NASAHA
Na. 035 Jumatano Februari 16 - 22, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Ushauri Nasaha 

Kuongoza tabia za watoto

NA KHADIJA IDD

WATOTO wadogo wanahitaji watu wazima ili waweze kuwaongoza na kuwasaidia ili wajifunze tabia na maadili yanayokubalika na yale yasiyokubalika. Wanahitaji pia watu wa kuwasaidia ili wajifunze namna ya kushirikiana na wengine. Jinsi tunavyotoa muongozo wa namna hii inategemea malengo yetu kwa watoto tunaowafundisha, tunataka watoto hawa wawe watu wa aina gani? Je wawe na nidhamu ya woga au wawe na nidhamu kutegemeana na yale yaliyokubalika na yasiyokubalika.
 

KATIKA kuwasaidia watoto kujifunza nidhamu, wazazi au walimu wanatakiwa kufikiria juu ya sababu za tabia fulani ya mtoto. Kwa mfano kumuoondoa mtoto anayepiga mpira na kuumiza wenzake hakutoshi kumrekebisha, bali unatakiwa kufikiria kiini cha mtoto huyo kuwa na tabia ya kupiga wenzake. Kwa kuelewa anachohitaji mtoto huyo, unaweza kutosheleza mahitaji yake kwa kumpa anachohitaji. 

Kwa mfano mtoto aliyetajwa hapo juu yawezekana hataki kucheza mpira na watoto wengine, unapompa fursa ya kuchezea mpira peke yake utakuwa umetosheleza mahitaji yake. 

Hata hivyo hili halitoshi unatakiwa kumsaidia mtoto huyu ili ajifunze namna nzuri ya kuonesha hisia zake. Ajue kwamba kama hapendi kuwa pamoja na mtoto mwingine afanye nini badala ya kumpiga. 

Katika kuongoza tabia ya mtoto ili awe anafanya yale yanayokubalika katika jamii unaweza kufanya yafuatayo:- 

i) Kuandaa mazingira. 

Tabia ya mtoto ya mtoto inategemea sana mazingira aliyonayo. Kutokana na hali ya kukosa uzoefu(experience) juu ya mambo mbalimbali, mtoto analazimika kutenda au kusema yale yanayokwenda sambamba na aliyomo. 

Ili kumpa muongozo wazazi au walimu hawana budi kuandaa mazingira ambayo yatachochea namna ya utendaji mzuri. Mtoto anayenyang'anya vitu walivyoshika watoto wengine anaweza kusaidiwa kwa kujitahidi kupunguza hali ya kushirikiana katika kutumia vitu. 

Kwa mfano kuongeza vitabu au 'toy'. Hata hivyo uangalifu wa hali ya juu unahitajika ili uweze kumsaidia mtoto huyu aweze pia kujifunza tabia ya kuomba kitu alichoshika mwenzake badala ya kumnyang'anya. 

Katika mazingira ambayo vifaa vya kuchezea watoto ni vichache na uwezo wa kuviongeza ni mdogo, watoto wasisitiziwe na wafundishwe namna nzuri ya kuomba na kushirikiana katika kutumia vitu hivyo. Mwalimu au mzazi anaweza kusaidia kwa kuweka zamu. Hivyo mtoto anaweza kujifunza kutumia kitu fulani kwa kupokezana zamu na mwenzake. Iwapo kuna uwezo wa kifedha, ni vizuri kuweka mazingira kwa namna ambayo watoto watakuwa na vifaa vya kucheza navyo mmoja mmoja. 

ii) Kutumia njia zinazofaa kumuongoza kila mtoto mmoja mmoja 

Kila mtoto ana tabia inayotofautiana na ya mtoto mwingine, vilevile kila mtoto anahitaji njia yake tofauti ya kusaidiwa. Mwalimu au mzazi anahitaji kutumia njia zinazomfaa kumuongoza kila mtoto kwa namna yake. Kwa mtoto ambaye anatupia mawe wenzake afundishwe njia nzuri ya kurusha mawe au kitu chochote, afundishwe pia kuwa akipiga mawe wenzake atawaumiza. Mzazi anaweza kutafuta mfano wa jinsi mtoto mwenyewe alivyoumia na amuulize alijisikiaje. Kwa kutumia mfano anaweza kumsaidia aache tabia ya kupiga wenzake. 

Kwa mtoto ambaye ananyang'anya vitu, mfundishe kuomba na mweleze kwamba kuomba ni jambo la kawaida hivyo asijisikie vibaya kwani kila mmoja anafanya hivyo. Mwalimu au mzazi anaweza kumsaidia kwa kumuomba kitu fulani yeye mwenyewe. Vile vile kumuuliza kuwa iwapo mtu mwingine atamnyang'anya kitu chochote atajisikiaje. Mueleze mtoto kuwa anavyokasirika ndivyo pia mtu mwingine atakavyochukia kunyang'anywa. 

iii) Kuwasaidia watoto kuelewa na kuonesha hisia zao katika njia zinazofaa. 

Wanapokuwa na hisia fulani kwa chuki, hasira n.k. watoto wanaweza kuonesha hisia zao kwa namna mbalimbali mfano kupiga, kulia,kurusha vitu n.k. Hii haina maana kwamba watoto hawa wanatabia mbaya bali hawajaelewa namna nzuri ya kuonesha hisia zao. Hivyo basi ni jukumu la mwalimu au mzazi kumsaidia mtoto ili aweze kuelewa namna atavyoonesha hisia zake. Kwa mfano kama mtoto mmoja hataki kucheza na mwingine na anataka kumpiga, mweleze amwambie kuwa sasa hivi sitaki kucheza na wewe na katu asimpige. Na kwa yule mtoto ambaye anataka apewe maji ya matunda (juice) anapocheleweshewa anaamua kuvunja glass, Mzazi anatakiwa amueleweshe kuwa si kila anapotaka kitu fulani atapata hapo hapo, amfundishe kuwa mwenye subira. Mzazi anaweza kumuelewesha pia kwamba anapovunja glass atakosa sehemu ya kuwekewa juice anayodai. 

Kumuongoza mtoto kunahitaji muda na uvumilivu, ni jambo muhimu sana iwapo mzazi anatumia muda fulani katika kuchunguza tabia na mwenendo na kujitahidi kurekebisha kwa upole. Hasira na ukali havisaidii; kama maji yazimavyo moto, upole hurekebisha tabia ya mtoto haraka sana. Tukumbuke pia watoto ni wanafunzi siku zote, wanahitaji uzoefu kutoka kwetu. Ni juu yetu basi kuwapa kilicho bora na muhimu katika uanafunzi wao. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri:
Serikali itoe hatma ya mauaji ya Mwembechai 

Wanafunzi wa Kiislamu shule za sekondari za serikali Dar wanyanyaswa 

Kanisa liliishinikiza serikali-Waislamu

Sakata ya mabadiliko ya Katiba Zanzibar 

Kukiri kosa na kuomba radhi ndio kipimo cha utu 

HABARI ZA KIMATAIFA 

Ushauri Nasaha  
Kuongoza tabia za watoto 

MAKALA 
Uhuru wa pili na ukombozi wa mwananchi 

MAKALA 
Umuhimu wa uchumi katika Uislam 

Kalamu ya Mwandishi 
Kwa nini kadhia ya Mwembe Chai isifanyiwe uchunguzi? 

Makala 
UPINZANI  OCTOBA 2000 - 3 

MAKALA
MAREKEBISHO YA 13 YA KATIBA YA  JAMHURI YA MUUNGANO: Wananchi Tanzania amkeni 

Riwaya 
Ndoto ya mafanikio 

LISHE 
Vyakula vitupatiavyo mafuta 

Barua/Maoni

MASHAIRI

MICHEZO

  • Tauzany afurahia ligi ya makundi 
  • Kibadeni hakutokomea na fedha za usajili- Milambo 
  • FAT yamuangukia Gama

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com


    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita