|
|
| Tusiwe Jogoo
wa Esopo na Almasi
MAREKANI pamoja na nchi za Magharibi zimekuwa mstari wa mbele kuzipiga vita zile nchi zinazoanzisha utawala wa kufuata sharia ya Kiislamu. Wanadai kuwa sharia hizo ni za kikatili na zinakwenda kinyume na haki za binadamu. Hazifai katika huu ulimwengu wa maendeleo. Mara kwa mara Marekani imekuwa ikikwaruzana na nchi hizo za Kiislamu kwa kisingizio hiki au kile. Ndiyo maana tukaona Marekani haielewani na Iran, Afghanistan na Sudan. Mwandishi MAALIM ALI BASSALEH anaelezea zaidi. LAKINI mtu anapokichukia kitu, haina maana kuwa lazima kitu hicho kiwe kibaya au hakifai. Huenda ikawa kasoro ni ya yule anayekichukia na siyo kile kinachochukiwa. Mwenye homa huweza akayachukia maji ya kunywa, yaliyo matamu na baridi, siyo kwa sababu maji hayo ni mabaya; bali ni kwa kuwa kinywa cha mgonjwa huwa ni chapwa, hakihisi ladha ya chakula! Aidha, kwa kutoelewa, mtu haweza akakipapatikia kile chenye madhara na yeye na kukipuuza kile kilicho na manufaa naye. Hapa nakumbuka kisa cha jogoo na almasi katika kitabu cha Hadithi za Esopo. Safari moja jogoo alitoka alfajiri kwenda kutafuta chakula. Kwa mbali akaona kitu kinang'ara sana. Akakiendea ili akijue kilikuwa ni kitu gani. Kumbe kilikuwa ni kipande cha almasi. Kuona hivyo jogoo akailaani bahati yake. Akatamani bora ile almasi ingalikuwa punje ya mahindi au mtama, angalipata kitu cha kufungulia kinywa. Ingawa kisa hiki ni cha kubuni; lakini kina mazingatio ndani yake. Almasi ni johari yenye thamani kubwa sana. Ingalitosha kumtajirisha jogoo pamoja na wote wanaomtegemea. Angalijua matumizi yake ingalimletea magunia elfu nyingi yenye punje lukuki za mtama, akala yeye, wanawe na wajukuu zake, umri wao wote. Lakini kwa vile jogoo hakuijua thamani ya kile kipande cha almasi, basi hakuielewa faida yake pia. Swali la kujiuliza jee, ile almasi ilikosa thamani kwa kuwa jogoo alikuwa haijui thamani yake? Bila shaka thamani ya almasi ilibaki pale pale; na jogoo ndiye aliyekula hasara kwa ule ujinga wake. Aliichukia almasi na kumbe ilikuwa ina maslahi naye. Mwenyezi Mungu (sw) anasema ndani ya Qur'an Tukufu: "Na huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkakipenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua na ninyi hamjui". (Al-Baqarah 2:266). Basi huenda hao wanaoichukia na kuipinga sharia ya Kiislamu wakafanana na jogoo wa Esopo. Wanaipinga kwa kuwa hawaielewi, na siyo kwa sababu haifai. Katika hii kashfa ya ufuska iliyomkumba Rais Bill Clinton, laiti angaliielewa sharia ya Kiislamu inasema nini, angaliikumbatia badala ya kuipinga. Angalitamani Marekani ingelikuwa inaongozwa na sharia ya Kiislamu. Mwenyezi Mungu (sw) anasema katika kitabu chake kitukufu; "Na wanaowasingizia wanawake wema, kisha wasilete mashahidi wanne, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio wapotovu". (An Nur 24:4). Na hukumu hii siyo kwa mwanaume tu kumsingizia mwanamke; bali pia kwa mwanamke anayemsingizia mwanaume. Kwa maana hiyo, laiti ingalikuwa Marekani inatawaliwa na sharia ya Kiislamu basi Monica Lewinsky asingalithubutu kabisa kutoka hadharani na kudai kuwa alikuwa ana uhusiano wa kimapenzi na Rais Bill Clinton. Mahakama ya Kiislamu ingalimtaka Monica alete masahidi wanne walioona kwa macho yao kitendo hicho cha ngono kikitendeka. Kama hataweza kuwaleta hao mashahidi wanne basi mahakama itaamuru apigwe mijeledi thamanini kwa kumsingizia mwenzie uongo. Adhabu hii inaitwa Hadil-Qadhaf. Hukumu hii imekusudiwa kulinda heshima ya mwanamke na mwanaume na ile tabia mbaya ya usingiziaji iliyoota mizizi katika jamii. Sharia inatoa adhabu kali ili kuikomesha tabia hiyo. Utaona kuwa sharia haitaji kama masingizio hayo ni ya kweli au ya uongo. Mradi hata ikiwa ni kweli kuwa huyo aliyesingiziwa kafanya tendo hilo lakini yule akashindwa kuleta mashahidi wanne basi atahesabiwa yeye ndiye mwongo na atapewa ile adhabu. Kwa vyovyote vile kama yule msingiziaji atashindwa kuwapata mashahidi wanne basi yule aliyesingiziwa atahesabiwa kuwa hana hatia yoyote. Sharia ya Kiislamu hairushu kabisa mtu kuvunja heshima ya mtu mwingine kwa njia yoyote ile. Huoni basi kuwa sharia inazilinda haki za binadamu na sivyo kama wanavyodai wapinzani kuwa ati inavunja haki hizo? Pili, sharia ya Kiislamu inalenga katika kuondoa kiini cha uovu na siyo kufyekeza juu juu tu na kuacha mizizi ya uovu utambae. Wakati vitabu vya dini nyingine vinasema "usizini", Qur'an tukufu inasema "Wala msikaribie uzinzi". (Bani Israil 17:32). Utaona Uislamu unatutaka tujiepushe siyo na uzinzi tu, bali nakila sababu zinazopelekea katika hilo tendo la uzinzi. Ndiyo maana mafunzo ya Kiislamu yakakataza wanawake wasichanganyike na wanaume. Wanawake wakatakiwa wavae nguo za stara, wala wasionyeshe mapambo yao kwa wanaume wa nje. Lau kwamba Marekani ingalikuwa inafuata mfumo wa serikali ya Kiislamu Clinton angaliwezaje kukutana na Monica wakafanya ufuska huo? Wapinzani wanasema sharia ya kumtenganisha mwanamke asichanganyike na wanaume inambagua mwanamke na kumkandamiza; lakini wanasahau kuwa kwa maumbile mwamke ni kivutio cha mwanaume. Kama ilivyo ni hatari kuweka petroli na moto pamoja, basi ndivyo hivyo hivyo ni hatari wanawake kuchanganyika na wanaume. Ili kuepusha hatari ya kuripuka moto, kila penye kituo cha petroli limewekwa tangazo la kukataza kuvuta sigara, lakini hakuna mwenye kuona umuhimu wa kuweka tangazo linalokataza wanawake wasichanganyike na wanaume. Kama ni shule tunangojea mpaka msichana apate mimba kisha ndiyo afukuzwe shule. Na kumbe kama tulichukua hadhari ya kuwatenganisha katika masomo lisingalitokea janga hilo. Tunampa adhabu mtoto wa kike kwa kosa lisilokuwa lake. Utachukuaje kitoweo kisichofunikwa ukiweke mbele ya paka, halafu paka yule akakirukia na kukila umfuate paka yule na kumcharaza bakora? Utakapofanya hivyo itakuwa hukutenda haki, umemwonea tu yule paka bure kwa kosa ulilolisababisha wewe mwenyewe. Basi vipi aadhibiwe msichana kwa kubeba mimba na kumbe jamii yenyewe ndiyo iliyomwacha achanganyike kukaa pamoja na wanaume? Uislamu ndiyo maana ukalenga katika kuzuia uovu usitokee na siyo kungojea utokee kisha ndiyo ukaanza kupambana nao kuuondosha. Kuna maana gani kujitumbukiza katika makosa kisha ukaomba msamaha; na hali ipo njia ya kukuzuia usiyaendee makosa? Tuna hakika ganikuwa hakuna akina Clinton wengine au hawatatokea tena akina Monica? Kama wanawake wataachwa waendelee kuchanganyika na wanaume tujue ufuska utaendelea kuwapo na misiba mikubwa itatukumba. Katika matoleo mbalimbali ya magazeti ya Jumatatu, Septemba 14, 1998 kuna habari ya mwanafunzi wa darasa la tano aliyemwua mvulana mwenzie wa darasa la saba katika ugomvi wa kimapenzi wa kugombania msichana, anayesoma darasa la tano katika shule moja ya msingi mkoani Iringa. Sababu kubwa iliyofanya itokee ajali hiyo ni ile tabia yakuwachanganya wanafunzi wa kike na wa kiume, waliokwisha baleghe wasome pamoja. Tungalifuata Qur'an tukufu ilivyoagiza tusingalifikwa na maafa kama haya. Inabidi tukiri kuwa sharia ya Kiislamu ndiyo inayofaa kutawala maisha ya wanadamu wote, popote walipo na katika zama zozote ziwazo. |
YALIYOMO
TAHARIRI Hakuna Muislamu aliyekufa kutokana na vurugu Mgogoro wa kiwanja Duma: Wakatoliki wasema kuna njama za Waarabu Same Na Mwandishi Wetu Wanawake wakutana Mwanza na kusema: Kunyanyaswa sasa basi Na Mwandishi Wetu, Mwanza Sheikh Omar Bashir ataka Waislamu waimarishe mshikamano Na Said Sharif Ustaadhi Abdallah Mfoyi afariki Na Muhibu Saidi Baraza Kuu halina Katibu Nguruka - Sheikh Kilima Na Abu Adli Viongozi Msikiti wa Ubungo Darajani waitwa polisi Na Kassim Juma Marekani `ilivyosaidia' Mujahidiin Barua ya mtoto wa miaka minne toka Lebanon kwa Bibi Hillary Clinton Ujumbe wa waandishi kwa Bw. Batendi, Wakristo Na Muhibu Saidi Waislamu wanadhalilishwa au wanajidhalilisha Tusiwe Jogoo wa Esopo na Almasi Na MAALIM ALI BASSALEH Sherehe za wiki ya usalama barabarani: Kauli nzito za waheshimiwa zimekalia kuti kavu Na Said Omar Mwanasayansi Avicenna: Tabibu bingwa. Na Dk. A. A. Amur Ujenzi wa Msikiti wa Ijumaa Mriti waanza Na Nasib A. Mziray Kutoweka kwa hazina adimu za kimazingira Na Yassir Salim Mfalme Najashi ni mfano bora wa kuigwa kwa watawala Na Idi Kikong'ona Waislamu Moro wasaidia wagonjwa Na Mwandishi Wetu, Morogoro KUFUATIA KUTISHIA MAGAZETI: Sheikh Ayoub amjibu Askofu Rajab Rajab Na Mussa Ally TAMSA Tanga waahidi kuendeleza mema Na Ibn Mohammed, Tanga Ufugaji, uuzaji nguruwe wakera wananchi Dar Na Mwandishi Wetu Mafundisho ya Quran Kuwepo kwa ufufuo Barua za wasomaji
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org