|
Na. 071 Jumatano Oktoba 25 - 31, 2000 |
|
|
|
|
|
Chaguo la Wapiga kura liheshimiwe Sasa tupo kizingitini, tunaingia katika hatua ya mwisho ya uchaguzi nayo ni kupiga kura. Ni Jumapili Oktoba 29, mwaka huu. Watanzania wote waliowahi kujiandikisha na wanazo shahada zao watapiga kura kuchagua Madiwani, Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano, na zaidi ya hao, kwa upande wa Tanzania Visiwani wapiga kura pia watawachagua wawakilishi na Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Awali ya yote tunapenda kubainisha kwamba, kwa yeyote anayeshiriki katika uchaguzi huu - akiwa ni mpiga kura, au mgombea, au msimamizi: KURA ZA WANANCHI ZISICHEZEWE NA CHAGUO LA WANANCHI LAZIMA LIHESHIMIWE. Hii ni mara ya pili Watanzania kushiriki katika uchaguzi chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa; awali ilikuwa mwaka 1995. Lakini safari hii wananchi wana ufahamu mpana zaidi wa ni nini mfumo wa vyama vingi na ni nini upinzani; wanafahamu kwamba mfumo wa chama kimoja cha siasa haikuwa ni amri ya Mwenyezi Mungu bali ilikuwa ni mapenzi ya watu. Miaka mitano inayokamilika hivi sasa imewapa Watanzania fursa ya kuufahamu uwezo, udhaifu na bila shaka mustakabali wa chama tawala. Leo Watanzania wanafahamu ni chama gani kilikuwa madarakani wakati wenzao zaidi ya 40 walipokufa njaa huko Ulanga mkoani Morogoro wakati mahindi yakikosa soko mkoani Rukwa! Leo Watanzania wanafahamu ni serikali ya chama gani ilikuwa madarakani wakati wenzao wakifyatuliwa risasi za moto na askari wa Jeshi la Polisi nchini na kuuawa pale Mwembechai, Februari 1998. Leo wananchi wanafahamu ni chama gani kilikuwa madarakani wakati wenzao wakifyatuliwa risasi za moto na polisi kiasi cha kuvunjwa miguu huko Zanzibar wakati wakihudhuria mkutano wa kampeni za chama cha upinzani mapema mwezi huu. Leo Mtanzania anaingia katika chumba cha kupigia kura akifahamu fika ni serikali ya chama gani ilikuwa madarakani wakati iliposhindwa kutuma jeshi la polisi kwenda kudhibiti mapigano Mererani ambako makumi ya Watanzania wameuawa lakini serikali hiyo hiyo haikukawia kutuma jeshi la polisi kwenda kuwatawanya wananchi wanaohudhuria mikutano ya kampeni inayohutubiwa na viongozi wa vyama vya upinzani. Leo Mtanzania anaingia kupiga kura akiwa na kumbukumbu 'mbichi' ya chama kilichotajika sana kwa rushwa na mizengwe ya kuhujuimana wao kwa wao wakati wa hatua za awali za zoezi hili la uchaguzi mkuu. Tunaamini kila mpiga kura, baada ya kujikumbusha haya, ataweza kuamua ikiwa atapiga kura yake kukirejesha chama tawala madarakani au ataipa nafasi kambi ya upinzani idhihirishe umahiri wake. Lakini, kupambanua kati ya chama tawala na upinzani pekee hakutoshi; upambanuzi pia unatakiwa miongoni mwa vyama vilivyoko katika kambi ya upinzani. Kwa mfano, "ni chama kipi kimetangaza sera inayolenga kumkomboa mwananchi; sera inayozungumzia bayana masuala elimu, afya na matibabu, ajira, uboreshaji wa kilimo na soko bora la mazao, mfumo bora wa kodi, vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu serikalini, na uongozi bora". Chama ambacho sera zake zina elekea kutekelezeka na wala sio chama ambacho kinaigia madarakani kwa mbwembwe halafu, miezi michache baadaye kinawatangazia wananchi eti, "ilani ya uchaguzi haitekelezeki". Leo Watanzania wanafahamu ni vyama gani vimeonesha mwelekeo wa kuheshimu na kudumisha umoja wa Watanzania kiasi vyama hivyo vikakubalina kuunganisha nguvu zao katika uchaguzi huu. Baada ya ukumbusho huu tunaamini kila mpiga kura ataingia katika chumba cha kupigia kura akijua ni nani au ni chama gani akipige kura; ni chama gani akikopeshe kura yake ili kimlipe maendeleo. Baada ya kuongea na wananchi sasa tunarudi kwa chama tawala na pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Wawili hawa tunawakumbusha kwamba kura za wanachi ziheshimiwe, chaguo la wananchi liheshimiwe na u-Milosovic usikaribishwe nchini. WATANZANIA WOTE MLIOJIANDIKISHA JITOKEZENI
MKAPIGE KURA, NA BAADA YA HAPO MSISAHAU 'MLINZI WA KURA NI WA MPIGA KURA
MWENYEWE'.
|
YALIYOMO
Tahariri
'Mdahalo' umekwisha: CCM haikujibu hoja za Lipumba Wananchi kuhakikisha haki inatendeka Wanafunzi Chuo Kikuu kuendelea na mgomo |
|
|
|
|