HALMASHAURI KUU YA WAISLAMU.
c/o Islamic Club, P.O Box 11392. Tel.: 185258/0511 613422, Dar
es Salaam.
26/08/1999.
Mhe. Benjamin William Mkapa
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
Ikulu, Dar es Salaam
YAH: MASHAURIANO KUHUSU MADAI YA WAISLAMU.
Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa tunaomba uhusike na kichwa cha maneno;
na urejee mazungumzo yetu ya awali pamoja nawe yaliyofanyika nyumbani kwako,
hapo Ikulu, jioni ya jumatano, tarehe 7 july 1999.
Awali ya yote halmashauri inatoa shukurani za dhati kwako kwa kitualika
kukutana nawe siku hiyo na kutukirimu. Mkutano huo ulitupa matumaini makubwa
juu ya uwezekano wa kipatikana na ufumbuzi wa kudumu wa madai ya waislamu
ambayo tuliyawasilisha rasmi kwako mwazoni mwa mwaka huu, wakati wa baraza
la Eid el Fitri. Madai hayo kwa ufupi yanahusu:
-
Ubaguzi uliojitokeza dhidi ya waislamu katika baadhi ya vyombo vya dola
ambao unafanywa na naadhi ya watendenaji walio katika serikali. Mfano wa
hili umejitokeza katika:
-
Kuwepo kwa idadi ndogo ya waislamu katika vyuo na maofisi ya serikali ukilinganisha
na iwiano halisi ulivyo katika jamii yetu ya watanzania; na
-
Kuwepo kwa idadi kubwa ya waislamu "wazururaji" na "wahalifu"katika magereza;
-
Suala la Mwembechai kupatiwa utatuzi;
-
Suala la Mahkama za Makadhi na
-
Suala la nchi yetu kujiunga na "organization of Islamic conference" (OIC)
na kiboresha uhusiano wake na nchi za Kiislamu.
Tulipokutana siku hiyo, kama tulikuelewa vjema, ulitueleza kwamba:
-
Serikali inatambua kuwepo "imbalances" dhidi ya waislamu katika jamii yetu
ya Watanzania;
-
Sio lengo wala njama za serikali au hata sera za Chama cha Mapinduzi (CCM)
kuwa na hizo "imbalances"
-
"Imbalances" hizo zipo tu kwa sababu ya kihistoria na ubinafsi ya baadhi
ya watu katika CCM na Serikali; na
-
Serikali bado inajukumu na wajibu wa kuondoa hizo "imbalances" kama inavofanya
na maeneo mengine.
Kauli hii ilitupa faraja na imani kwamba viongozi wa CCM na Serikali sio
tu hawapaswi kufuata sera hiyo potofu za kibaguzi dhidu ya Waislamu, bali
pia wako pamoja nao katika kutetea usawa. Tunashukuru pia kwamba siku hiyo
ulitudokezea kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua za kurekebisha hali hiyo
na kuondoa kabisa kasoro hizo. Miongoni mwa hatua ulizozitaja ni:
-
Maelekezo uliyokwisha kuyatoa juu ya kutatuliwa kwa matatizo ya Waislamu
yanayohusu "hijabu" na kuwepo kwa mabaa (bars), nyumba za wageni (gest
houses), ufugaji ovyo na uchuuzi wa nguruwe na mabucha yake.
-
Ofisi yako ina "update human resources bank" yake, ikiwa ni pamoja na kutafuta
waislamu wenye taaluma za kushika nyadhifa mbali mbali; na
-
Katika masuala ya utoaji wa vyeo, serikali imeanza suala la kuzingatia
uwiano baina ya waumini wa dini tafauti.
Pamoja na maelezo hayo ulitoa tahadhari kwamba:
-
Utatuzi kamili wa matatuzi ya Waislamu utachukuwa muda;
-
Masuala ya OIC na Mahkama za Makadhi bado yanahitaji utafiti, matayarisho
na kuelimishana; kwa vile baadhi ya watu bado wanadhana au khofu kuwa kukubali
masuala haya ni sawa na kukubali kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Kiislamu;
na
-
Kuwapa Waislamu nafasi zote wanazostahiki kunataka busara na hekima kubwa
kwa vile inabidi kwanza baadhi ya nafasi hizo wanyimwe au wanyanganywe
watu wengine.
Mwisho ulishauri kuwa:
-
Badala ya Waislamu kudai kwenye majukwaa, ni vyema madai hayo kuletwa kwako
moja kwa moja kwa vile uko tayari kuyapokea na kuyashughulikia.
Mhe Rais, Halmashauri ilikubaliana nawe kwa hayo yote; na uliongeza kwa
kusema kwamba:
-
Siyo muhimu sana kwa Waislamu hivi sasa kujua nani amesababisha hizo "imbalances",
bali muhimu zaidi ni serikali kutambua kwamba "imbalances" hizo zipo na
inapaswa kuziondoa.
-
Suala la ku "update human resource bank" ya serikali ni suala muhimu sana
kwani inawezekana Waislamu kukosa baadhi ya nafasi kwa sababu ya Serikali
kutojua kama kati yao wamo wenye taaluma za kushika nafasi hizo.
-
Waislamu hawataraji miujiza ya kutatuliwa matatizo yao yote kwa usiku mmoja;
bali wanahitaji kuona kuwa hatuwa thabiti zinachukuliwa za kutatua matatiza
hayo ikiwa ni pamoja na:
-
Kuundwa kwa tume huru za kuchunguza suala la Mwembechai;
-
Kuanzishwa kwa mpango, hata kama ni wa muda mrefu, na ratiba ya kuondoa
hizo "imbalances" na
-
Kukemewa na kukomeshwa kwa propaganda potofu dhidi yao.
Halmashauri, Mhe Rais, ilikudokezea kwamba takriban imeshamaliza kufanya
utafiti wake; na, pamoja na mambo mengine, matokeo ya utafiti huo yanaonyesha
kwamba:
-
Imbalances zipo kwa vile hakuna "mechanism" ya kuzuia kuwepo kwake; na
zipo kwa sababu takwimu zote takriban zinaonesha hivyo.
-
Ilikuwa ni kinyume na Katiba kuondoa Mahkama za Makadhi kwa vile Katiba
ya Tanzania inadhamini uhuru wa kuabudu na Waislamu kuwa na Mahakama hizo
ni sehemu ya ibada.
Kwa kumalizia, Halmashauri yetu ilikuhakikishia kwamba:
-
Haifanyi haya yote kwa sababu ya choyo, uroho au maslahi ya ubinafsi ya
Waislamu peke yao; ila inafanya hayo kwa maslahi ya Taifa zima na kwa nia
safi ya uzalendo na kutaka kuimarisha demokrasi na uadilifu.
Hapa tunapenda kutoa taarifa, Mhe Rais, kwamba siku chache kabla ya kikao
hicho pamoja nawe,
na baada ya kuona muda mrefu umepita tangu Halmashauri yetu kukupatia
Madai ya Waislamu, tulikuwa tumejiandaa kulieleza Baraza la Maulid siku
ya tarehe 10 julai 1999 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, kuwa Serikali
inachelewa kushughulikia Madai hayo. Lakini, kutokana na mazungumzo hayo
ya tarehe 7 julai 1999, Halmashauri kwa furaha ilibidi ibadilishe risala
yake na kutoa tamko rasmi kwamba madai hayo sasa yameanza kushughulikiwa
na Serikali ipasavyo.
Mhe Rais, pamoja na mkutano wetu huo nawe hapo Ikulu, kumetokea mambo
mengine kadhaa ambayo tunapaswa kuyazingatia kwa vile yana uhusiano mkubwa
na masuala yetu.
-
Mosi, kumekuwa na tamko la CCT la kutaka Serikali iache mara moja fikra
ya Tanzania kujiunga na OIC kwa hoja kwamba OIC ni jumuiya ya Kiislamu
na nchi hii ina Waislamu na Wakiristo
-
Tamko hilo ambalo tunatarajia kuwa limetolewa kwa nia nzuri linathibitisha
kauli yako kwamba baadhi ya wananchi wana dhana kuwa Tanzania ikijiunga
na OIC itakuwa nchi ya Kiislamu. Ndio maana Halmashauri inakubadiliana
nawe kuhusu kuelimishana ili kuondoa dhana hii. Ni muhimu wenzetu wajue
kuwa nchi zisizo za Kiislamu ambazo zimejiunga na OIC kama vile Uganda
na Mozambique, zinaendelea kuwa si za Kiislamu. Tangu kujiunga na OIC bado
hatujasikia hizo nchi kutakiwa au kushauriwa kuwa za Kiislamu. Badala yake
nchi hizo zinashiriki kikamilifu kakika shughuli za OIC kwa sababu ya maslahi
yake. Aidha, kwa maoni yetu, nchi kuwa yenye Waislamu na Wakiristo ndio
sababu nzuri zaidi ya nchi hiyo kujiunga, na sio kutojiunga na jumuiya
hizo za kimataifa ama za Kiislamu au za Kikristo. Hivi sasa kwa mfano nchi
yetu tayari ni mwanachama wa jumuiya ya madola (ya Commonwealth) ambayo
kiongozi wake lazima awe Mkristo na mkuu wa Kanisa la Kianglikana; na hii
haifanyi Tanzania, Kenya, Uganda, Nigeria n.k kuwa nchi za Kianglikana.
-
Bali hata ingalikuwa Tanzania haijajiunga na jumuiya kama hizo, isingekuwa
vibaya kuanza kwa kujiunga na OIC. Kwani Watanzania tunajiamini na tunajulikana
kwa utamaduni wetu mkubwa na mzuri wa kuvumiliana katika masuala ya itikadi.
Mfano nzuri ni kwamba katika Tanzania Waislamu na Wakristo wanapumzika
Jumamosi na Jumapili, na sio Ijumaa na wanasherehekea mwaka mpya wa Kikristo,
na sio wa Kiislamu. Aidha Vatican inayo mwakilishi wake hapo nchini ambae
amepewa hadhi na anatambuliwa na kuheshimika kama Balozi. Ikiwa haya na
mengi mengine ya aina hii yanafanyika hapa Tanzania kwa usalama na amani,
ni dhahiri kwamba hakutakuwa na tatizo nchi yetu ikiboresha uhusiano wake
na nchi za Kiislamu au ikijiunga na OIC.
-
Zaidi ni kwamba tunataka Tanzania iboreshe uhusiano wake na nchi za Kiislamu
kama invyoboresha uhusiano wake na nchi za Kikristo, na ijiunge na jumuiya
za kimataifa za kidini sio tu kwa maslahi ya kiroho, bali pia kwa maendeleo
ya kidunia. Ikijiunga na OIC, nchi yetu itastahiki misaada na mikopo kama
ile ya Islamic Development Bank (IDB) ambayo ni nafuu zaidi kuliko mingi
tuipatayo kutoka jumuiya au nchi nyingine. Aidha, kwa kufanya hivyo nchi
yetu itakuwa imejipatia jukwaa jengine ambalo ni muhimu kwa harakati zake
za kidiplomasia.
-
Pili, kulitokea upinzani mkubwa katika Bunge, wakiwemo baadhi ya Mawaziri,
dhidi ya Waziri wa Elimu na Utamaduni, Mhe. Juma Kapuya, kwa sababu ya
kutangaza baadhi ya yale mambo ambayo wewe umeagiza yatekelezwe. Katika
maelezo yake Mhe. Kapuya alizungumzia:
-
Haki ya wanafunzi wa itikadi mbali mbali ya kuabudu nyakati za sala, na
kuvaa mavazi yanyokubalika katika maadili yao.
-
Wajibu wa wanafunzi wa kuendesha miradi yao ya uchumi kwa kuzingatia tafauti
za udini zilizopo bila ya kuleta bughudha kwa kundi au dhehebu lolote.
-
Jukumu la Wizara la kuhakikisha kwamba suala la udini halijitokezi wakati
wa kujaza fomu za maandalizi ya kujiunga na Kidato cha 1, cha V pamoja
na kujiunga na mafunzo ya ualimu.
Maneno haya, ambayo yangelisaidia sana kuonesha kwamba serikali haiko dhidi
ya dini, Waziri Kapuya alilazimishwa sio tu kuyafuta, bali pia kuomba radhi
kwa kuyatamka. "Kama anahitaji kubaki waziri", Mbunge mmoja alimwambia,
"basi aondoe suala la udini kwenye bajeti". Jambo ambalo, pamoja na kufanya
Serikali ionekane kuwa dhidi ya dini, limesababisha Waislamu kuandamana
na baadhi yao kupigwa na kutiwa ndani.
Tunashukuru kuwa kwa upeo wako mpana, ulibainisha hivi karibuni kwamba:
-
Wapo wanasiasa au viongozi wengine wa jamii wanaozungumza wazi wazi lugha
ya udini, ukabila na majimbo. Tusiwapuuze na wala tusiwaonee haya.
Tunakubali kauli yako hiyo kwa ukweli wake; kwani hata katika tukio hili
baadhi ya viongozi wa aina hiyo wamejitokeza. Akiashiria Mhe. Kapuya, Mbunge
mmoja alifika kusema kwamba: "Al-Haji hafai kuwa Waziri". Ila, kinyume
na maagizo yako, viongozi hawa sio tu hadi sasa wamepuuzwa, bali pia walishangiliwa
na wabunge wenzao Wakristo wa chama tawala na vile vya Upinzani. Wabunge
Waislamu wa chama tawala walioomba kuchangia katika mada hii wakati huo
walinyimwa nafasi na Mhe. Spika. Mawaziri waliokuwepo pia walihiari kukiuka
maadili ya "collective responsibility" kuliko kumuunga mkono waziri mwezao.
Kauli za aina hii hazikusikika kabisa wakati Mhe. Rev Simon Chiwanga alipokuwa
Waziri wa wizara hiyo!
-
Tatu, kumetokea teuzi mbali mbali za viongozi wa Chama, Serikali na Mashirika
ya Umma. Wahusika wa teuzi hizo hawakuonekana kuzingatia suala la uwiano
baina ya waumini wa itikadi tofauti; jambo ambalo linaonesha sio tu kupuuza
Madai ya Waislamu, bali pia kutokujali maelekezo yako. Katika chaguzi ndogo
zilizofanyika Temeke na Ubungo hivi karibuni, kwa mfano, CCM iliteuwa wagombea
wote wawili kutoka dini moja. Aidha katika bodi la ya Wakurugenzi wa shirika
la PPF walioteuliwa hivi karibuni wote ni kutoka dini moja; na wale watatu
ambao walikuwemo kabla wa dini nyingine wametolewa kwa mpigo. Mifano ya
aina hii ni mingi na hapa hatuwezi wala hatuhitaji kuitaja yote. Ila ni
muhimu kutanabahi kwamba Waislamu wanaangalia kwa makini sana teuzi zote
zinazofanywa hivi sasa katika CCM, Serikali na Mashirika ya Umma.
-
Nne, kumekuwa na Mkutano Mkuu wa Bakwata ambao umefanyika Dodoma mnamo
siku ya Alhamisi, tarehe 29/07/1999. Ukihutubia katika ufunguzi wa mkutano
huo kama mgeni rasmi ulisema kuwa:
Uko tayari, na kwa kweli, umeshaanza kuyashughulikia matatizo ya kitaifa
yanayohusu Waislamu.
Halmashauri inakupongeza kwa ujasiri huo wa kuweza kuwatangazia wananchi
kwa jumla yale ambayo ulitueleza sisi kabla. Kauli hii sasa imeweka wazi
kuwa, pamoja na kutambua kuwepo kwa "imbalances" kadhaa dhidi ya Waislamu,
umekubali kubeba jukumu la kuziondoa. Ila kutokana na hutuba hiyo, masuala
mengine yamejitokeza ambayo tunahitaji, na kwa hiyo, tunaomba ufafanuzi
wake:
-
Kwanza, kuna suala la "machanism" ambayo itatumika kusawazisha hizi "imbalances".
Ukizungumzia suala hili ulisema:
-
Serikali haitasuta kumchukulia hatua kali mtu yeyote atakae bainika akimbagua
mwengine katika masuala ya elimu, ajira, upandishaji vyeo na utoaji wa
leseni au hati mbali mbali kwa misingi ya jinsia, dini, kabila au eneo
anakotoka mtu.
-
Serikali haiwezi kuweka kanuni ya kudumu ya kugawa vyeo kwa misingi hiyo
ya udini, ukabila na jnsia.
-
Kwa faida ya taifa ni vizuri tugawe vyeo kwa vigezo vya ujuzi, uwezo na
upimaji makini wa matokeo ya kazi.
Kuhusiana na suala hili sisi tuna maoni tafauti na, kwa hiyo, ni vyema
kukutana na kubadilishana mawazo. Sisi tunaona kwamba:
-
Haitakuwa rahisi kuwachukulia hatuwa wabaguzi bila ya kuwa na vituo vya
kutosha vyenye taratibu madhubuti na uwezo wa kupokea na kufuatililia madai
ya wanaobugudhiwa.
-
Itakuwa vigumu kukomesha ubaguzi na kuhukumu wabaguzi kama hakutakuwa na
sheria maalumu, hata kama ni ya muda ya kufanya hivyo.
-
Katika kuomba au kutoa nafasi za elimu au ajira, utaratibu wa kutumia nambari
badala ya majina ni vyema utumike; kwani usipo saidia kuinua wanyonge,
utasaidia kuondoa zana ya upendeleo.
-
"Affirmative action" au "positive discrimation" tayari inatumika hapa nchini
na inasaidia kuinua wanyonge wa jinsia; kwa hiyo ni bora pia ijaribiwe
katika kuinua wanyonge wa dini, kabila na maeneo, n.k.
Hii sio kwamba tunapendekeza kuwa wanyonge hao wapewe nafasi hata kama
hawafai. Halmashauri inakubaliana nawe moja kwa moja kwamba ugawaji wa
vyeo ni lazima uzingatie ujuzi na uwezo. Ila tunaomba kuwa kuna haja vile
vile ya njia ya kuhakikisha kwamba wanyonge wenye uwezo na ujuzi hawakoseshwi
vyeo kwa misingi ya dini au kabila; na wale wanaopewa vyeo miongoni mwao
hawasumbuliwi kwa maneno; kama vile: "Al-Haji (au Reverend, hata kama ni
Profesa) hafai kuwa Waziri". Kukiwa na njia hiyo, wanyonge hawatapendelewa
ila kutakuwa na uhakika wa wao kupata haki yao, bila ya kudhulumu au kudhulumiwa.
Kwa maneno mengine, sisi tunaona kuwa si vyema uwezo na ujuzi
kuwa ndio vigenzo pekee vya kuzingatiwa katika kugawa vyeo. Kuna haja pia
ya kuwa na "mechanism" ya kuzuia watu wa dini, kabila au jinsia moja kuchukua
vyeo vyote au (vingi mno) mpaka wenzao wa dini, kabila au jinsia nyengine
wakakosa kabisa (au wakapata vichache sana) hali nao
wanafaa. Kwa hiyo,
badala ya kuchagua baina ya vigezo vya kabila, jinsia na dini kwa upande
mmoja, na vigezo vya ujuzi, uwezo au uzalishaji kwa upande mwengine, ni
muhimu vigezo vyote hivi vitumike kw wakati mmoja.
-
Kisha, kuna suala la matokeo ya utafiti ambao sote tumefanya. Hotuba yako
imetupa hisia kwamba sasa Serikali imemaliza kufanya utafiti wake juu ya
Madai ya Waislamu; na ndio maana iko tayari kuyashughulikia. Ila pia hotuba
hiyo imetupa wasiwasi kuwa labda "conclusion" ya utafiti huo ni tofauti
ba ile ya utafiti wa Halmashauri. Wasiwasi huu umekuja baada ya kusikia
kauli yako kwamba:
-
Hakuna mchujo wowote katika kuandikisha watoto shule, kwenda sekondari,
au vyuo vikuu, au katika ajira, unaofanywa kwa msingi wa kuwabagua watu
wa dini fulani. Hiyo nawahakikishia kabisa.
-
Na kama yupo mwenye ushahidi kwamba mwanafunzi fulani amezuiliwa kuendelea
na elimu kwa sababu tu ya dini yake, jinsia yake au kabila lake basi wanaohusika
wajulishwe.
Kama hii ndio "conclusion" ambayo Serikali imefikia baada ya utafiti wake,
basi bila shaka inatofautiana na ile ya Halmashauri. Kwa hivyo, kuna haja
ya kukutana ili kubadilishana "notes" na kufanya uchambuzi wa pamoja. Kinyume
na uoni huo, sisi tunanona kuwa mchujo upo; ila labda mchujo wenyewe si
rasmi, au haufanywi kwa makusudi. Ni maoni yetu pia kwamba, ili tuweze
kuondoa mchujo huo, ni muhimu tukubaliane kwanza kwamba upo. Sisi tunaamini
kuwepo kwake kutokana na hoja kadhaa. Baadhi ya hoja hizo ni kwamba:
-
Ukosefu wa ushahidi wa kwepo kwa mchujo, si uthibitisho wa kutokuwepo kwa
mchujo huo; kwani ushahidi unaweza kukosekana hata kama mchujo ukiwepo
madhali unafanywa kwa siri au uangalifu wa kutosha.
-
Ushahidi wa kesi za mchujo si rahisi kupatikana kwa kuwataka wanaobaguliwa
waripoti kesi zao kwa wahusika au hata kwa Rais mwenyewe. Kwani mara nyingi
hao wahusika huwa hawajulikani au wenyewe ndio wabaguzi. Aidha si rahisi
kwa mwananchi wa kawaida kuwa na uwezo na ujasiri wa kufika Ikulu.
-
Athari ya mchujo ipo, inaonekana, nayo ni hizi "imbalances" ambazo tunakubaliana
kwamba zipo.
-
Itakuwa ni kitu cha ajabu sama mchujo kutokuwepo; kwani kwa kawaida, binadaamu
haachi kuchuja (kujipendelea yeye mwenyewe na kupendelea walio wake) kama
hakuna cha kumzuia.
-
Takwimu zetu zinaonyesha kwamba watoaji wa nafasi za masomo au ajira wengi,
kama si wote, ni waumini wa dini moja; na wanaopewa nafasi hizo wengi,
kama si wote, pia ni waumini wa dini hiyo; ila wakosaji sasa, kama si wote,
wengi wao ndio waumini wa dini vyingine.
-
Halafu kuna suala la kujenga badala ya kubomoa madaraja ya kijamii. Ni
vyema umelitaja suala hili katika hotuba yako; na umesema kuwa:
-
Mojawapo ya visingizio vinavyotumiwa na wanaotaka kuvunja madaraja ya umoja
na utaifa wetu ni kwamba watu wa eneo fulani wameachwa nyuma, au watu wa
dini fulanai hawapewi nafsi fulani katika uongozi wa nchi na jamii.
Ikizingatia suala hili, Halmashauri imeona ni muhimu vile vile kuwa hadhari
sana watu ambao nao wanaweza kuvunja madaraja ya kijamii kwa kusingizia
kwamba hakuna ubaguzi, hali upo; au hakuna watu wa dini, kabila, jinsia
au eneo ambao wameachwa nyuma kimaendeleo au wamenyimwa au nyadhifa, wakati
wapo.
Mheshimiwa Rais, huu ni muhtasari wa baadhi ya yale tulionayo moyoni ambayo
tunapenda kushauriana nawe. Baada ya kukubaliana kuhusu kuwepo kwa "imbalances"
dhidi ya Waislamu; ni muhimu sasa tukutane kujadili "mechanism" ya kusawazisha
hizo "imbalances". Hapa tunajaribu kubainisha baadhi ya tofauti zilizopo
baina yetu katika suala hili kwa kueleza rai yako na kutoa maoni yetu,
ambayo kwa ufupi ni:
-
Kuwa na utaratibu wa nambari badala ya majina katika kuomba na kutoa nafasi
za elimu;
-
Kutumia mpango wa "positive discrimination" au "affirmative action" katika
kutoa nyadhifa na ajira;
-
Tanzania kuboresha uhusiano wake na nchi muhimu za Kiislamu kwa kufungua
balozi zake katika nchi hizo na kujiunga na OIC;
-
Mahkama za Makadhi kurudishwa;
-
Serikali kukemea propaganda potofu na kukomesha ubaguzi dhidi ya Waislamu
kwa:
-
Kuanzisha tume ua kuchunguza kesi muhimu za aina hiyo, hususan Kesi ya
Mwembechai;
-
Kuanzisha vituo maalum na vya kutosha vya kupokea na kufuatilia kesi za
ubaguzi.
Kwa hivyo, tunaomba kukutana nawe mapema, ikiwezekana, kuzungumzia kwa
kina suala hili la "mechanism". Kwani, kama maradhi, matatizo huzidi kila
yanapochelewa kutatuliwa na hayaondoki kwa kuondoa tu dalili (symptoms)
zake. Kama tulivyokubaliana kuhusu kuwepo kwa "imbalances" dhidi ya Waislamu,
tuna imani kwamba tutakubaliana pia juu ya "mechanism" ya kuzisawazisha.
Aidha tunaomba kukutana nawe ili kupata ufafanuzi juu ya hi hali iliyojitokeza
ya baadhi ya watendaji wa CCM na Serikali kufanya mambo kinyume na maelekezo
yako. Hali hii imeonekana zaidi katika utekelezaji wa maelekezo yako kuhusu:
-
Kutatua matatizo ya Waislamu yanayohusu "hijabu", sala wakti wa ibada na
kuwepo kwa mabaa (bars), nyumba za wageni (guest houses), ufugaji ovyo
na uchuuzi wa nguruwe na mabucha yake.
-
Kuzingatia suala la uwiano baina ya watu wa itikadi tofauti katika uteuzi
wa viongozi mbalimbali.
-
Kutozungumza lugha ya udini, ukabila na majimbo.
Tukiamini kwamba utatukubalia ombi letu, tunatanguliza shukrani.
Ahsante.
Al-Miskry, Saleh
Secretary.