NASAHA
Na. 035 Jumatano Februari 16 - 22, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Kalamu ya Mwandishi 

Kwa nini kadhia ya Mwembe Chai isifanyiwe uchunguzi?

NA MAALIM BASSALEH

BAADA ya kuwekewa ngumu, katika dakika za mwisho na wamiliki wa ukumbiwa Diamond Jubilee, Jumapili iliyopita, tarehe13-02-200,Waislamu wa Dar es Salaam, pamoja na wenzao, wawakilishi kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania, wanaume kwa wanawake, walifurika katika Msikiti mpya wa Tanzania Islamic Centre, uliopo Magomeni, kichangani, kwa ajili ya kuwaombea dua ndugu zao, waliopoteza roho zao, katika kadhia ya MwembeChai, pamoja na kuwarehemu masheikh mbalimbali waliokwisha tangulia mbele ya haki ambao walikuwa mstari wa mbele katika kuupigania Uislamu na haki za Waislamu, katika nchi hii.

Ilikuwa ni miaka miwili iliyopita, Februari 13, 1998, ndipo Waislamu hao walipouawa kikatili, kwa kupigwa risasi na polisi, katika ghasia zilizotokea katika eneo la Msikiti wa MwembeChai, Magomeni, jijini, Dar es Salaam. Aidha, katika mtafuruku huo Waislamu wengine walijeruhiwa vibaya akiwamo kijana Chuki Athumani aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondai ya Al-Haramain, ambaye kwa hivi sasa amekuwa ni mlemavu. 

Mengi yalisemwa juu ya chanzo cha ghasia hizo. Mwanzo ilikuwa nikuwasaka wachochezi wa kidini wanaokashifu dini za wengine. Baadaye tukaambiwa kuwa ghasia hizo zilichochewa na baadhi ya balozi za nchi za nje zilizopo hapa nchini, bila ya kutajwa, ni balozi gani hizo. 

Kisha tukaambiwa ni Waislamu wenye siasa kali ndio walioaanzisha fujo hizo. Mara tukaelezwa kuwa ni mujahidiana waliouvamia Msikiti huo wa Mwembechai na kulundika sialaha humo msikitini ndio waliokuwa chanzo cha ghasia hizo. Na hatimaye tukaelezwa kuwa ghasia hizo hazihusiani kabisa na mambo ya kidini; bali zimetokana na fujo za wahuni wachache. 

Kauli zote hizo ni zenye kutatanisha. Ni uropokwaji tu! Ni kauli zisizokuwa na ushahidi wowote. Ni shutuma zisizokuwa na msingi. Kauli za aina hii hazifai kabisa kutolewa na mtu mwadilifu sembuse awe kiongozi au ofisa wa Kiserikali, mwenye dhamana ya kusimamia haki na uadilifu katika nchi. 

Kauli zote hizo hazioneshi nani au nini hasa kilichosababisha kadhia nzima ya Mwembechai isipokuwa zinazidisha utata wa swali lenyewe. Lakini roho za watu zimetoka na wengine wamejeruhiwa vibaya; pia, mali zimeharibiwa. Nini chanzo cha yote hayo? Kila upande unatoa jawabu yake. 

Tumeona viongozi wa Serikali, kwa upande wao walivyotoa maelezo yenye kutatanisha na mwisho serikali ikasema kuwa ghasia hizo hizihusiani na mambo ya kidini. 

Lakini Waislamu kwa upande wao wanaona mbona waliouawa katika ghasia hizo ni Waislamu tu? Aidha, wanauliza mbona walikamatwa Wakristo na Waislamu kwa kuhusika kufanya fujo hizo; lakini baadaye Wakristo wakaachiwa na Waislamu wakafunguliwa kesi. Mpaka hivi leo kuna zaidi ya kesi thelathini mahakamani, kuhusu ghasia za Mbwembechai, zinazowakabili Waislamu. Vipi basi, wanauliza, Waislamu kadhia hiyo iambiwe kuwa haikuwa na mtazamo wa kidini? 

Waislamu wanahisi kadhia yote ya Mwembechai, imetokana na shinikizo la baadhi ya viongozi wa kanisa kuitaka serikali iwadhibiti wahadhiri wa Kiislamu, ambao walishutumiwa kwa kuendesha mihadhara ya kuukashifu Ukristo. Ilikuwa ni vyombo vya dola katika kutaka kuwadhibiti wahadhiri hao ndiyo likatokea sokomoko hilo. 

Katika hali kama hiyo, ambapo pande mbili zinahitalifiana, na hasa kwa vile serikali yenyewe ilikuwa ikitoa kauli zenye kutatanisha juu ya chanzo cha kadhia hiyo ilitarajiwa serikali ingaliona umuhimu wa kuunda tume huru kuchunguza chanzo cha kadhia hiyo na pia, kuwajua wale waliosababisha. Lakini inastaajabisha kuwa serikali haikuona umuhimu wa kufanya hivyo. 

Na hata Waislamu walipoiomba serikali iunde tume kama hiyo bado serikali ilikataa, na kusema haioni haja ya kuunda tume kama hiyo. Jambo hilo limewapelekea Waislamu wahisi kuwa hawakutendewa haki. 

Lakini kwa mujibu wa maelezo ya wanasheria wanasema kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi, kifo chochote kilichotokea ndani ya mikono ya Polisi au Magereza lazima kifanyiwe uchunguzi wa kisheria unaoitwa INQUEST. Ingawa Waislamu wamewasilisha maombi yao ya kutaka ifanywe INQUEST hiyo, katika vyombo vinavyohusika, lakini hawajapewa jawabu lolote mpaka hivi sasa! 

Swali wanaloliuliza Waislamu ni kwa nini serikali inaweka ngumu usifanywe uchunguzi wa kisheria juu ya kadhia ya Mwembe Chai? Nini kinachoogopewa au kufichwa? 

Ama yale madai ya kusema kuwa wahadhiri wa Kiislamu wanaendesha mihadhara ya kukashifu Ukristo hayo si madai sahihi. Hizo ni jazba tu za baadhi ya viongozi wa kanisa wanaoona wivu juu ya wahadhiri wa Kiislamu wanaovyoweza kujenga hoja kwa kutumia Biblia na kuwasilimisha mamia ya Wakristo. Jambo hili limewatia hofu kubwa Makasisi. 

Lakini hizo kashfa za kidini ni nini? Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Al-Haj Ali Hasaan Mwinyi, aliwahi kuwaita viongozi wa Kikristo pamoja na wa Kiislamu,Ikulu, na kuwataka wajadili nini maana ya kashfa za kidini. Mkutano huo ukashindwa kutoa jibu sahihi. 

Ukizichunguza hizo zinazoitwa kashfa za kidini wanazodaiwa kuzifanya wahadhiri wa Kiislamu utakuta wahadhiri hao wanashutumiwa kwa mambo matatu. Kwanza, wanaambiwa wanatumia kitabu kisicho chao katika mahubiri yao. Badala ya kutumia kitabu chao, Kur-ani wao wanatumia Biblia, ambacho ni kitabu cha Wakristo. Pili, wanashutumiwa kwa kuikosoa Biblia pamoja na mafundisho ya Kikristo. Na mwisho wanalaumiwa kwa kuukana uungu wa Yesu, wao wanasema Yesu si Mungu. 

Shutuma zote hizo tatu hazithibitishi kuwapo kwa kashfa za kidini! Kwanza ikiwa muumini wa dini moja kutumia kitabu cha dini nyingine, ndiyo kashfa, basi Wakristo ndio walioanzisha mtindo huo! Tafsiri ya kwanza ya Kur-ani Tukufu, kwa lugha ya Kiswahili, huku kwetu Afrika Mashariki, imeandikwa na Padre Geoffrey Dale wa Shirika, la U.M.C.A., Zanzibar. Na katika tafsiri yake hiyo amepotosha, kwa makusudi, maana halisi ya aya zilizomo katika kitabu hicho. Lakini hatukusikia Padre huyo akishutumiwa kuwa ameukashifu Uislamu! 

Pili kama kukosoa mafundisho ya dini nyingine ndiyo kashfa, basi kwanza ingalibidi ashutumiwe Padre Anglars wa Kanisa Katoliki kwa kuukashifu Uislamu. Yeye ameandika kitabu alichokiita "Wana wa Ibrahimu." Katika kitabu hicho ameyakosoa mafundisho ya Uislamu, Kur-ani Tukufu pamoja na Mtume Muhammad (s.a.w.). Mbona haijadaiwa kuwa Padre Anglars ameukashifu Uislamu? 

Au kashfa huwapo pale Mwislamu anapoukosoa Ukristo tu; lakini Mkristo akiukosoa Uislamu huwa si kashfa? Au kukosoa mafundisho ya dini nyingine kwa kuandika vitabu huwa si kashfa, bali kashfa huwa pale yule mwenye kuikosoa dini nyingine anapofanya hivyo kwa kutumia vipaza sauti? 

Ama kusema Yesu si Mungu hiyo haiwezi kamwe kuitwa kashfa. Ni kweli kuwa ndugu zetu Wakristo wanateseka sana wanaposikia Waislamu tukisema Yesu si Mungu lakini hiyo ndiyo imani yetu Waislamu. Na ndivyo hivyo hivyo Waislamu wanahesabu ni kufuru hasa kusema Yesu ni Mungu, lakini hiyo ndiyo imani ya Wakristo. 

Na kila mmoja ana haki ya kuamini dini anayoitaka, pamoja na kuitangaza imani yake hiyo hadharani. 

Jee! Baina ya hao wawili nani anayemkashifu mwenziwe. Ni Waislamu wanaosema Yesu si Mungu, au ni Wakristo wanaosema Yesu ni Mungu? 

Kwa kweli ,mambo haya hayahitaji hoja za nguvu na jazba; bali yanahitaji hekima, busara na nguvu za hoja. Ni wajibu wa dini zote mbili kuvumiliana. Ni uvumilivu tu ndio utakaoondosha jazba za kila upande. 

Kuna wanaowataka wahadhiri wa Kiislamu waache kutumia Biblia, katika mahubiri na badala yake watumie kitabu chao, Kur-ani Tukufu. Jee! Hao wanaosema hivyo, wamekwisha isikia Kur-ani Tukufu inavyosema? Kama hawajaisoma wasikilize Kur-ani Tukufu inavyosema. 

Inasema, "Hakika wamekufuru waliosema:Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Mariamu." Al-Maida 5:17. Na pia, inasema, "Kwa hakika wamekufuru waliosema, Mwenyezi Mungu ni wa tatu wa utatu!" -Al Maida 5:73. 

Hivyo ndivyo inavyosema Kur-ani Tukufu. Inawaita wale wanaosema kuwa Yesu ni Mungu kuwa ni makafiri! Na pia, inawaita makafiri wale wanaoamini juu ya utatu wa Mungu! Jee! Wahubiri wa Kiislamu watakapokitumia hicho kitabu chao, Kur-ani Tukufu, wakazisoma aya za aina hiyo pamoja na kuzifasiri hadharani haitakuja kudaiwa kuwa Kur-ani nayo inaukashifu Ukristo, kwa hivyo ipigwe marufuku? 

Inafaa tuelewe kuwa imani za dini hizi mbili ni zenye kupinzana. Mkristo daima ataamini juu ya utatu na juu ya Uungu wa Yesu. Na Mwislamu siku zote ataukataa utatu na uungu wa Yesu! Na kama Mkristo ana haki ya kuitangaza imani yake hiyo hadharani basina Mwislamu anayo haki hiyo hiyo. Sasa jazba za nini? Au huku kutaka kutumia nguvu kuwanyamazisha Waislamu kunatokea wapi? 

Mbona vyama vya siasa vinatofautiana kwa sera, vinapinzana na kushutumiana, na haviambiwi vinyamaze? Kama vyama vya siasa huvutia wafuasi kwa kutangaza sera zao basi na dini ili kuvutia wafuasi inabidi wayatangaze mafundisho yao hadharani. Dini yenye nguvu za hoja itapata wafuasi na ile yenye udhaifu wa hoja itakimbiwa na waumini wake. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri:
Serikali itoe hatma ya mauaji ya Mwembechai 

Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa 

Kanisa liliishinikiza serikali-Waislamu

Sakata ya mabadiliko ya Katiba Zanzibar 

Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu 

HABARI ZA KIMATAIFA 

Ushauri Nasaha  
Kuongoza tabia za watoto 

MAKALA 
Uhuru wa pili na ukombozi wa mwananchi 

MAKALA 
Umuhimu wa uchumi katika Uislam 

Kalamu ya Mwandishi 
Kwa nini kadhia ya Mwembe Chai isifanyiwe uchunguzi? 

Makala 
UPINZANI  OCTOBA 2000 - 3 

MAKALA
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA  JAMHURI YA MUUNGANO: Wananchi Tanzania amkeni 

Riwaya 
Ndoto ya mafanikio 

LISHE 
Vyakula vitupatiavyo mafuta 

Barua/Maoni

MASHAIRI

MICHEZO

  • Tauzany afurahia ligi ya makundi 
  • Kibadeni hakutokomea na fedha za usajili- Milambo 
  • FAT yamuangukia Gama

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita