Majibu ya Rais kwa Waislamu


The President of the United Republic ofTanzania
The State House
Dar es Salaam

17 Desember, 1999
 

Ndugu Saleh Al-Miskry,
Halmashauri Kuu ya Waislamu,
C/o Islamic Club,
S.L.P. 11392,
DAR ES SALAAM.
 

Ndugu Al-Miskry,

NINAKIRI kupokea, kwa shukrani, barua yako ya tarehe 26 Agosti, 1999, pamoja na viambatanisho vyake. Imenichukua muda mrefu kukujibu kwa sababu mambo uliyoandika ni mazito, ya kitaifa na inabidi niyatafakari kwa kina, niyafanyie utafiti zaidi, na nishauriane na wenzangu serikalini kabla ya kuyajibu.

Leo ninakuandikia si kwa lengo la kujibu hoja moja baada ya nyingine, au kutoa jibu kwa kila swali. Katiba ya Jamhuri yetu inanipa mimi, kama Rais, wasaidizi wengi. Ninaye Makamu wa Rais, na ninaye Waziri Mkuu. Ninaye waziri wa kila sekta, na ninao wakuu wa mikoa na wilaya kwa kila eneo la nchi yetu. Nitakuwa siwatendei haki nikijibu maswali yanayowahusu wao. Ningeshauri, kama mlivyojenga mahusiano mazuri nami, mjenge pia mahusiano mazuri na mawaziri, wakuu wa mikoa, na kadhalika, ili kila jambo lisingoje mpaka lifikishwe kwa Rais.

Nina uhakika, kwa mfano, kwamba Waziri wa Elimu ana uwezo na madaraka ya kutosha kushughulikia masuala ya elimu, ambayo kwangu ni muhimu sana. Akikwama atayaleta kwangu. Hiyo itasaidia kufanya mawasiliano nami yawe yale yanayohusu mambo ya msingi, badala ya kujadili matukio. Misingi hiyo itasaidia kuwaongoza watendaji wa serikali, na kuniwezesha mimi na nyinyi kuwa na vigezo vya kupima tunafanikiwa kiasi gani katika kuhakikisha kila mwananchi anapata haki zake za msingi bila ubaguzi wowote kwa sababu za dini, dhehebu, kabila, jinsia, eneo analotoka, na kadhalika.

Msingi wa kwanza ni utawala wa sheria. Nchi yetu lazima iendelee kutawaliwa kwa msingi wa sheria zilizowekwa kwa njia za demokrasia. Hivyo napata taabu kidogo raia wa nchi hii anapofikiri matatizo aliyo nayo yanaweza kutatuliwa nje ya mfumo wa utawala wa sheria. Kila mwenye kero akichukua msimamo huo, nchi hii itakuwa haitawaliki tena, itakuwa vurugu tupu. Kazi ya msingi ya serikali yoyote ni kuhakikisha unakuwepo utawala wa sheria, ulinzi na usalama wa raia wote, wa aina na imani zote. Uhalali wa raia kudai haki nje ya mfumo wa utawala wa sheria unaweza ukakubalika penye utawala wa kikoloni, utawala wa ubaguzi wa rangi, au utawala wa kidikteta. Uhalali huo haupo hata kidogo katika nchi huru, inayoongozwa kwa misingi ya demokrasia kama ilivyo Tanzania.

Kwa sababu hiyo nimefadhaishwa sana na kauli za kuashiria shari za wale wanaojiita "Shura ya Maimamu Dar es Salaam". Pamoja na mambo mengine ya uchochezi wanasema, "Waislamu hatuna moyo tena na serikali ya nchi hii na vyombo vyake vyote likiwemo Bunge na Mahakama". Ninajua huu sio msimamo wa Waislamu walio wengi, lakini matamko yasiyokuwa na kiasi kama haya yasipokanushwa, na wanaoyatoa wanapopewa fursa na majukwaa ya kuyasema, hiyo inawapa silaha wale wachache wanaojaribu kupaka matope heshima na picha nzuri ya Waislamu. Mimi na ninyi tuna kazi ya kuwasahihisha wenye hulka ya aina hiyo, lakini matamko kama haya yatafanya kazi hiyo iwe ngumu zaidi.

Utawala wa sheria chimbuko lake ni Katiba ya Jamhuri. Katiba yetu imepiga marufuku ubaguzi wowote, kwa msingi wowote, ikiwemo dini, kabila, rangi, eneo analotoka mtu, na kadhalika. Katiba hiyo pia imetoa uhuru kamili, ndani ya uwigo wa sheria, wa imani za dini kustawi katika uhuru wa ibada. Isipokuwa kwa wale ambao hawana imani na vyombo vyote vya dola, mimi nina imani kuwa mahakama zetu zina uwezo na uhuru kamili wa kumpa haki hizi za msingi yule ambaye atakuwa amenyimwa kwa ubaguzi.

Narudia. Haki za msingi za kila raia zimo ndani ya sheria Mama - Katiba - ya Jamhuri yetu. Kama kweli upo ushahidi kwamba baadhi ya taasisi za umma, au viongozi wa umma, wamebuni mfumo wao wa kuhakikisha Waislamu wananyimwa haki zao, hao wala si wa kuchukuliwa hatua za nidhamu tu, bali ni wa kushitakiwa mahakamani. Wasionewe haya. Tusaidianeni washitakiwe!

Siwezi kushangaaa iwapo kuna mtu au kiongozi mahali ambaye ndani ya moyo wake ana chuki dhidi ya Wakristo au dhidi ya Waislamu, au ana chuki dhidi ya wanaume au wanawake, au ana chuki dhidi ya Wazaramo au Wahaya, au chuki dhidi ya watu warefu au wafupi. Ninachosema ni kuwa katika utafiti niliofanya hakuna mahali popote katika serikali hii ambapo upo mfumo rasmi wa kubagua au kumnyima haki za msingi mtu yeyote kwa msingi wowote.

Kweli, zipo tofauti kati ya idadi ya Waislamu na wasio Waislamu katika shule, vyuo, sehemu mbalimbali za kazi lakini huo si ushahidi wa mfumo wa ubaguzi. Sababu zake sote tunazijua - ni za kihistoria na za kijamii, kama ilivyo kwa tofauti kati ya idadi za watu wa kabila mbalimbali, au jinsia. Ingekuwa tofauti hizo peke yake zinatosha kuthibitisha mfumo rasmi wa ubaguzi wa Waislamu, kwanini tusiseme pia kuwa upo mfumo rasmi wa kubagua wanawake, au watu wa kabila fulani, au rangi fulani, au umbo fulani. Na ukweli ni kuwa si kila mahali Waislamu ni wachache. Kwa mfano nimejaribu kuhesabu ni mabalozi wangapi, tena kwenye zile ofisi za ubalozi muhimu sana, ambao ni Waislamu. Naomba na ninyi mfanye hesabu hiyo.

Lakini turudi kwenye masuala ya msingi. Si jambo zuri sana kuanza kujenga utamaduni wa kuhesabu watu kwa misingi ya kabila zao, dini zao, rangi zao, jinsia zao, au maeneo yanayotoka. Tangu uhuru tumejitahidi kujenga taifa ambapo haki na heshima ya mtu inatokana na utu wake, si dini yake, kabila lake, jinsia yake, na kadhalika. Siko tayari kujenga mfumo wa utawala ambapo sifa ya mtu kupata nafasi ya shule, au nafasi ya kazi, ni dini yake. Aidha, tukishaanza na dini tutawazuiaje wengine kudai nao wafikiriwe kwa misingi ya dhehebu la dini, jinsia na kadhalika. Hapo tutakuwa tumefumua misingi ya umoja, upendo, mshikamano na kuheshimiana waliyotuachia waasisi wa Taifa letu. Naomba sana tusitafute dawa ya ugonjwa mdogo itakayozua magonjwa makubwa zaidi yasiyokuwa na tiba.

Vile vile kuanzisha taasisi mpya ya kupokea na kuchunguza ubaguzi wa kidini kutazidi kutuvuruga tu kwa vile ni kukiri kuwa kweli upo ubaguzi uliojengeka ndani ya mfumo wa utendaji serikalini, jambo ambalo si kweli. Aidha, kama nilivyosema, ukianzisha taasisi ya kushughulikia ubaguzi wa kidini, huwezi kukataa wengine wakidai taasisi nyingine ya kushughulikia ubaguzi wa jinsia, ubaguzi wa kabila, rangi na kadhalika.

Tusijitose sana katika zoezi la kuhesabu watu kwa misingi ya dini. Tukifanya hivyo tutaimarisha, badala ya kufifisha, hali ya watu kujihisi kwanza kama watu wa dini fulani, badala ya kujihisi kwanza kama Watanzania. Mimi nilifikiri kuwa Tanzania ilishavuka hatua hiyo. Naomba tusirudi nyuma kwenye kutukuza udini, ukabila, au maeneo tunayotoka. Tukishajitumbukiza huko hatuwezi kutoka tena. Badala yake lengo letu liwe kuelekea mahali ambapo tutakuwa vipofu wa dini, vipofu wa rangi, vipofu wa kabila, na kadhalika. Na pia tusisahau kuwa Tanzania yetu hii ina hata Maaskofu wenye majina ya Ramadhani au Hussein, na wengine wengi ambao wana majina yasiyofichua dini zao au kabila lao.

Jambo jingine la msingi ni kuhakikisha kuwa Tanzania kama Taifa, na kama serikali au chama chochote cha siasa, inakuwa haina dini. Kwenye hili hakuna mjadala, maana ni hali hiyo ya kutoinamia upande wa dini yoyote ndiyo inayotupa nguvu ya kusimamia na kuhakikisha kila raia anapata haki zake za imani za dini na uhuru wa ibada bila hofu au wasiwasi.

Kwa hili serikali ni refa anayehakikisha kila upande una haki sawa, na uhuru sawa, na kuwa uhuru wa kuabudu au kutangaza dini kwa upande mmoja hauathiri haki ya uhuru wa ibada na kutangaza dini kwa upande wa pili.

Mimi ni Rais wa watu wa dini zote, na ni Rais pia wa wale wasiokuwa na dini, ni Rais wa kabila zote na rangi zote, jinsia zote na hulka zote.

Mimi ni Rais wa wanywa pombe na wasio wanywa pombe; wala nguruwe na wasiokula nguruwe. Si kazi yangu kuhukumu nani kati yao ni mwema na nani si mwema. Kunitaka nimkataze mmoja anachopenda ni kunitaka nifanye kazi ya kuhukumu juu ya imani za watu ambayo si yangu; hiyo mimi naamini ni kazi ya Mwenyezi Mungu mwenyewe.

Hiyo pia ndiyo inayonifanya nichelee kukubali haraka haraka hoja ya Tanzania kujiunga na Shirika la Waislamu (OIC). Nadhani si sahihi kuishinikiza serikali ikubali hoja hiyo kwa vile tu zipo nchi nyingine zilizojiunga. Kila nchi huangalia mazingira yake na sababu zake. Kwa vile ukijiunga unafanya hivyo kama Taifa zima, si kama sehemu ya Taifa, siwezi kupuuza kabisa maoni ya wale ambao si Waislamu. Hivyo huu si uamuzi ambao ninaweza kuufanya kwa wepesi; unahitaji mashauriano zaidi na pande zote na kuelimishana ili jamii yote ya Tanzania ielewane.

Kuhusu suala la Mwembechai mimi nilifikiri tulishaelewana kuwa haitasaidia sana kuunda Tume ya Uchunguzi, maana tunajua kilichotokea. Na tunajua kuwa zile fujo, ambazo hatimaye zilihitaji nguvu kubwa ya dola kuzizima, hazikuwa na uhusiano na mambo ya dini kabisa. Ndio maana miongoni mwa waliokamatwa walikuwapo watu ambao wala si Waislamu. Bado haja na hoja ya kuunda Tume sijaiona.

Tulipokutana tarehe 7 Julai, mwaka huu, mojawapo ya mambo tuliyozungumzia ilikuwa umuhimu wa kuwa na fursa ya mazungumzo ya kudumu baina ya waumini wa dini mbalimbali, (inter-faith dialogue), ili mradi wahusika wawe watu waliokomaa kimawazo, wenye busara na nia njema. Hii itasaidia kujenga maelewano baina ya waumini wa dini zote na hivyo kupunguza hisia za kibaguzi za kila upande, na kujenga msingi bora zaidi wa kufurahia uhuru wa imani katika mazingira ya kupendana na kuheshimiana, japo tuwe na imani tofauti za dini.

Mlango wangu bado uko wazi kwa majadiliano ya mambo ya msingi kama haya kila nikiwa na nafasi.

Tanzania ni nchi yetu sote, watu wa imani tofauti za dini. Tukiwa na busara, tutawajengea watoto wetu nchi nzuri ya kumcha Mungu kwa uhuru, amani na kuheshimiana kwa kuzingatia kwa dhati maneno haya.

Wasalaam,

Benjamin William Mkapa
RAIS WA JAHAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA