AN-NUUR 
Na.172 Rajab 1419, Oktoba 23 - 29, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Inawezekana kufanyika mdahalo kati ya Waislamu na wasio Waislamu?
Na Nandenga wa Mkomidachi

Uislamu na Ukristo ni dini mbili zenye wafuasi wengi hapa nchini na ulimwenguni kwa ujumla. Si idadi kubwa ya watu isiyohusiana na moja ya makundi hayo. Ni hakika kuwa katika baadhi ya mambo ya msingi dini hizi "hukutana" japo utekelezaji haulingani. Kiasili, maandiko yanazirejesha kwenye umoja. Ni desturi, mazoea au "upotoshaji" baadaye ndiyo uliozaa uwili huu. Vile vile zipo tafauti zinazofanya kila moja kati ya hizo ichukue "mkondo wake" ingawa zote zina maelezo yanayoashiria kuwa na hatima moja. Mawili haya ndiyo yanayoibua uwezekano wa mijadala. Katika kulijadili hili Mwandishi wa makala haya amejenga hoja ya hitajio la mijadala ya kidini Tanzania lakini akipendekeza kuzingatiwa masharti na busara fulani. Amedokeza utayari wa Muislamu kimaandiko katika hilo. Kisha amejaribu kutoa tafsiri ya istilahi na dhana muhimu zinazotumika ndani ya Uislamu, wakati huo huo akisahihisha maeleweko potofu juu ya hayo. Mwisho ametoa mapendekezo yake. Fuatilia uchambuzi huu makini... 

Shukrani zote anastahiki Allah, Muumba na Mlezi wa Vyote. Nashuhudia kwamba hapana Mola ispokuwa Allah na Muhammad ni Mjumbe wake na hitimisho (Khatam) la wajumbe wa Allah katika Historia ya Mwanaadamu. 

Kuzungumzia suala la mdahalo, mhadhara au mazungumzo baina ya Waislamu na wasio Waislamu Tanzania, maana yake kwa sehemu kubwa, ni kuzungumzia masigano au mafanano ya fikra za kidini kati ya Waislamu na Wakristo. 

Midahalo ya makundi mengine yote inahusisha wachache na inafuata baada ya huo. Si Tanzania tu bali kiulimwengu suala hili linaangaliwa hivyo pia. 

Ni hakika iliyowazi kwamba zaidi ya asilimia 40 ya Walimwengu, kwa kiasi kikubwa, matendo, matashi na tafakuri zao zimeathiriwa na dini hizi mbili, yaani Uislamu na Ukristo. Kila moja kati ya hizo ina wafuasi wanaokisiwa kufikia bilioni moja. Zipo tofauti nzito tu za kitheolojia kati ya dini hizo.Halikadhalika yapo maeneo ya kiimani ambayo wanajamii wa makundi hayo hukutana. Kwa mfano imani ya kuwepo Mungu Muumba, imani ya ufunuo, Mitume, Vitabu Vitakatifu, maisha baada ya kifo na ulazima wa kufuata mwongozo kutoka kwa Muumba wa namna ya kuendesha maisha ya kila siku katika kipindi hiki cha maisha ya mpito ya dunia katika safari ndefu kuelekea maisha ya milele. 

Hivyo, nidhahiri kwamba kukutana huku katika mambo ya kiimani ndio asili ya mijadala baina ya wafuasi wa dini hizo. Halikadhalika zipo tofauti za msingi kati yao. Hizi nazo ni chokoo za mijadala. Isingalikuwepo haja ya midahalo kama pasingalikuwepo na kuwiana, tofauti, khitilafu, upinzani na migogoro baina ya makundi hayo mawili. 

Waislamu wanaweza kuwa na majadiliano na Wakristo? 

Muislamu yuko huru kufanya mdahalo au majadiliano jenzi (constructive dialogue) na yeyote yule. Lakini suala hapa ni, mdahalo juu ya nini na nini hatima yake. 

Muislamu yuko huru kujadiliana kwa kuwa ruhusa na mahimizo yashatolewa na Qur’an. Si hivyo tu na hata mbinu za kuendea majadiliano hayo zimeelekezwa vyema ndani ya Qur’an. Katika Qur’an tunajifunza ifuatavyo:- 

Sema: Enyi watu mliopewa kitabu! Njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu; ya kwamba tusimwabudu yoyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe (Mwenyezi Mungu) na chochote; wala baadhi yetu tusiwafanye wengine kuwa waungu badala ya Mwenyezi Mungu. Wakikengeuka; Semeni: "Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu tumenyenyekea kwa Mwenyezi Mungu (3:64). 

Yapo mengi ya kufikiria kuhusiana na suala hili. Na vile vile upo upogo na khitilafu za kujihadhari kwazo. Yote mawili hayo na hasa hili la khitilafu, hutokana na desturi na mazoea kiutendaji. Inaaminika hali hizo mbili nazo ni matokeo ya ukiukaji matendo sahihi. 

Kwa hili, Waislamu wamekuwa wakihoji mambo kadhaa kama vile ni kwa vipi wanaadamu wapeane utakatifu wao kwa wao. Vile vile wanahoji baadhi ya mambo ndani ya Uislamu wenyewe; kama vile ni vipi jumuiya au Baraza fulani kuhodhi madaraka na kuwakalia waumini wote. 

Maswali na kuhoji huko pia hutoa fursa ya mijadala na hasa pale inapoonekana haja ya kujadili suala fulani kwa kina. Kadri kila kundi linavyozama na kuipa uzito khitilafu fulani ndivyo jamii inavyoselelea katika migogoro na ukinzani. Hapana budi kuwepo na mijadala ya wazi,inayozingatia ukweli, isiyo na upendeleo wala chuki zisizo na msingi baina ya makundi. Hata hivyo mihadhara ya hivi sasa haina sura wala muelekeo huu. 

Labda ikumbushwe kwamba utaratibu mzuri wa kujadiliana unaelezwa vyema katika Qur’an. 

"Waite (watu) katika njia ya Mola wako kwa hikima na mauidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyobora. Hakika Mola wako ndiye Anayemjua aliyepotea katika njia yake. Naye ndiye Anayewajua walioongoka. (16:125)." 

Pengine ingepaswa sasa kuweka masharti fulani ili kupatikane mihadhara au majadiliano yenye kuchukua sura hiyo. 

Muhimu hapa ni kwamba makundi ya waumini yasifundishane kupitia mambo yanayokera, ukosoaji usio wa lazima, kashfa, rejea potofu, kuchokozana na kukejeliana. Kimatendo, kwa mfano, itakuwa ni balaa, na kwa hakika ni kejeli, kwa yeyote yule anayetaka kuujua uhindu wa India aende kujifunza itakadi hiyo kwa Muislamu wa Pakistan, na kinyume chake. Vivyo hivyo, itakuwa si busara kwa yule anayetaka kujua jambo fulani la Uislamu kwenda kujifunza kwa Mustashrikiin au mwingine mfano wa huyo. 

Nukta ya msingi hapa ni kwamba jamii zote mbili zijaribu kuonyesha kwa waumini jinsi zinavyopaswa kuaminiwa; kutoka vyanzo sahihi na mifano ya kiutendaji kutoka kwa waumini wa kweli. 

Haja ya majadiliano na mbinu bora za uendeshaji wa majadiliano hayo ni kubwa na inahitajika zaidi Tanzania ya leo kuliko wakati mwingine wowote. Haja hiyo inatokana na ukweli kwamba wengi wa wale wanaoitwa wasomi wa Tanzania hivi leo, wanafahamu machache kuhusu Uislamu na wamejifunza hayo kupitia mashule na waandishi ambao kwa kiasi kikubwa walisukumwa na sera za Kikoloni au Kanisa. Wasomi hawa wanapowaona Waislamu wanaotekeleza au kuieleza dini yao tofauti na wanavyoelewa huibua uadui na chuki. 

Kimsingi zipo hakika tano zinazohitajia mjadala baina ya Waislamu na Wakristo. Hakika hizi ndizo zitakazokuwa chemchem ya uchambuzi huu. Nazo ni maana ya neno Uislamu; maana ya Neno Allah; asili ya Mwanaadamu; uhusiano kati ya mja na Muumba; na nafasi ya Mwanaadamu hapa ulimwenguni. Baada ya kuzichambua hakika hizo yatafuatia maelezo machache yanayoangalia uwezekano wa kuwepo midahalo ya kidini katika mazingira ya leo. 

Itaendelea toleo lijalo. 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 

TAHARIRI 
Kuangukia makaa hakuna nafuu kwa aliye kikaangoni 

Wanawake Dodoma wataka mtoto aliyepigwa risasi akatibiwe nje 

Kesi za Mwembechai zaanza kusikilizwa 

Fitna ya Bakwata 

Dondoo za saikolojia: Tuonavyo mambo 

Waraka wa Baraza Kuu kuhusu Parole 

Inawezekana kufanyika mdahalo kati ya Waislamu na wasio Waislamu? 
Na Nandenga wa Mkomidachi 

Teknologia 
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (2) 
Na Hassan Omar 

Serikali ihamie Dodoma kwanza ! 
Na. Said Rajab 

Mahafali ya AMSIR Iringa 
Na Mwandishi Wetu 

Madrasatul Nnajjary Islamiya 

Ijue Madrasatul Riyaadh 

Bihawana Sekondari wafungua Ijumaa 

Vijana Shinyanga watakiwa kuwa mfano mwema 
Na Jihad R. Saballa, Shinyanga 

Vyeo visiwasahaulishe majukumu yenu- Sheikh Abri 
Na Mwandishi Wetu, Iringa 

Jiandaeni na kifo – Sheikh Abdallah 
Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

Semina zawazindua wanawake Bukoba 
Na Nadhiru Ishengoma 

Waislamu wanaomaliza Kidato cha Nne Tanga waaswa 
Na Ibn Mohamed 

Ndugu Kamuhabwa ndiye mwenye chuki na AN-NUUR 
Mwandishi: Maalim Bassalah 

'Ukombozi wa mwanamke si kugeuzwa biashara huria' 
Na Japhary Lemah, Arusha 

Polisi walinda amani katika muhadhara wa Wakristo 
Na Badru Kimwaga 

Mazengo wapewa uwanja wa kujenga Msikiti 
Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

'Ajiengua Chuoni Z'bar kwa kutoruhusiwa kuvaa hijab' 
Na Seif Hamad Suleiman, Zanzibar 

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Shairi 
Simlazimishe Yesu ukombozi wa ulimwengu (jibu)  

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita