|
|
| BARUA
Wadhamini wa Misikiti Ndugu Mhariri MATATIZO makubwa yanayowakabili Waislamu hivi sasa ni kutoitumia Misikiti kama taasisi muhimu kwa maendeleo yao. Tumechukua ibada moja tu ya sala na baada ya hapo watu wanatawanyika au kuanza kupiga soga nje ya Msikiti, ndiyo maana "mpendwa" wangu mmoja aliwahi kusema kuwa baada ya sala fungeni Misikiti mtawanyike maana Qur'an inasema: Sala ikiisha tawanyikeni. Hii ni kutokana na kutokuwa na ujuzi juu ya tafsiri ya Qur'an, lakini kwa mazoea ya Watanzania ni kuwa kilichosemwa na kiongozi ni sahihi hata akiponda vipi maana mazoea yetu ni hata DC au RC au Waziri mwenyewe kasema, hili limeturudisha nyuma siyo tu Waislamu bali Watanzania wote kwani tumekuwa wavivu kufikiria. Kuna watu wanaojiita "wadhamini" wa Misikiti, lakini sidhani kuwa wanafahamu majukumu yao na mipaka yao, pia sisi waumini hatufahamu mamlaka tuliyonayo, na serikali yetu kwa kutumia chombo kisicho kuwa chetu "BAKWATA" imekuwa inalazimisha mamlaka ya hawa mabwana bila kujali sheria kwani serikali inafahamu wazi kazi za wadhamini. Ningeomba jambo hili ndugu Waislamu tulianzishie mjadala wa kujua madaraka ya hao wadhamini na jinsi wanavyopatikana kisheria (za nchi). Wadhamini huandikishwa chini ya sheria ya Muungano wa wadhamini (Cap. 375). Baraza hili la wadhamini huchagua Mwenyekiti wake miongoni mwa wajumbe wake. Kazi au majukumu yake nikuwa na uwezo wa kuuza, ,kununua, kuhamisha, kupokea, kuweka rehani au kufanya namna yoyote ya chombo wanachokidhamini kwa kushirikiana na uongozi, na kwa Waislamu haya yote yawe kwa mujibu wa Qur'an na Sunna. Wajumbe hao huchaguliwa aidha na kamati au mkutano mkuu wa chombo husika. Huu ndiyo uchache wa vile mimi ninavyofahamu, ndiyo maana naomba mijadala. Hawa si watendaji nao si wakuu wa waumini, katika hali yoyote ile waumini au wanachama wanakauli ya mwisho. Kinyume cha mambo ni kuona kuwa wadhamini hawa Msikitini ati nao ndiyo wenye kauli ya mwisho, wao ndiyo wenye kumweka Imam na kumuondoa, bila kufuata mafundisho ya Mtume (saw) jinsi ya kumpata Imam, bahati mbaya waumini wanaridhika kuwa hivi ndivyo ilivyo, hayo ni makosa ambayo lazima tuyarekebishe, watu hawa hawahusiki na utendaji wa kila siku wala hawataulizwa Msikitini wamesema nini. Bali Imam na Kamati yake ndiyo wataulizwa, wao wataulizwa madeni na wadai. Vyama vya siasa vinawadhamini, vikiwemo vile vikubwa viwili CCM na CUF, hivi inawezekana siku moja wakaamua kumfukuza Mwenyekiti wa chama wa Kitaifa kwa kuwa wao ni wadhamini? Kwanini serikali haiwaambii wana NCCR kuwa matatizo yenu yatamalizwa na wadhamini? Hapa tunaona kuwa ufahamu wetu mdogo kuhusu watu hawa ndiyo umesababisha wao kujiona ni viongozi wenye mamlaka juu ya kila kitu. Hapa panazuka jambo jingine ambalo watu wamelikosea pia nalo linasaidia kuwapa nguvu wasiyokuwa nayo. Haya yametokea kwenye mpira kupatikana watu wanaoitwa wafadhili, sasa sisi pia tumeiga kila anayetoa kingi anaitwa mfadhili na anayetoa kidogo, katoa sadaka. Hapa pamezuka utata la watu kufikia kusema huu Msikiti wangu kwa kuwa katoa kingi, yeye pamoja na sisi tupo tayari kumpinga Allah anayesema Misikiti yote ni mali yake. Mfadhili ni mtu anayemsaidia mtu mwingine kutatua matatizo yake, sasa hata hao walioanzisha jambo hili, ni vipi "Dewji" aseme yeye Simba damu halafu awe mfadhili wa Simba? Hii ni timu yake, sasa anamfadhili nani? Yeye mwenyewe? Vivyo hivyo kwa Gulamali, yeye Yanga sasa anamfadhili nani? Yeye Mwenyewe? Kuchangia maendeleo ya klabu zao, ila mmoja wa hawa akitoa kwa upande mwingine hapo atakuwa mfadhili. Sasa katika Uislamu mtu anakuwa mfadhili kwa kujenga Msikiti au Madrasa au kuchimba kisima badala ya kuwa ametoa sadakat jaria itakayomfaa hapo baadaye, sisi tunasema mfadhili wetu, na kwa hiyo akija tutasimama na kumbusu mikono. Ndugu Waislamu kila mmoja anajipendekeza kwa Mola wake kwa kadri yeye alivyojaaliwa. Lazima tuambiane anayetaka kujenga nyumba na aimiliki yeye atakavyo basi na akajenge Hotel au nyumba ya kulala wageni huko Mnazi Mmoja au Ilala badala ya kutaka mamlaka katika Misikiti ambayo haingii ia kuna kiongozi amekuja au mwezi wa Ramadhani, sala ya Magharibi tena hukaa kibarazani. Allah (sw) anasema: "Ole wao wenye kusali ambao hufanya hivyo ili kuwaonyesha watu". Ni matumaini yangu kuwa wataalam miongoni mwetu watalichambua kwa ufasaha zaidi ili tupate kusonga mbele katika harakati za kuujua na kuutetea Uislamu. Wabilah Taufiq, M.A. Kazukamwe, S.L.P. 2928, DAR ES SALAAM
. Tanga tumechoka kutukanwa na viongozi Ndugu Mhariri VIONGOZI wa Serikali kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiwakejeli wananchi wa Tanga kuwa ati ni wavivu ndiyo maana wako nyuma kimaendeleo. Kwa kweli kauli hiyo si mpya kwa Watanzania, na sisi watu wa Tanga tumeizoea. Kauli hiyo hiyo iliwahi kumkosanisha Mkuu fulani wa Mkoa na wazee wa Tanga miaka ya nyuma. Cha kujiuliza, ni je, shutuma hizi ni kweli, na je viongozi wa serikali hupewa semina ya kuwajulisha juu ya uvivu wa Tanga? Kwa sababu inashangaza kila mmoja kati yao huja na hoja hiyo hiyo hata pale sababu isipoonekana. Ili ieleweke iwapo kweli Tanga tuwavivu, ni muhimu kwanza ijulikane shughuli gani huitwa kazi za maendeleo na vitu gani ni dalili ya uvivu. Maeneo yaliyotajwa hasa kujaa wavivu, wilaya ya Pangani na Tanga Mjini, shughuli zetu ni za uvuvi na kilimo cha minazi pamoja na mazao ya chakula. Tangu barabara yetu ilipojengwa awamu ya pili, je nazi hazifiki Arusha na Mwanza? Hivi sasa majeruhi wa vipigo vya wanajeshi miongoni mwa wavuvi wanaongezeka, kwa visingizio vya leseni na uharibifu wa mazingira, lakini bado hatuli mihogo mitupu, lazima kitoweo cha samaki kitakuwepo. Uko wapi uvivu hapa? Ama iwapo kazi ni kulima kahawa na maharage, basi kwetu hayaoti. Ikiwa suala ni kukaa mabarazani na kunywa kahawa, basi hili halifanyiki wakati wote na si kwa kiwango cha kuitwa wavivu. Vipi wenye kushinda vilabuni, groceries na mabaa na kugombana, mbona hatujasikia katika ziara zenu mukiwashutumu kwa ulevi? Kuna mikoa ina wazinifu wengi, mpaka sasa idadi ya watu inapungua kwa kasi, kwanini hawashutumiwi kwa uzinifu wao. Je, ni sawa kuitaja mikoa hiyo kama mikoa ya makosa hayo? Uvivu, ulevi, uzinifu ni sifa mbaya ambazo kila pahala zipo. Pale zilipo ni kuweka mazingira ya kuziondoa, na kutokufanya upendeleo katika kuzikemea. Vinginevyo tutahisi kuna ajenda ya siri. Kazi kwa wengine maana yake ni kila mtu kuonekana akivuja jasho na jembo mkononi. Iwapo hili halionekani Mjini Tanga na Pangani, kwa kila mtu, basi hata hao wanaotusema hawanalo. Kutokuwa na majumba ya ghorofa haina maana kuwa hatufanyi kazi, pengine ni kwa sababu ya kudhulumiwa sana na hao wajengaji mukija Tanga muje na majibu, hatutaki lawama. Mwananchi Mkereketwa, Tanga.
Wanamuziki hawa walaaniwe Ndugu Mhariri NAOMBA nitoe pole kwa nchi za Kenya na Tanzania kwa msiba uliotupata kwa milipuko ya mabomu kwenye Ubalozi wa Marekani Kenya na Tanzania. Lakini masikitiko yangu ni jinsi nchi nyingi duniani, vyombo vya habari, watu binafsi na sasa wanamuziki wanavyojaribu kulihusisha jambo hili na Waislamu. Jambo la kusikitisha ni hivi karibuni bendi maarufu nchini Kenya imetunga wimbo ambao kabla ya kuanza wanamuziki hao wa Mashroom (Wazee wa kazi) wanamtaja Mungu kwa kusema Takbir Alahuakbar mara mbili halafu madhalimu hao wanaendelea kuimba jinsi hali ilivyotokea Kenya na Tanzania na kuonyesha jinsi walivyo na masikitiko na kuzipa pole nchi za Kenya na Tanzania kwa msiba uliowapata. Na mwisho wanarudia, Takbir Alahuakbar mara mbili. Mashrooms wawaombe radhi Waislamu na huo wimbo upigwe marufuku kwa kuidhalilisha dini ya Mwenyezi Mungu na wachukuliwe hatua kali za kisheria, na wote wenye tabia kama hizo waache kwani mambo kama hayo yanahatarisha amani ya nchi na dunia kwa ujumla. Suleyman H. Suleyman, S.L.P. 363, SAME.
Uadilifu baina ya mke na mume wanapokhitalifiana Ndugu Mhariri KWA wingi wa heshima na utii, naleta barua yangu hii kwako katika gazeti hili tukufu kama lilivyo jina lake (AN-NUUR). Kwa maslahi ya wasomaji wote, nakuomba barua yangu hii uipe uzito ili tunufaike sote ambao tumeshaingia katika maisha ya ndoa. Kama tunavyofahamu kuwa Uislamu ni dini ya uadilifu na hatuwezi kuuona uadilifu wake bila ya kukifuata kitabu cha Allah (sw) na katika Hadithi za Mtume wetu Muhammad (saw). Na kila anayetaka manufaa ya dunia na akhera lazima afuate Qur'an na Sunnah. Uislamu haumkandamizi mwanamke wala mwanamme, ila sisi binadamu tunajitafutia matatizo wenyewe. Aya nyingi zinahimiza uadilifu, si kwenye ndoa tu ila katika kila jambo likiwa la kidini au la kidunia. Matatizo mengi katika jamii mbalimbali hutokezea katika ndoa unapokosekana uadlifu. Talaka ni halali aliyoichukia Mwenyezi Mungu. Mtu huoa kwa ajili ya kupata manufaa mbalimbali kama ilivyo katika aya ya 21 ya Suurat - Rum. Siamini kuwa mtu huoa kwa ajili ya kuacha, lakin ikiwa hapana budi ndio hufikia hatua hiyo. Sisi wanaume tuna matatizo yetu na wanawake wana matatizo yao, lakini wanawake nao wana historia tangu enzi za Mitume. Na kama si ingelikuwa sharia watu wengi wasingelioa, kweli kuna faida kubwa lakini nitaeleza matatizo yaliyopo na binadamu akikumbana nayo huweza hata kukufuru (inshaallah Mwenyezi Mungu atuepushe nayo). MATATIZO: Kama mwanamke hamtaki au watakhitilafiana mume basi kila visa humfanyia ili bilisi aje karibu, hujaribu kupeleka mashitaka ya kweli yaliyochanganywa na uongo, hapo tena kwa ulimwengu wa kileo asilimia kubwa ya wazee si watu wenye busara, hekima, uadilifu na wakiwa ni wazee walioruzukiwa wingi wa mali, hutumia kibri, kejeli, dharau, hasira hujifanya wao ndio wamefika, ujinga umewazidi, pesa wameziweka mbele zaidi. Hebu tuiangalie Qur'an aya ya 35 ya Suurat Nisa-I, kwa vile "damu ni nzito kuliko maji" wao huamini moja kwa moja maelezo ya mtoto wao. Aidha, turejee katika aya ya 6 ya Suurat Hujraat. Hapo kama mwanaume atatumia hatua ya kutoa uamuzi wa talaka ndio wanaanza kuujua ulimwengu. Matukio mengi kama haya tayari yameshatokea, masikini serikali yetu haihukumu kisheria ya Kiislamu, Masheikh wetu wengi wakishapewa pesa nao huangalia kesi upande mmoja tu. Ndoa nyingi huvunjika kwa malezi mabaya ya mtoto mwanamke au mawalii wa mtoto kuwa sio waadilifu inapotokezea khitilafu. PENDEKEZO: Mimi napendekeza kiundwe chama chenye kusajiliwa kinachojihusisha na matatizo ya ndoa katika jamii. Kiwe chama cha uadilifu kweli. Sio chama cha kutafutia pesa ya kula. Naona tutafaidika mno kama kesi kama hizi zitaundiwa chama chake na itakuwa bora kabisa zichapishwe kesi mbalimbali katika AN-NUUR ili tuwe kwenye `nuru' mbele ya hesabu (maisha baada ya kufa). Abdallah A. Abdallah P.O. Box 7325/5252, DSM |
YALIYOMO
TAHARIRI Hakuna Muislamu aliyekufa kutokana na vurugu Mgogoro wa kiwanja Duma: Wakatoliki wasema kuna njama za Waarabu Same Na Mwandishi Wetu Wanawake wakutana Mwanza na kusema: Kunyanyaswa sasa basi Na Mwandishi Wetu, Mwanza Sheikh Omar Bashir ataka Waislamu waimarishe mshikamano Na Said Sharif Ustaadhi Abdallah Mfoyi afariki Na Muhibu Saidi Baraza Kuu halina Katibu Nguruka - Sheikh Kilima Na Abu Adli Viongozi Msikiti wa Ubungo Darajani waitwa polisi Na Kassim Juma Marekani `ilivyosaidia' Mujahidiin Barua ya mtoto wa miaka minne toka Lebanon kwa Bibi Hillary Clinton Ujumbe wa waandishi kwa Bw. Batendi, Wakristo Na Muhibu Saidi Waislamu wanadhalilishwa au wanajidhalilisha Tusiwe Jogoo wa Esopo na Almasi Na MAALIM ALI BASSALEH Sherehe za wiki ya usalama barabarani: Kauli nzito za waheshimiwa zimekalia kuti kavu Na Said Omar Mwanasayansi Avicenna: Tabibu bingwa. Na Dk. A. A. Amur Ujenzi wa Msikiti wa Ijumaa Mriti waanza Na Nasib A. Mziray Kutoweka kwa hazina adimu za kimazingira Na Yassir Salim Mfalme Najashi ni mfano bora wa kuigwa kwa watawala Na Idi Kikong'ona Waislamu Moro wasaidia wagonjwa Na Mwandishi Wetu, Morogoro KUFUATIA KUTISHIA MAGAZETI: Sheikh Ayoub amjibu Askofu Rajab Rajab Na Mussa Ally TAMSA Tanga waahidi kuendeleza mema Na Ibn Mohammed, Tanga Ufugaji, uuzaji nguruwe wakera wananchi Dar Na Mwandishi Wetu Mafundisho ya Quran Kuwepo kwa ufufuo Barua za wasomaji
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org