NASAHA
Na. 082 Jumatano Januari 10 - 16, 2001
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Wananchi wamwambia Mkapa:
Mbumbumbu wa demokrasia waliomo katika chama tawala ni hatari zaidi
 • Wadai pia demokrasia mbumbumbu 


Na Mwandishi Wetu
 

IMEELEZWA kuwa makuzi hafifu ya demokrasia nchini ya mechangiwa na kuwepo ndani ya chama tawala kwa wananchi ambao ni mbumbumbu wa demokrasia kwa vile bado wanaamini mfumo wa chama kimoja.

Aidha imefafanuliwa kwamba umbumbumbu huo umewagubika hata baadhi ya watendaji katika chama hicho ambao pia hukutana na wananchi kama watendaji serikalini. 

Hayo yameelezwa na wananchi waliozungumza na gazeti hili kufuatia kauli ya Rais Benjamin Mkapa aliyedai kwamba wapo mbumbumbu wa demokrasia. 

Wakiyafafanua maelezo yao hayo, wananchi hao wamesema, kwa mfano, Mwenyekiti wa chama tawala anapotumia kofia yake ya Urais kushinikiza nguvu za dola kuzuia mikutano ya vyama vingine (pinzani) vya siasa husaidia kuwapotosha zaidi wale mbumbumbu wa demokrasia wanaodhani kuwa bado tupo kwenye mfumo wa chama kimoja. 

Wamesema pia kwamba kuwepo kwa "demokrasia mbumbumbu" kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na wale wanaodhani kuwa kununua kura, kuwahonga wapiga kura, kuiba kura, kutumia vitisho na hata nguvu za dola kupora kura na kukandamiza upinzani ni sehemu ya demokrasia. 

Pia wameeleza kwamba wapo miongoni mwa mambumbumbu hao wa demokrasia walijiumbua wakati wa kampeni pale walipopanda kwenye majukwaa "wasijue cha kuzungumza ila kuanza kutumia maneno machafu dhidi ya wake za baadhi ya wagombea ambao hotuba zao zilijaa hoja nzito ambazo mambumbu walishindwa kuzijibu." 

"Mambumbumbu wengi pia wamo ndani ya chama tawala. Hawa demokrasia yao ni 'demokrasia mbumbumbu' pia. Kwao mwananchi akijiunga na chama cha upinzani hustahili hata kunyimwa haki zake za msingi za kibinadamu na zile za kiraia. Baadhi ( ya mambumbumbu hao) hudhani kuwa ni halali hata kutumia nguvu za dola kumbughudhi na hata kumtesa mtu na familia yake kwa kumnyima ajira na njia yoyote ya kujitafutia riziki kuwa japo kwa biashara ya genge la nyanya. Ndio maana imekuwa kawaida ya wengi kuwaalika baadhi ya viongozi wa chama tawala kuwasimikia 'vijiwe' na bendera za mashina ili wapate uhalali wa kufungua magenge ya kujipatia riziki", alieleza Mwalimu Shaaban Hadidu. 

Mwalimu Hadidu aliongeza kwamba baadhi ya mambumbumbu hao huwa hawaoni haya wala vibaya kuwaambia wananchi tundika bendera usalimike. 

Wakizidi kuchambua kina cha umbumbumbu uliopo wananchi hao wamedai wapo pia mambumbumbu waliona sawa tu kutukana dini za baadhi ya wananchi kuwa ni wenye kuhongwa tena ndani ya majumba yao ya Ibada , na wengine wakadiriki hata kuwakodi watu waliojiita "masheikh" ili wapande majukwaa kukashifa dini za watu wanaoonekana kutokipenda chama cha mambumbumbu hao. 

Wananchi hai pia walielezea kuwepo kwa umbumbumbu demokrasia upande wa upinzani pia. Wamesema mambumbumbu katika upande huo hudhani demokrasia maana yake kujipendekeza chama tawala ili "wasalimike," na Msajili wa Vyama asije akataka kuhakiki vyama vyao kama bado vina wanachama, vinafanya mkutano wake kwa mujibu wa katiba na vinafanya uchaguzi wa kidemokrasia wa viongozi wake tangu viundwe miaka 8 iliyopita. "Miongoni mwao hawa wapo pia viongozi wa vyama ambao hawaishi kujipendekeza kwao huko, hufikia hata baadhi yao kutumiwa kama mapandikizi dhidi ya kambi ya upinzani, wanahribu vyama vyetu na sasa wanatufanya wote tuonekane hatuna maana" alilalamika Bw. Furaha Msonga. 

Aidha, wananchi hao wamesema lipo pia swala la umoja wa kitaifa ambapo wametahadharisha .vyama vingi visiwe sababu ya kuvunja utaifa. 

Hata hivyo wameongeza kutoa tahadhari kwamba watanzania waasitegemee kujenga utaifa huo huku baadhi ya viongozi kwenye chama tawala hawaishi kuwakashifu na kuwakejeli baadhi ya viongozi na wananchama wa vyama vya upinzani. 

Wakitolea mfano wa jinsi viongozi wa chama tawla wanavyoweza kufanya kazi na wale wa upinzani kwa msalahi ya taifa, wananchi hao wamemtaja Mzee Nelson Mandela wa Afrika ya Kusini ambapo wamesema watu wa chama tawala wangejifunza toka Afrika Kusini au hata Marekani. 

"Mandela alikuwa akifanyakazi na viongozi wa upinzani, na (George) Bush (wa Marekani) pia kaonesha hilo", alieleza mwanchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Mgana.­. 


Waislamu watakiwa kuwa watekelezaji wa maamuzi 

 • Watakiwa kwatambua wale wanaokwamisha utekelezaji ambao ni vibaraka, waoga na wazembe 


Na Mwandishi Wetu

WAISLAMU nchini wametakiwa kuyatekeleza yale yaliyoamuliwa na Mwenyezi Mungu (S.W.) na yakafundishwa kwao na Mtume wake (S.A.W.) kama moja ya ahadi juu yao.

Aidha wametakiwa vilevile kutekeleza na yale ambayo wao huyaamua kwa misingi ya dini yao na kisha wakaaomba dua kwa Mweneyzi Mungu (S.W.) awawafikishie. 

Akitoa wito huo, Mhadhiri wa kiislamu jijini Dar es Salaam, Ustaadh Kondo Bungo amewaambia Waislamu kwamba maamrisho ya Mwenyezi Mungu (S.W.), mafundisho ya Mtume (S.A.W) na maamuzi wanayoyachukua Waislamu hao na kisha wakayaombea dua kwa Mwenyezi Mungu (S.W) awawafikishie yote hayo ni miongoni mwa ahadi mbele ya Mwenyezi Mungu (S.W.) ambazo wanayo dhima ya kuzitekeleza. 

Ustaadhi Bungo alikuwa akiongea na Waislamu katika Msikiti wa Taqwa, uliopo Mwananyamala, Dar es Salaam, baada ya Swala ya I'sha, Jumapili, Januari 7 mwaka huu. 

Akiufafanua msimamo wake huo juu ya suala hilo, Ustaadh Bungo alisema licha ya Waislamu wengi kuwa wanalijua jambo hilo bado kuna tatizo la utekelezaji wa ahadi hizo wanazozichukua na kisha aliwauliza Waislamu: "...nini kiini cha tatizo hili?". 

Akifafanua kuhusu kiini cha tatizo hilo la kutotekelezwa ahadi hizo, Ustaadh Bungo alisema kwamba ahadi nyingi zinakwamishwa na watu wa aina tatu miongoni mwa umma wa Waislamu ambao aliwataja kuwa ni vibaraka, waoga na wazembe. 

Akiwazungumzia vibaraka alisema: "mtu kibaraka ni (yule) ambaye mko naye msikitini na anapiga takbira kwa wingi lakini kesho utamkuta anajipendekeza kwa kiongozi anayewatukana Waislamu... na yeye ndio wa kwanza kupanga mstari kutoa mkono kwa kiongozi huyo (kama dalili ya salamu ya heshima)" 

Ustaadhi Bungo aliendeleza uchambuzi wake ambapo alisema ikitokea Muislamu huyo kibaraka kuwa ni Imam au kiongozi wa Taasasi ya Kiislamu, basi yeye ndio huwa wa kwanza anapokuwa na hafla kuwaalika viongozi wenye kauli chafu dhidi ya Waislamu kuwa wageni rasmi. 

Alilitaja kundi la pili kuwa ni Waislamu waoga ambao alisema hao nao ni tatizo. Alisema Waislamu walio katika kundi hilo, kutokana na woga wao, husahau kumhofu Mwenyezi Mungu (S.W.) na badala yake wakawahofu wanandamu wenzo kutokana na madaraka walionayo na vitisho vyao. 

Ustaadhi Bungo aliwatamnabaisha Waislamu kwamba ikitokea mtu huyo mwoga kuwa Imam, sheikh au amir, basi anapotoa hotuba zake huwa anayumbayumba katika mada. 

"Siku zote huwa hawasemi kweli watu hawa na wala hawafundishi yanayostahiki kuwa haki... kwa mfano badala ya kufundisha kuindoa dhuluma wao hufundisha kuikwepa", alieleza Ustaadh Bungo. 

Akifafanua hoja yake hiyo alisema ikitokea 'grosari' imejengwa mbele ya msikiti, basi imamu au sheikh huyo mwoga hubadili njia badala ya kuwataka waumini "wakaiondoe grosari hiyo", na kisha akauliza: "je katika njia hiyo nyingine pakijengwa baa imam huyo na waumini watapita wapi?" 

Akilitaja kundi la tatu Ustaadh Bungo alisema watu wake ni wazembe na akadai kwamba hao ni hatari zaidi. 

Alisema wakati wale waoga hutoa visingizio vya "eti wanatumia hekima", waumini wazembe hudai "eti wanasubiri amiri wao aseme!" 

Ustaadh Bungo ameeleza kuwa katika Uislamu, suala la kupambana na maovu kwa misingi ya dini hiyo ni amri, na kwamba amri yoyote ni ibada. 

Akitolea mfano alisema: "Kuswali ni ibada na pindi wakti (wakati) unapotimu waumini huinuka wakaswali pasi na kumsubiri amir", na kisha akahoji, "sasa iweje suala la kuondoa maovu wasubiri kauli ya amir?" 

Amesema, muda wa swala ukifika, waumini, wakiwemo wazembe hao, huinuka kwenda kuswali na wala hawasikiki wakitoa visingizio vyao vya kumsubiri amir, na aashangaa iweje katikia ibada zingine waumini wadai kumsubiri amir. 

Ustaadh Bungo aliwataka waumini kuwatambua watu hao watatu wanaokwamisha utekelezaji wa ahadi wanazozichukua Waislamu ili wapate kuwaelimisha na pale inaposhindikana kuelimishwa basi wawaepuke kwa vile alisema watu hao ni kikwazo katika maendeleo ya jamii ya Waislamu. 

Aizungumzia umuhimu wa kuwaelimisha, ustaadh huyo aliwakumbusha waumini msiktini hapo kisa cha Nabii Musa (A.S) aliyekimbilia Madiyan baada ya kukabiliwa na tuhuma ya kupiga mtu hadi kufa katika utawala wa Firauni. 

Lakini wakati Musa akiwa Madiyan, Ustaadh Bungo alisema Mwenyezi Mungu alimwambia Musa (A.S) aende kwa Furauni "akamlinganie" aache kiburi chake cha kujidai yeye Mungu, kufanya dhuluma, mauaji ya raia na ukandamizaji uliokithiri. 

Alisema, Musa (A.S), ambaye awali aliukimbia utawala wa Firauni kwa hofu ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili, alilazimika kuishinda nafsi yake iliyokuwa ikimuhofu Firauni ambaye alikuwa ni kiumbe na mwanadamu kama yeye Musa (A.S). 

"Musa (A.S) akaacha mara moja kumhofu Firauni na badala yake akazidisha kumhofu Allah (S.W) (hivyo) akaamua kwenda kumkabili Firauni licha ya maguvu yake ya dola na wapambe wake wachawi na washirikina", alifafanua Ustaadh Bungo. 

Alisema Musa (A.S) aifanikiwa kumshinda Firauni na kuwakomboa wananchi waliokuwa wakiteseka chini ya utawala huo wa kidhalimu wa Firauni. 

Aidha , kuhusu kundi la waislamu wazembe, Ustaadh Bungo aliwakumbusha Waislamu mazingira ya enzi ya Mtume (S.A.W) ambapo alisema katika vita zote zilizopiganwa wakati huo na ambazo zilijulikana kama "Ghazua", waumini baada ya kujua kuwa walikuwa wakipigana kwa amri ya Mola wao na haki ya dini yao, hawakuwa wakizembea kwa kujenga visingizio vya kusubiri amri ya Mtume (S.A.W), bali kila walipoona dhuluma, vita au shari ikielekezwa kwao walipamabna nayo. 

"Ama kwa wale vibaraka", alisema Ustaadh Bungo, "hawa ni wa kupigwa vita sambamba na madhalimu wanaowaweka mbele na kuwapa majukwaa ya kuwatusi Waislamu". 


'Hajj Trust' yaongeza huduma kwa mahujaji 
 • Usafiri wa Jeddah-Madina sasa kwa ndege 


Na Mwandishi Wetu
 

Mahujaji wa Tanzania watakaokwenda Hija kuanzia mwaka huu watapatiwa usafiri wa ndege kutoka Jeddah kwenda Madina ili kukwepa uchovu wa safari ndefu ya masaa nane kati ya miji hiyo miwili ambao wangeupata endapo wangetumia usafiri wa basi.

Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kiislamu inayoshughulikia masuala ya Hija hapa nchini, Tanzania Muslim Hajj Trust, Abdallah M.Jabir, alipokuwa akizungumza na NASAHA kuhusu maandalizi ya Hija ya mwaka huu. 

Jabiri amesema kuwa nyongeza hiyo ya huduma ya usafiri wa ndege kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Saudi Arabia, Saudi Airlines, haitaathiri huduma nyingine zitolewazo na taasisi yake wala ongezeko la gharama kutoka kwa Mahujaji. Gharama za Hija kwa mwaka huu kama ilivyotangazwa na taasisi yake ni dola za Kimarekani 1600, ikiwa ni ongezeko la dola 100 zaidi kutokana na kupanda kwa gharama za huduma za ndani za serikali nchini Saudi Arabia. 

Alizitaja huduma nyingine kwa uchache wazitoazo kwa Mahujaji kuwa ni pamoja na chakula kwa siku zote wawapo katika miji ya Maka, Madina na Mina na huduma ya matabibu wa kiume na wa kike wakati wa Hija. Huduma nyingine ni za waongozaji Mahujaji katika miji hiyo mitatu na ziara za maeneo matakatifu ya kihistoria zilizopo Madina. 

Aidha alisema matayarisho ya Ibada ya Hija ya mwaka huu yalishaanza toka miezi sita iliyopita ambapo mpaka sasa Waislamu zaidi ya 200 tayari wamejiorodhesha, lengo likiwa ni kusafirisha Mahujaji kati ya 350 na 400. 

Akijibu swali la mwandishi kwanini wasitumie ndege za Shirika la Ndege la Yemen ambazo inasamekana bei zake ni nafuu sana, Jabir alisema Hajj Trust hutumia ndege za kukodi za shirika la ndege Tanzania (ATC) ambazo pamoja na kuwa huenda moja kwa moja Jeddah, lakini pia wanajihisi ufahari kama wazalendo kushuka katika uwanja wa ndege wa kigeni wakiwa na ndege yenye alama ya Taifa wanalotoka. 

"Sisi ni wazalendo wa Taifa hili, tunasikia ufahari pesa za Watanzania zinapobaki katika mikono ya Watanzania wenyewe badala ya kuzipeleka kwa watu wa nje... Lakini pia ni ufahani kushuka Jeddah tukiwa kwenye ndege yenye nembo ya Taifa letu", alisema Katibu Mkuu hayo wa Hajj Trust. 

Hata hivyo, alidai kuwa tofauti kati ya nauli inayotozwa na ndege ya shirika hilo la Yemen na ile inayotozwa katika ndege za ATC ni dola 15 tu, huku safari za ATC zikiwa ni za moja kwa moja na hivyo kupunguza usumbufu kwa Mahujaji kwa kupanda na kushuka wabadilishapo ndege wakiwa njiani. 

"Safari hizi za ndege ya Yemen sio kitu kipya, zimeanza toka toka Novemba 1999. Hata sisi huko nyuma tuliwahi kutumia ndege zao kusafirishia waumini waliokwenda (kufanya Ibada ya) Umra," alisema Jabir. 

Ratiba ya safari za Hija kama ilivyooneshwa kwa mwandishi ni kuwa ndege zitaondoka Dar es Salaam kwenda Jeddah Februari 17, 18, 19 na 23, na zile za kurudi zitaanzia Machi 11, mwaka huu. 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

MAONI YETU
Mapinduzi Zanzibar yameleta kilichokusudiwa?

Wananchi wamwambia Mkapa:
Mbumbumbu wa demokrasia waliomo katika chama tawala ni hatari zaidi

Waislamu watakiwa kuwa watekelezaji wa maamuzi

‘Hajj Trust’ yaongeza huduma kwa mahujaji

DONDOO MUHIMU

MAKALA
Jamii ijihadhari viongozi wasaliti

MAKALA
Msimamo wa Pengo haushangazi

KALAMU YA MWANDISHI
Kitendawili cha millenia: Urais bila dola

MAKALA
Dhana ya kumwabudu Mungu anayeafiki udhalimu lazima tuikatae

MAKALA
Mapinduzi Zanzibar: Dhuluma bado ipo

MAKALA
CCM haiwezi kuondosha umasikini Tanzania

MAKALA
Tirivyogo la sekta ya elimu

Mwenye Macho……
Demokrasia haiwezi kujengwa kwa kuvunja katiba

HABARI ZA KIMATAIFA

MASHAIRI

MICHEZO

 • Baadaya Mkapa kushindwa kusaidia: Prof. Lipumba aombwa kuiombea Tanzania FIFA
 • Mtwa aanza kulala mapema
 • Salvatory aitwa Mtibwa

 •    Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
  Au
  Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

  Ukurasa wa mwanzo
  Islam Tanzania
  Matoleo yaliyopita