AN-NUUR 
Na.172 Rajab 1419, Oktoba 23 - 29, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Ndugu Kamuhabwa ndiye mwenye chuki na AN-NUUR
Mwandishi: Maalim Bassalah

NDUGU Charles Kamuhabwa wa DSA, Mtwara katika makala yake yaliyotolewa katika gazeti hili, toleo Nam. 169, la Oktoba 2-8, 1998, amelishutumu gazeti hili, pamoja na Waislamu wanaochangia makala humu, kuwa ati wana chuki na Ukristo. Lakini kwa yule aliyeyasoma makala yake hayo hataacha kugundua, mara moja, kuwa mwandishi wa makala hayo ndiye aliye na chuki, tena siyo na gazeti la AN-NUUR tu, bali hata na Uislamu na Waislamu wenyewe. 

Kwanza, kama AN-NUUR lina chuki na Wakristo, kama alivyodai, mbona limempa nafasi ya kuchapisha makala yake hayo yaliyojaa shutuma na kejeli dhidi ya Uislamu na Waislamu? 

Ndugu Kamuhabwa anauchukia bure Uislamu na gazeti la AN-NUUR. Na hilo halitushangazi. Kuchukia au kupenda ni utashi wa moyo wa mtu. Waswahili hawa kukosea waliposema, "Apendaye chongo huita kengeza". Mtu huweza kukipapatikia kibaya akakiona kizuri machoni mwake, na akakichukia kizuri, akakiona kibaya. Basi kama ndugu Kamuhabwa ameamua kuichukia nuru kwa kuuita giza, asiwalazimishe wale wenye kulichukia giza walipende kwa kutaka waliite nuru. Uislamu ni nuru hakuna awezaye kuizima. 

Anastaajabu kwa nini Waislamu wanatumia nafasi kubwa ya gazeti la AN-NUUR kulalamika. Na kwa nini wasilalamike na haki wanaona wanapunjwa haki zao? Katika elimu wanafunzi wa Kiislamu wanaojiunga na shule za msingi, kila wanaoingia sekondari ni chini ya asilimia 30% na wanaopata nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu hawafikii asilimia 20%. Je! Tuseme wanafunzi wa Kiislamu ndio mbumbumbu au kuna mkono wa mtu unaowakandamiza ? Tokea tupate uhuru asilimia kubwa sana na vyeo vya madaraka serikalini vimekuwa vikichukuliwa na Wakristo. Je! Hilo nalo hutokea kwa sadfa tu. Au kuna mkakati maalumu ulioandaliwa ? Hayo ndiyo maswali yanayowasumbua Waislamu mpaka wakalalamika. Na wana kila haki ya kusikilizwa na siyo kupuuzwa. 

Siku zote mwenye kudhulumiwa ndiye anayelalamika; lakini dhalimu ana sababu gani ya kulalamika. Mwizi hufarahi kuwaibia wngine, halalamiki. Ukimwona mtu analalamika ujue amedhulumiwa. Siku madai ya Waislamu yatakaposikilizwa na kutekelezwa, Waislamu wataaacha kulalamika. 

Ama kudai kuwa ati Waislamu wanaukashifu Ukristo hilo halipo. Wanachokifanya Waislamu ni kutangaza imani yao na kuitetea pale wanapoona inapotoshwa. Kama kulikuwa na uhalali kwa Wakristo kudai kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, tena amesulubiwa na kuuawa, kisha akafufuka, mambo ambayo humkera sana Muislamu anapoyasikia, akavumilia; kwa nini basi Muislamu anaposema Yesu si mwana wa Mungu na hakuuawa wala kusulubiwa, aonekane kuwa anakashifu Ukristo ? Kama kusema hivyo kunawakera Wakristo kwa nini hawavumilii kama wanavyovumilia Waislamu ? Huo ndio uhuru wa kuabudu ! Kila mmoja anaruhusiwa kuitangaza na kuitetea imani yake. Madamu imani za dini hizo mbili zinapingana basi mafundisho ya upande mmoja hayawezi kupendezesha upande wa pili. Kilichobaki nikuvumiliana. 

Juu ya yule Muislamu aliyetaka serikali iwatoze kodi Wamisheni wanaoagiza dawa kwa ajili ya hospitali ya Ndanda na Nyangao, huenda shahaba yake ilikuwa ni kuona kuwa kuna uwiano katika kutoa misamaha ya kodi kwa mashirika ya kidini. Kama kuna sababu ya kutoa misamaha hiyo basi iwe kwa mashirika ya dini zote na isiwe kwa misheni tu. Au labda alikwishagundua udhaifu fulani katika kutoa misamaha hiyo. Labda mashirika hayo yanaitumia vibaya misamaha hiyo. 

Habari za kujenga hospitali, shule au barabara katika wilaya au mkoa ni jukumu la serikali. Mashirika ya kidini yanapofanya kazi hiyo huwa yanasaidia tu zile juhudi za serikali. 

Kuwalaumu Waislamu kwamba hawajajenga hospitali ni kuwabebesha lawama zisizo washusu. Wamisheni wanapojenga zahanati, hospitali au shule kweli huwasaidia watu, lakini pia huwa wanaitumia miradi hiyo kama chambo cha kuvulia watu wanaofaidika na huduma hizo wavutike na Ukristo ili waingie katika dini hiyo. Kwa nini shirika la Kikristo likajenge hospitali katika eneo ambalo asilimia themanini ya wakazi wake ni Waislamu? 

Aidha, ndugu Kamuhabwa anauliza Waarabu (Waislamu) ambao ndio wa mwanzo kufika huku Afrika Mashariki na kutawala miji yote ya mwambao waliwafanyia nini Waislamu wa sehemu hizi, katiak nyanja za elimu, uchumi na afya; mbali ya kuwapeleka mamilioni utumwani, na ambao hadi hii leo vizazi vyao havijulikani vimepotea wapi. 

Tatizo la Ndugu Kamuhabwa kutoelewa historia. Yeye anafuata maneno ya kusikia tu, na anafuata bila hata kuyapima au kuyafanyia utafiti. Anashindwa hata kufuata Biblia inavyosema: "Mjinga huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo". (Mithali 14:15). 

Angalisoma historia angaliona Waarabu (Waislamu) walifanya nini katika kanda ya Pwani ya Afrika Mashariki. Wasafiri wa mwanzo kufika sehemu hizi kama kina Yakut, Al-Masudi na Ibn Batuta wameandika katika vitabu vyao kuwa walipotembelea sehemu hizi walikuta ustaarabu mkubwa. Waliwakuta wenyeji wakitumia nguo za pamba na hariri. Wanawake wakijipamba kwa dhahabu kutoka sofala. Kulikuwa na biashara kubwa baina ya wafanyabiashara kutoka mashariki ya kati na nchi zinazotumia Bahari ya Hindi. Wenyeji walikuwa wanatumia sarafu walizozitengeneza wao wenyewe. Kwa mfano, pesa zilizogunduliwa huko Mtambwe Mkuu, kisiwani Pemba, na kuchunguzwa na Bibi Helen Brown wa makumbusho ya Ashmolean, Chuo Kikuu cha Oxford, nchini Uingereza amehakikisha kuwa fedha hizo ni za karne ya kumi na moja kutokana na umbo lake dogo zinaonekana zimetengenezwa kienyeji. Miji mingi ilichipuka na kustawi vizuri. Hata hili jiji la Dar es Salaam limepata jina lake kutokana na watawala hao. Jina hilo limetokana na neno la Kiarabu Dari Salaam, maana yake nyumba (bandari) ya amani. Huo ulikuwa ni wakati wa usitawi. 

Wenyeji walikuwa wakijua kusoma na kuandika kiswahili kwa kutumia herufi za kiarabu. Na wakatunga vitabu vingi vya elimu mbalimbali kwa kutumia herufi hizo. 

Kuhusu afya walikuwa mabingwa wa kutumia dawa za kienyeji zilizotajwa katika vitabu vya dawa vya Kiarabu. Huko Zanzibar mpaka hivi leo kuna maduka yanayouza madawa hayo ya Kiarabu kama kwa Saleh Madawa na Angalimarango. Ni wakoloni ndio waliowafanya wenyeji wadharau matibabu yao ya kiasili na kuwahimiza wafuate matibabu yao. Na ndiyo kasumba hiyo hiyo inayotufanya sisi leo tuwadharu waganga wetu wa kienyeji wanaodai kuwa wana dawa ya kutibu ukimwi. Hatutaki kuzifanyia utafiti dawa hizo; tunazidharau. Tunangojea mpaka Wazungu wavumbue ndio tukubali. 

Anataka kujua vizazi vya mamilioni ya Waafrika waliopelekwa utumwani viko wapi. Mwenye macho haambiwi tazama? Je! Wale Wamarekani weusi kule Marekani ni kizazi cha nani? Na wametokea wapi wale. Kizazi hicho mpaka hivi leo kinabaguliwa na kudharauliwa kwa kuitwa Manigro. Na kwa vile weupe hawakutaka kuoana nao, walibki kuoana wenyewe kwa wenyewe, weusi kwa weusi, ndiyo wakazaliana na kubaki hivyo hivyo kama walivyo. Lakini kwa vile wale waliowapeleka huko utumwani walikuwa ni Wakristo wenziwe, ndugu Kamuhabwa hayaoni hayo. 

Asili ya wale waliopelekwa utumwani Arabuni hawaonekani ni kwa sababu walioana na wenyeji wao na kuzaa. Wakachanganya damu. Ndiyo maana utaona kuna Waarabu wa rangi mbalimbali, kuna weupe, wekundu na hata weusi tititi; lakini wote hao ni Waarabu. Na hayo wameyaweza kuyafanya kutokana na Uislamu wao. Uislamu hauna ubaguzi. 

Kuulaumu Uislamu kuwa ndiyo ulioleta utumwa huku Afrika Mashariki si sahihi. Biashara ya utumwa imekuwako kwa muda mrefu katika historia ya mwanaadamu na takriban mataifa yote yalijiingiza katika biashara hiyo. Hata Waafrika kwa Waafrika nao walizana, wenyewe kwa wenyewe. Uislamu ulipokuja na kuukuta utumwa uliandaa taratibu za kuukomesha. Kwanza Mtume Muhammad (s.a.w) aliona ipo haja ya kupunguza idadi ya watumwa. Akakataza mtu asimtie utumwani mtu aliye huru. Pili, baadhi ya makosa adhabu yake ikafanywa ni kuacha huru mtumwa. Na mwisho Mtume (saw) akawaambia masahaba wake kuwa kila kiungo cha mwili cha mtumwa watakayemwacha huru, Mwenyezi Mungu (s.w.) ataviepusha viungo vyao wao na moto wa jahanamu. Waislamu wengi wakamwitikia Mtume (s.a.w) na wakawapa uhuru watumwa waliokuwa wakiwamiliki. Lakini Ukristo hatuuoni kuukemea mfumo wa utumwa, bali unawahimiza watumwa wawe watii kwa Mabwana zao. Paulo anasema "Watumwa na wawatii bwana zao, wakiwapendeza katika mambo yote, wasiwe wenye kujibu". (Tito 2:9). 

Na Wazungu hawakuwapa watumwa uhuru mpaka yalipotokea huko Ulaya mapinduzi ya viwanda (industrial revolution). Walipovumbua viwanda na mashine za aina mbalimbali zinazozalisha mali kwa wingi na kwa muda mchache wakaona kuweka watumwa itakuwa ni gharama kubwa. Ndiyo wakawapa uhuru. Na ahwakutaka wabaki Ulaya wakapeleka kuishi katika nchi ya Liberia. Asili ya Liberia ni taifa la Watumwa! 

Inaonekana ndugu Kamuhabwa hatofautishi baina ya Waarabu Waislamu, Waarabu ni kabila, lakini Uislamu ni dini. Si kila aliye Mwarabu ni Muislamu, wengine ni Wakristo, nao pia walishiriki katika biashara hiyo ya utumwa. 

Kusema kwamba misaada inayotoka Arabuni lazima ilengwe kwa Waislamu, hilo si kweli. Mara ngapi mataifa ya Kiarabu yaliisaidia matufa nchi yetu ? Je, mafuta hayo yalikuwa yakitumiwa na Waislamu tu ? Hivi sasa Kuwait na Saudi Arabia zinasaidia kujenga daraja la kisasa katika mto Rufiji. Je! Daraja hilo likimalizika litatumiwa na Waislamu peke yao? 

Dai lake kuwa Qur’an nayo imepunguzwa kama ilivyopunguzwa Biblia, nalo si la kweli. Qur’an tuliyo nayo sasa ndiyo ile ile iliyokuwapozama za Mtume (saw). Haikuongezwa wala kupunguzwa. Kuhusu maelezo yanayosemekana kuwa ya Seyyidna Umar bin Khatab (ra) kuhusu "aya" ya Rajm. Hiyo ni taaluma pana nachelea kuiminya katika nafasi hii finyu. 

Kuhusu Waislamu kufanya mambo yasiyokuwapo zama za Mtume (saw), katika Uislamu kuna utaratibu maalum wa kuruhusu kufanya hivyo. Hutazamwa lile jambo lenyewe kama halipingani na Qur’an tukufu au Sunnah ya Mtume (saw) basi linaruhusiwa. Kwa mfano kuadhini katika spika ilikuwa hakuna zama za Mtume (saw). Lakini ilivyokuwa lengo la kuadhini ni sauti ifike mbali basi wakaruhusu kutumia vipaza sauti katika Uislamu. Pia upigaji cha Qur’an ulikuwa haupo wakati wa Mtume (saw) lakini kwa vile jambo hilo halivunji maadili ya Kiislamu linakubalika. 

Mwisho, ndugu Kamuhabwa anashangaaa kuona Waislamu wanasema kuwa dini yao ndiyo iliyo bora, na kitabu chao hakibadilishwa, na Mtume wao ndiye aliye mkuu kuliko manabii wote halafu Waislamu hao hao baada tu ya kufariki Mtume wao wakaanza kuuana wenyewe kwa wenyewe. Walimwua mzee kikongwe, Seyyidna Uthamn bin Affan (r.a). Sijui ndugu Kamuhabwa anatumia kipimo gani kupimia ubora na usahihi wa dini ? Kama kuuawa Seyydina Uthman na Waislamu ndiyo kipimo alichokitimia basi inaonyesha Ukristo si dini bora wala siyo sahihi kwani waliomwua Seyyidna Uthman ni kipote kidogo cha waasi na wala hawakuwa katika wale wanafunzi kumi wa Mtume (saw) aliowabashiri pepo. Lakini Yesu aliuawa kwa usaliti wa Yuda Eskarioti, mmojawapo wa wale wale wanafunzi wake kumi na mbili! Tena Seyyidna Uthman hakuwa Mtume, alikuwa ni mfuasi wa Mtume (saw) lakini Yesu alikuwa ni mwana wa Mungu au ni Mungu hasa kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa. Basi Yuda akamsaliti Mungu wake kwa tamaa ya vipande vichache vya fedha! 

Ndugu Kamuhabwa anaupinga ubora wa Qur’an kwa kusema eti kuna Waislamu wanaofuata mambo ya ushirikina. Je! Tuseme na Bibilia nayo si bora na Ukristo si din sahihi kwa vile katika Ukristo kuna mashoga wa kiume wanaooana wenyewe kwa wenyewe tena Kanisani? Na ndoa hizo zikaongozwa na Mapadri ? 

Namshauri Ndugu Kamuhabwa afikiri kabla ya kukamata kalamu. Asisahau maandiko yanayosema, "Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa; bali kinywa cha mpumbavu hula upumbavu" (Mithali 15:14). 


Wanawake Arusha waambiwa:
‘Ukombozi wa mwanamke si kugeuzwa biashara huria’
Na Japhary Lemah, Arusha

WANAWAKE mjini Arusha wametahadharishwa waepukane na fikra potofu pamoja na mitazamo lemavu iliyobebwa na dhana ya ukombozi wa mwanamke. 

Akizungumza katika darsa zake kwa nyakati tofauti katika Msikiti wa Bondeni mjini hapa, Sheikh Shaaban Juma amesema kwamba kumekuwa na dhana potofu ya kuhusisha ukombozi wa mwanamke na kumuasi Mwenyezi Mungu kwamba kujisitiri vyema kwa mujibu wa sheria za Allah ni kuwa gizani na kukosa maendeleo na ukombozi wenyewe ni kutembea uchi na kushiriki mashindano kama yale ya Miss Aspen, Miss Tanzania n.k. 

Sheikh Shaaban Juma amesisitiza kwamba programu zote hizi na kelele zote hizi za ukombozi wa mwanamke athari yake ya jumla itakayopatikana ni kumvua mwanamke stara yake na kumtia katika ujahili wa kumuasi Mola wake. 

Katika kusisitiza kwamba Uislamu hauhitaji kampeni hizi, Sheikh Shaaban amesema kwamba Uislamu unajitosheleza katika masuala mazima yanayohusu hadhi na nafasi ya mwanamke katika Uislamu na jamii kwa ujumla. 

Ili kuonyesha jinsi Uislamu unavyothamini na kuchunga heshima ya mwanamke, Sheikh Shaaban amesema kwamba adhabu kali hutolewa kwa wanaowazulia uongo wanawake. 

Amesema adhabu hiyo imetajwa katika sura ya 24 aya ya 4. 


Polisi walinda amani katika muhadhara wa Wakristo
Na Badru Kimwaga

POLISI wamekuwa wakilinda amani na utulivu katika mihadhara ya dini ya Kikristo inayoendelea Jijini Dar es Salaam. 

Ukweli huu umebainika wiki hii wakati askari polisi walionekana katika mkutano wa kidini wa Kikristo unaendelea maeneo ya viwanja vya Drive Inn, Msasani ambapo askari hao wakiwa na sare na wengine wakiwa na nguo za kiraia, wamekuwa wakiwahoji watu wapitao katika mkutano huo wanaowahisi sio Wakristo waliokuja kusikiliza mahubiri. 

Mwandishi wa habari hizi aliweza kuwaona askari wapatao wawili waliovaa sare na wanne wenye nguo za kiraia kana kwamba ni wahudumu wakiwahoji watu huku wakiwataka kutokomea ikiwa sio waliofuata mahubiri hayo. 

Mkutano huo ulianza Jumamosi ya Oktoba 10, mwaka huu unaotegemewa kumalizika Oktoba 31, 1998 unaendeshwa na Mchungaji Meshack Nyagori Olouch ambapo viwanja hivyo vinavyotumika kama vya michezo ya wazi vimejengwa mahema na wasikilizaji wake wametengewa mabenchi, ili waweze kuwang’amua kwa urahisi watu wasiohusika. 

Hali hii ya kuwekewa walinzi katika mahubiri yao sio mageni kwani hata mikutano ya Jangwani huwa hivyo, hali ambayo ni tofauti na Waislamu ambao mahubiri na mihadhara yao huendeshwa Misikitini lakini bado askari wamekuwa wakiwasumbua na kuwakamata kwa madai wanatoa kashfa kwa wasio Waislamu, ingawa kinachoongelewa katika mihadhara ya Kiislamu huwa hakina kashfa. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 

 
TAHARIRI 
Kuangukia makaa hakuna nafuu kwa aliye kikaangoni 

Wanawake Dodoma wataka mtoto aliyepigwa risasi akatibiwe nje 

Kesi za Mwembechai zaanza kusikilizwa 

Fitna ya Bakwata 

Dondoo za saikolojia: Tuonavyo mambo 

Waraka wa Baraza Kuu kuhusu Parole 

Inawezekana kufanyika mdahalo kati ya Waislamu na wasio Waislamu? 
Na Nandenga wa Mkomidachi 

Teknologia 
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (2) 
Na Hassan Omar 

Serikali ihamie Dodoma kwanza ! 
Na. Said Rajab 

Mahafali ya AMSIR Iringa 
Na Mwandishi Wetu 

Madrasatul Nnajjary Islamiya 

Ijue Madrasatul Riyaadh 

Bihawana Sekondari wafungua Ijumaa 

Vijana Shinyanga watakiwa kuwa mfano mwema 
Na Jihad R. Saballa, Shinyanga 

Vyeo visiwasahaulishe majukumu yenu- Sheikh Abri 
Na Mwandishi Wetu, Iringa 

Jiandaeni na kifo – Sheikh Abdallah 
Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

Semina zawazindua wanawake Bukoba 
Na Nadhiru Ishengoma 

Waislamu wanaomaliza Kidato cha Nne Tanga waaswa 
Na Ibn Mohamed 

Ndugu Kamuhabwa ndiye mwenye chuki na AN-NUUR 
Mwandishi: Maalim Bassalah 

'Ukombozi wa mwanamke si kugeuzwa biashara huria' 
Na Japhary Lemah, Arusha 

Polisi walinda amani katika muhadhara wa Wakristo 
Na Badru Kimwaga 

Mazengo wapewa uwanja wa kujenga Msikiti 
Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

'Ajiengua Chuoni Z'bar kwa kutoruhusiwa kuvaa hijab' 
Na Seif Hamad Suleiman, Zanzibar 

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Shairi 
Simlazimishe Yesu ukombozi wa ulimwengu (jibu) 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita