NASAHA
Na. 035 Jumatano Februari 16 - 22, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MICHEZO

Tauzany afurahia ligi ya makundi 

  • Lakini atiwa kiwewe na kundi la Simba 
  • Aliita la maafa 
Na HAMIS KASABE 

KOCHA Mkuu wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Nzoyisaba Tauzany amefurahishwa na kitendo cha FAT kubadili mfumo wa ligi kuu Tanzania Bara na kuwa katika mtindo wa makundi.

Nzoyisaba amedhihirisha furaha hiyo Jumatatu wiki hii mbele ya mwandishi wa habari hizi wakati akifanya mahojino maalum. 

"Sababu ni nyingi kwa kweli za ubora wa mfumo huu, kwanza, muda utakuwa mfupi wa ligi, kitu ambacho kitawapa muda mzuri wachezaji wetu wa kupumzika. 

"Vile vile kutakuwa na matumizi kidogo ya fedha kwa vilabu katika kugharamia timu kutokana na ligi kutokuwa ndefu", amesema. 

Nzoyisaba anaamini kuwa soka ya Tanzania itakuwa kwa kasi na hata kufikia kiwango cha soka la Afrika Magharibi kama Cameroun, Nigeria na Ghana endapo FAT wataendelea na mfumo huu mpya. 

Akizungumzia kauli za baadhi ya wanamichezo na viongozi wa vilabu waliojitokeza kupinga mfumo wa makundi, Nzoyisaba alisema, kupinga huko kunatokana na hofu ambayo anadhani imesababishwa na viongozi hao kutoziamini timu wanazoshabikia. 

Mara baada ya FAT Taifa kutangaza mfumo huo mpya wa ligi mapema wiki iliyopita, viongozi kadhaa walijitokeza kupinga, akiwemo Katibu wa chama cha soka mkoa wa Tanga, Salim Bawazir na viongozi wa CDA ya Dodoma. 

Kwa mujibu wa viongozi hao, mfumo huo mpya wa ligi utasababisha wachezaji wengi kutocheza kwa muda mrefu endapo timu zao zitatolewa mapema na hivyo kuviza vipaji vyao. 

"Sasa kama timu yako ni mbovu, kwanini isitolewe mapema, na ikitolewa si ndio unapata nafasi ya kutosha ya kujizatiti kwa ajili ya mwaka unaofuata kuliko kuendelea kupoteza muda na fedha wakati timu inafanya vibaya", amefafanua Nzoyisaba. 

Pamoja na kufurahia mfumo wa makundi, Nzoyisaba ameonesha wasiwasi juu ya kundi ambalo timu yake imepangiwa, kwa kulitaja kuwa ni kundi bora kabisa na gumu ukilinganisha na mengine. 

Kulingana na ratiba iliyotolewa na FAT hivi karibuni, Simba imepangwa kundi moja na Majimaji ya Songea na Prisons ya Mbeya ambao ni mabingwa wa Tanzania 1998 na 1999 pia zimo timu za Tukuyu Stars ambao ni mabingwa wa Tanzania Bara 1986 na Lipuli ya Iringa. 

Nzoyisaba amepuuza madai ya baadhi ya washabiki kuwa Majimaji ya leo ni dhaifu kutokana na kukimbiwa na nyota wake wengi. 

"Nani anasema Majimaji ni dhaifu, mimi nakwambia, ile ni timu nzuri kwa sababu wamesajili vijana wengine wazuri ambao mimi nawafahamu", amesema. 

Aidha, Nzoyisaba amekiri kuwa kundi linalofuatia kwa ubora ni lile linalojumuisha timu za Bandari, Kariakoo, Reli, Kajumulo na Yanga. 


Kibadeni hakutokomea na fedha za usajili- Milambo

  • Yadai alifanya usajili kwa uaminifu 


Na Mwandishi Wetu 
 

VIONGOZI wa timu ya soka ya Milambo ya Tabora wamekanusha habari zilizoandikwa na gazeti moja litolewalo mara mbili kwa wiki jijini jana, kwamba aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Abdallah 'King' Kibadeni ametokomea na fedha za klabu hiyo.

Kanusho hilo limetolewa na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Abdul Ezat jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na NASAHA.

Ezat amesema habari hizo siyo sahihi na zilitolewa kwa lengo la kuharibu uhusiano mzuri uliopo kati ya uongozi wa Milambo na Kibadeni. 

"Ukweli ni kwamba Kibadeni tulimpa fedha ambazo si zaidi ya shilingi laki tatu, afanye usajili wa baadhi ya wachezaji wetu, kitu ambacho alifanya kwa uaminifu", amesema. 

Aidha, Mwenyekiti huyo amemuomba radhi Kibadeni ambaye yupo nchini Brazil kwa usumbufu wowote alioupata kutokana na habari hizo. 


FAT yamuangukia Gama 

  • Dk. Gama ni mdhamini wa chama cha mpira wa miguu nchini 


Na Mwandishi Wetu 
 

KAMATI ya Utendaji ya chama cha soka nchini (FAT) imemuomba radhi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Laurance Mutazama Gama kufuatia habari zilizotolewa na Mjumbe wa Kamati hiyo, kwamba Gama siyo mdhamini wa FAT.

Wiki kadhaa zilizopita Mjumbe wa kamati hiyo ya utendaji, Abdallah Majura Bulembo alinukuliwa na vyombo vya habari nchini akidai kuwa Dk. Gama siyo mdhamini wa FAT kama ambavyo imekuwa ikielezwa na vigogo wa chama hicho. 

Kwa mujibu wa taarifa ya FAT kwa vyombo vya habari iliyopatikana jana, habari iliyotolewa na Bulembo siyo sahihi. 

Kwa kuwa habari za Bulembo siyo sahihi Taarifa ya FAT imedai Kamati ya Utendaji imemuagiza Mwenyekiti wa FAT, Muhidin Ndolanga kumuomba radhi Gama. 

Pia kamati ya utendaji imemuagiza Bulembo kumuomba radhi Gama pamoja na kufuta taarifa yake aliyoitoa kwa wanahabari. 

"Kamati ya Utendaji inaendelea kutambua na kuheshimu ya kuwa Dk. Gama ni mdhamini wa chama cha mpira wa miguu nchini. 

"Mwisho Kamati ya utendaji inaomba radhi kwa Dk. Gama kwa usumbufu alioupata kutokana na taarifa potofu iliyotolewa na Bulembo", imemalizia taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FAT Ismail Aden Rage. 

Naye Bulembo akizungumza na NASAHA jana kuhusu suala hilo alisema atatoa taarifa rasmi leo. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri:
Serikali itoe hatma ya mauaji ya Mwembechai 

Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa 

Kanisa liliishinikiza serikali-Waislamu

Sakata ya mabadiliko ya Katiba Zanzibar 

Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu 

HABARI ZA KIMATAIFA 

Ushauri Nasaha  
Kuongoza tabia za watoto 

MAKALA 
Uhuru wa pili na ukombozi wa mwananchi 

MAKALA 
Umuhimu wa uchumi katika Uislam 

Kalamu ya Mwandishi 
Kwa nini kadhia ya Mwembe Chai isifanyiwe uchunguzi? 

Makala 
UPINZANI  OCTOBA 2000 - 3 

MAKALA
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA  JAMHURI YA MUUNGANO: Wananchi Tanzania amkeni 

Riwaya 
Ndoto ya mafanikio 

LISHE 
Vyakula vitupatiavyo mafuta 

Barua/Maoni

MASHAIRI

MICHEZO

  • Tauzany afurahia ligi ya makundi 
  • Kibadeni hakutokomea na fedha za usajili- Milambo 
  • FAT yamuangukia Gama

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita