi ya kusoma katika shule za Makanisa. Shule hizo kila moja ilikuwa na Kanisa dogo na yapo hadi leo. Hatuna nafasi yakutaja majina yao. 

Athari hiyo ni ile iliyowalazimisha Waislamu kufanya mitihani ya Elimu ya Biblia _ masomo ambayo yalisugua vichwa cha watoto wa Kiislamu. Na kwa kukosa hoja za utetezi dhidi ya mafunzo ili wapate nafasi za masomo ya juu. Ndiyo maana leo tuna akina Sylvester Hassan, Charles Omar, George Ally, Daniel Ramadhani, Robert Haji na wengineo wengi sana. Kwa kukubali kuuza dini yao ya Kiislamu wakapewa nafasi za masomo vyuo vikuu na nchi za nje na waliporejea wakapewa nafasi za uongozi katika ngazi za juu serikalini na katika taasisi za umma. 

Shule kama hizo hadi leo zipo Mombo, Same, Handeni na mikoa mingineyo. Lakini wale ambao hawakukubalika kiimani walikosa mwelekeo wa Uislamu sahihi na wala hawakuwa na elimu "Tauhiidi (upweke wa Allah). Hadi leo utawaona hawana athari ya Uislamu wala istiqama (msimamo thabiti). 

Itaendelea toleo lijalo. 
 
 

 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI  

Maoni yetu: 
Kama hodari wa kuhoji Tuhoji pia Tume ya Majeshi ya Vita 

Waraka wa Abu Aziz  

Unafiki si suala la wakati fulani  
  
Wakatoliki wawili wasilimu 

Ashitakiwa baada kusilimu 

Historia ya harakati za ukombozi wa Kashmir 

Sheikh wa Wilaya Same ahimiza Waislamu kushiriki tamasha 

Sheikh awataka wanawake wajistiri 

Madrasat Al-Hujuun washerehekea mwaka mpya 
 
Kutoa talaka ovyo ovyo ni kuchupa mipaka ya Allah - Ust. Khamis Salim 

Uislamu ni mfumo wa maisha - Mbukuzi 

Pole ya Mwinjilisti Kusupa ni kejeli 
 
 

 

 
 Maoni yoyote kuhusu ukarasa huu yapelekwe kwa: islamtz@wowmail.com
 
An-nuur Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita