NASAHA
Na. 071 Jumatano Oktoba 25 - 31, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
'Mdahalo' umekwisha: 
CCM haikujibu hoja za Lipumba
  • Mkapa alijisahau kuwa naye ni mgombea 
  • Mrema, Cheyo wamejiharibia 


Na Waandishi Wetu 
 

HATIMAYE ile safari kuelekea Oktoba 29 inakamilika ambapo wagombea urais sasa wanakaa chini kusubiri uamuzi wa watanzania baada ya wao kushiriki katika 'mdahalo' wa aina yake uliodumu kwa zaidi ya miezi miwili ya kampeni.

'Mdahalo' huo umewapa wananchi fursa ya kujua uwezo wa wagombea hao kuyatambua, kuyachambua kujua kiini chake na kushauri juu ya namna bora ya kuyashughuukia masuala mbalimbali ya kitaifa. 

Uchunguzi wa gazeti hili uliodumu kwa urefu sawa na kipindi cha kampeni umeonesha kuwa 'chati' ya Profesa Ibrahimu Lipumba anayegombea Urasi kwa kwa tiketi ya CUF-CHADEMA imepanda kutokana na uwezo wake wa kutambua, kuanisha na kupendekeza ufumbuzi wa mausala kadhaa ya kitaifa ikiwemo kilimo, afya, elimu na uongozi bora. 

Aidha, uchunguzi huo umeonesha kuwa wagombea wengine toka kambi ya upinzani ambao wanaungwa mkono na vyama vyao pekee, Bw. Augustine Mrema (TLP) na Bw. John Cheyo (UDP) "wamejiharibia" baada ya kuacha kuzungungumzia masuala ya kitaifa na, badala yake, wakaanza 'kumkandia' Prof. Lipumba, jambo ambalo limepelekea wananchi kudai kuwa wagombea wawili hao ni kama mapandikizi katika kambi ya upinzani toka chama tawala cha CCM. 

Kadhalika matokeo ya uchunguzi huo yameonesha kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Bw. Benjamin Mkapa, mara nyingi, amekuwa akihutubia katika mikutano yake ya kampeni kama Rais wa nchi na siyo mgombea ambapo wananchi wamedai Bw. Mkapa alikuwa mkali, mwenye kutoa vitisho dhidi ya wafuasi wa vyama vya upinzani na viongozi wao, badala ya kuomba kura zao. 

Aidha Bw. Mkapa ambaye ndiye kiongozi wa serikali inayoondoka madarakani hakuwa akijibu hoja za wapinzani dhidi ya serikali yake; badala yake aliishia kutoa visingizo tu. 

Uchunguzi huu wa NASAHA pia umeonesha kuwa ukali na vitisho vya Bw. Mkapa haikuwa kwa wananchi wa kambi ya upinzani tu bali hata wale wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao yeye ni Mwenyekiti wa Taifa. 

Katika baadhi ya mikutano yake Bw. Mkapa aliwaambia wanaCCM ambao hawakuridhishwa na maamuzi ya vikao vya CCM vya Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati Kuu ya halmashauri hiyo watoke katika chama hicho. 

Wana-CCM katika majimbo mbalimbali walikuwa wakilalamikia uamuzi wa vikao hivyo kutowapitisha wagombea waliopitishwa na wana-CCM hao katika kura za maoni katika majimbo yao na badala yake CCM Taifa kuteua wagombea wengine wasio chaguo la wana-CCM katika majimbo hayo. 

Aidha, huko visiwani Zanzibar, Wazanzibar walisikitishwa na uamuzi wa Halimashauri Kuu ya taifa ya CCM kumteua Bw. Amani Karume ambaye katika kura za maoni zilizopigwa na Wazanzibar wenyewe alishika nafasi ya tatu, badala ya kumpitisha Dk. Mohamed Bilal ambaye aliongoza katika kura hizo akifuatiwa na Bw. Abdisalam Hatib. 

"...lau kama Amina (Bi Amina Salum Ali, Waziri wa Fedha katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar) asingeshiriki kura hizo, basi Karume angeshika mkia,... kwa kweli Karume si chaguo letu asilani", aliwahi kufafanua mkereketwa mmoja wa CCM toka kisiwani Unguja. 

Wananchi waliozungumza na gazeti hili wamemuelezea Prof Lipumba kuwa ndiye mgombea pekee katika nafasi ya urais aliyeonesha upeo wa juu wa uchambuzi wa masuala yanayowagusa wananchi kitaifa. 

"Profesa Lipumba sio tu ni msomi bali pia ni mtaalamu...alipokuwa akimshauri Mzee Mwinyi (Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili) wakati wa Urais wake mambo ya nchi yetu yalianza kunyooka, lakini Mzee 'Ruksa' alipoanza kusikiliza yaliyotakiwa na NEC (Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM), Profesa akajitoa na hapo ndipo chombo kikaanza kwenda mrama", alieleza mwananchi mmoja ambaye alidai ni msatafu toka serikalini. 

Aidha, wananchi hao wamesema wamefurahishwa na mikutano ya kampeni ambayo wameilezea ilikuwa kama mdahalo ambapo wagombea walikuwa wakipeana hoja ingawa wengine walishindwa kujibu. 

"Hotuba toka pande zote ilikuwa ni mdahalo wa kutosha..." alieleza Bi Elionora Macha wa Kinondoni B, jijini Dar es Salaam. 

Wakifafanua kilichomponza Bw. Mrema hadi kufikia kuonekana kuwa yeye ni kama pandikizi ndani ya kambi ya upinzani, wananchi hao wamesema wakati wapinzani walipokuwa wanajadiliana kuungana na kumsimamisha mgombea moja tu, Bw. Mrema alitaka apitishwe mgombea aliyepata kura nyingi katika uchaguzi mkuu wa 1995, "na tunajua aliyepata kura nyingi mwaka 1995 ni Mkapa, kwa hiyo ni wazi Mrema alikuwa anampigia debe Mkapa kwa wananchi; sasa kama huyu sio pandikizi ni nani basi". 

Wakimsimulia mgombea urais kwa tiketi ya UDP, Bw. Cheyo, ambaye aliishutumu CUF kwa kudai kuwa ina udini, wananchi wamesema kuwa yeye ni mbinafsi. 

"ikiwa ni kweli CUF kuna udini yeye Bw. Mapesa (Bw. Cheyo) aliwezaje kukaa nao bungeni kwa miaka mitano tena chini ya uongozi wa Mbunge wa CUF, Mama (Fatma) Maghimbi... yaani alitaka tuamini kuwa udini ameuona baada ya Bunge kuvunjwa!", walimshutumu Bw. Cheyo na kuongeza: "yeye ni m-binafsi na hana tofauti na Mrema kwani wote wanaelekea kuwa ni mapandikizi wa Chama tawala" 

Katika kura ya maoni iliyoendeshwa wakati wa uchunguzi wa gazeti juu ya uwezo wa kila mgombea kuchambua na kutaja namna masuala mbalimbali ya kitaifa yanavyoweza kushughulikiwa , wananchi hao walimpa Profesa Lipumba 95%, Rais Mkapa 43%, Bw. Cheyo 21%, na Bw. Mrema 19%. 

Wakitolea mfano wa jinsi Profesa Lipumba alivyoonesha kuweza kuyachmbua masuala walisema: "Daktari bora ni yule anayempima mgonjwa (ili) kufahamu tatizo lililopo, chanzo cha tatizo hilo na kisha ndio kutoa ufumbuzi wake". 


Mkapa uzalendo umemshinda
  • Ashangaa kwa nini wapemba hawarudi kwao 
  • Wananchi wasema CCM haiuheshimu tena Muungano 
Na Mwandishi Wetu 

KAULI ya Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Benjamin Mkapa kuwashangaa Wapemba ni kwa nini hawawekezi kwao Kisiwani Pemba, imeshutumiwa vikali na wananchi kwa madai kuwa Bw. Mkapa, kama Mtanzania mwenzao amekosa uzalendo.

Bw. Mkapa anadaiwa kutoa kauli hiyo katika mkutano wake wa kampeni alioufanya Micheweni, mkoa wa Kaskazini Pemba, Oktoba 19, mwaka huu. 

Wananchi waliozungumza na gazeti hili katika nyakati tofauti kufuatia kauli hiyo ya mgombea urais wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayemaliza muda wake wamesema ni jambo la kusikitisha kuona Rais mwenyewe ameshindwa kufanya uchambuzi wa kina kuweza kujua tatizo halisi la kisiwa cha Pemba kuwa nyuma kimaendeleo. 

Wamesema wapemba ni sehemu ya raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo wana haki kamili ya kuishi sehemu yoyote ile ya Jamhuri. 

"Watanzania sote ni kitu kimoja ndio sababu Wahaya na Wamachinga wanafanya biashara zao hapa Dar es Salaam lakini hakuna anayewagusa; kadhalika, Wachaga wanaendesha biashara zao Mwanza, Tabora na kwingineko lakini hakuna anayestaajabia jambo hilo", alieleza mwananchi mmoja mkazi wa Sinza Madukani jijini ambaye hakutaka atajwe gazetini. 

Akichambua sababu za kitaalamu zenye kumfanya mtu yeyote atake kuwekeza sehemu fulani , Mwalimu mmoja katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), pia cha jijini, amesema ni kuwepo kwa huduma za kiuchumi ambazo ni pamoja na njia bora za uchukuzi, mawasiliano, huduma za kibenki, maji na umeme. 

"Lakini huduma hizi za kiuchumi katika nchi zetu hizi ni jukumu la serikali... barabara zote hizi hapa Dar es Salaam au Arusha au Moshi au mkoa mwingine wowote ule zimejengwa na serikali, vivyo hivyo vituo vya kuzalisha umeme na network zake (mitandao yake) ni kazi ya serikali", alisema mwalimu huyo na kuongeza kuwa mambo hayo ndiyo yenye kupelekea mji kukua na watu kukimbilia kuanzisha biashara mbalimbali. 

Wananchi hao wamesema alichotakiwa kusema Bw. Mkapa ni kwa nini serikali ya CCM kwa miaka yote hii tangu muungano mwaka 1964 haikukiendeleza kisiwa hicho cha Pemba kiasi cha kuwavutia watnzania wakimbie kuwekeza kisiwani humo. 

"Kama yeye Rais (Mkapa) aliona chama chake hakina sababu ya msingi za kushindwa kuanzisha huduma za kukuza uchumi huko kwa wapemba, angekiri tu kwamba walizembea na akaahidi kuwa jambo hilo litarekebishwa", alisema Bw. Valentine Muro wa Mwenge Dar es Salaam na kuongeza: "...lakini tabu ya rais wetu anataka kuhalalisha hata lisilo halali". 

Aidha, wananchi hao wamesema hakuna mfanyabishara anayeweza kufungua biashara mahali ambapo wakazi hawana uwezo wa kununua bidhaa anazoiuza. 

"...unapotaka kuanzisha biashara ni lazima ugalie purchasing power (uwezo wa watu kumudu kununua bidhaa), bila hivyo bidhaa zitadorora dukani ... matokeo yake ni mabaya na kama ulikopa mtaji ujue ndio umekwisha kwa sababu benki watakufilisi kwa kushindwa kulipa hela yao." 

Kadhalika, wananchi hao waliuozungumza na gazeti hili pia wamehoji ni kwa nini serikali haijafanya juhudi za makusudi za kuinua kipato cha wakazi wa Pemba. 

"Kwa kawaida serikali huwa inaiinua miji fulani ili kuwaletea hali bora wakazi wake; kwa mfano serikali iliamua kujenga kiwanda cha nguo cha Mutex katika mji wa Musoma ingawa kiuchumi kiwanda hicho hakikufaa kuwekwa huko kwa vile tayari kulikuwa na kiwanda kingine cha nguo cha Mwatex pale Mwanza... lakini ile ilikuwa ni njia ya kuwapiga jeki wakazi wa Musoma", alidai mwalimu huyo wa CBE. 

Mwishoni mwa wiki vyombo vya habari viliripoti habari kuwa Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Bw. Mkapa amesema hali ya umasikini iliyopo kisiwani Pemba haikutokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na akaongeza kuwa wapemba walioko nje ya kisiwa hicho warudi kuja kuwekeza. 

Likiripoti habari hizo gazeti moja la kila siku toleo la Oktoba 21, mwaka huu lilimnukuu mkapa akisema: "wafanyabiashara wapemba wamejaa toka Kinondoni hadi Kahama Shinyanga, wapinzani wangewashauri hao wote warudi kuweka vitega uchumi hap kisiwani". 


Wananchi kuhakikisha haki inatendeka
  • Ngangari wasema kura haziibiwi 
  • Atakayeiba atakiona 
  • Afrika Kusini waliteswa na kuuawa, lakini ushindi ulipatikana 


Na Mwandishi Wetu 

UCHAGUZI wa mwaka huu unatarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake ambapo wapiga kura, baada ya kuzisoma kanuni mbalimbali zinazotakiwa katika zoezi lote la uchaguzi kama zilivyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wameazimia kulifuatilia zoezi hilo kwa karibu zaidi kuhakikisha kuwa zinafuatwa na haki inatendeka.

Aidha, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wapiga kura hao, hususan wanaoiunga mkono kambi ya upinzani, "mwaka huu wamejizatiti kukabiliana na propaganda zozote zitakazoenezwa katika dakika za mwisho ". 

Wananchi waliohojiwa na gazeti hili wamesema wao wenyewe watakuwa waangalifu na hawataruhusu kura za wizi. 

"Kura hazitaibiwa wala hakuna mgombea atakayeweza kujiwekea kuraza bandia", alisema mmoja wa wananchi hao na kuongeza kuwa hata utafutaji wa jumla ya kura utadhibitiwa. 

Wakirejaea hali ilivyokuwa nchini Zimbabwe wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu, wananchi hao amesema wanafahamu kwamba gharama ya kupata haki ni kubwa lakini wao wapo tayari. 

"Zimbabwe wapinzani wa Mugabe walikuwa wakishambuliwa na dola, watu 50 waliuawa lakini wapinzani walijizolea viti. 

"... hata South Africa (Afrika ya Kusini wafuasi wa Mandela walitaabishwa sana na makaburu lakini mwisho wa yote walishinda", alisema mwananchi mwingine. 

Akizungumza na gazeti hili, mjumbe mmoja wa Halmashauri ya Kumuimarisha Profesa Lipumba amesema: "mwaka 1995 propaganda nyingi dhidi ya Profesa zilitukuta hatujakaa sawasawa, lakini mwaka huu tupo ngangari". 

Mjumbe huyo ambaye tangu alipoanza kutoa habari za Halmashauri hiyo iliyoundwa Mwanza mwezi Agosti mwaka huu hajakubali kutajwa jina lake gazetini amekumbushia propaganda kadhaa zilizotolewa wakati wa uchaguzi wa mwaka 1995 ikiwemo madai kuwa Profesa Lipumba alikuwa amechelewa. 

"Ni kweli Profesa alikuwa wa mwisho kujitokeza miongoni wa waliowania urais mwaka huo, lakini huko sio kuchelewa kwa sababu aliyechelewa huwa hajazi fomu...lakini Profesa alijaza fomu na Tume ya Uchaguzi (ya Taifa) ikazipokea na ikampitisha kuwa ni mgombea halali", alieleza mjumbe huyo. 

"...zaidi ya hapo wakazusha tena eti Profesa hafahamiki kwa watu wengi hasa wa vijijini kwa hiyo kumpigia kura itakuwa ni kupoteza bure kwa sababu hawezi kushinda", aliendela kusimulia mjumbe huyo. 

Aidha, kulikuwa na hofu kwamba sehemu ya kura alizopata Profesa Lipumba mwaka 1995 'zilifanyiwa mchezo'. Dai hili linapata nguvu kutokana na ukweli kwamba baada ya uchaguzi huo kesi nyingi kupinga matokeo zilifunguliwa ambapo pamoja na kukiukwa kwa taratibu nyingine za kanuni za uchaguzi, baadhi ya malalamiko yalihusu wizi wa kura . 

Taarifa ambazo gazeti hili imezipata ni kwamba mpaka sasa kesi moja ya uchaguzi ya mwaka 1995 bado ipo mahakamani. 

Aidha, mwanasheria mmoja ambaye alikuwa akishughulika na baadhi ya kesi hizo aliwahi kutamka kwa mshangao kwamba, "kwa mtindo huu (wa kura kuchezewa ili kumwangusha mgombea fulani) huenda hata kura za presidential candidates (wagombea rais) zingeleta utata kama ingekuwepo ruhusa ya kufungua kesi..." 

Akielezea hali ya mambo ilivyo katika uchaguzi wa mwaka huu, mjumbe huyo wa Halmashauri ya Kumuimarisha Profesa Lipumba amesema: "Safari hii Profesa kajitokeza mapema kabisa, na amewatembela Watanzania nchi nzima. 

"...popularity yake (kufahamika kwake kwa watu) Profesa ni kubwa sana, na kwa hilo hawawezi tena kuwadanganya wapiga kura eti hafahamiki", alisema mjumbe huyo. 

Wananchi wengine wamedai kuwa zimekupo njama za kumhujumu Profesa Lipumba asipate kura nyingi ambapo wametaja matukio kadhaa kuthibitisha madai yao hayo. 

Wakiongea na gazeti hili wananchi hao wamedai siku ya uzinduzi wa kampeni kitaifa baadhi ya magazeti yalitumika "kuvumisha uongo kwamba mkutano wa CUF ulikuwa umefutwa" jambo ambalo halikuwa kweli. 

Wamesema katika siku hiyo hiyo askari wa kutuliza ghasia walitumwa kuwatawanya wanachama wa vyama vya CUF na CHADEMA na wanachi wengine wanaomuunga mkono Profesa Lipumba ili wasihudhurie mkutano wa uzinduzi wa kampeni uliokuwa ukifanyika katika Viwanja vya Kidongo Chekundu, Dar es Salaam. 

Matukio mengine ambayo wananchi hao wameyataja ni kitendo cha mgombea urais wa Jamhuri kwa tiketi ya TLP, Bw. Augustine Mrema kupeperusha bendera ya CUF huku Asofu Zakaria Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship akizunguka nchini kumnadi Bw. Mrema kuwa ndiye anayefaa kuungwa mkono na wapinzani. 

Mjumbe wa Halmashauri ya Kumuimarisha Profesa Lipumba pia ameliambia gazeti hili kwamba halmashuri hiyo , pamoja na mambo mengine, imekuwa ikiwatahadharisha wananchi kwamba katika wiki ya mwisho mambo mengi yatavumishwa kuhusu mgombea wao. 

"Tumekuwa tukiwaambia wananchi kwamba Profesa anaweza kupata mafua kidogo tu lakini magazeti yakaandika 'Lipumba mahututi', au 'Lipumba kajitoa kugombea, ni mgonjwa'". 

Hata hivyo mjumbe huyo amesema kwa jinsi halmashauri yao ilivyoweza kupata mafanikio katika muda mfupi, wale wote wenye nia mbaya na Profesa Lipumba hawatafanikiwa. 

Halmashauri ya kumuimarisha Profesa Lipumba mjini Mwanza baada ya kikao kilichowakutanisha wazee toka vyama vya UDP, TLP, na NCCR-Mageuzi. 

Hoja iliyowakutanisha wazee hao ilikuwa ni kushauriana juu ya namna ya kuiondoa |CCM madarakani. Ilionekana kuwa kwa vile lengo la upinzani ni kukiondoa madarakani chama tawala cha CCM, na kwa kuwa sehemu kubwa ya wananchi wameonesha kuiunga mkono kambi ya upinzani baada ya kuchoshwa na utawla wa CCM, lakini kulikuwa na hatari ya kuzigawa kura zao iwapo wapinzani wangeendelea kusimamisha wagombea zaidi ya mmoja. 

Kwa mujibu wa mjumbe huyo wa halmashuri hiyo, kwa kuwa wagombea wengine wawili wa kambi upinzani - Cheyo (UDP) na Mrema (TLP) - walikuwa wameng'ang'ania kuendelea na nafasi zao wazee hao waliona ni busara kuwaunganisha wapiga kura kupitia ushawishi wa wazee. 

Baada ya kukubaliana, wazee hao walifanya tathmini kujua ni mgombea yupi anayekubalika zaidi na wananchi na hapo ndipo ilipoamuliwa kumuiamrisha Profesa Lipumba. 

Baadaye wazee waliwasialina na wazee wenzao upande wa CUF kutaka kujua kama Profesa angekuwa tayari kufanya kazi na akina Cheyo na Mrema katika serikali mpya iwapo wafuasi wao watamuunga mkono. Wazee wa CUF walisema Profesa Lipumba hana tatizo na wawili hao. 

Kilichofuata, wazee hao waliunda Halmashauri ya Kumuimarisha Profesa Lipumba ambayo wajumbe wake walijigawa katika vikundi vya watu watatu watatu na kuanza kuzunguka nchini kuwaunganisha wapiga kura wamchague Profesa Lipumba. 

Akisifia mafanikio ya Halmashauri hiyo. Mjumbe huyo alisema: "...juhudi yetu haikupotea, (kwa sababu) kila alikopita Profesa alikuwa akipokewa na wananchi wa vyama vyote" 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Chaguo la Wapiga kura liheshimiwe

'Mdahalo' umekwisha: CCM haikujibu hoja za Lipumba

Mkapa uzalendo umemshinda

Wananchi kuhakikisha haki inatendeka

Wanafunzi Chuo Kikuu kuendelea na mgomo

Pengo awatahadharisha wezi wa kura

Taarifa ya kituo cha haki haikuzingatia haki
 
 


   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita