NAOMBA nafasi katika gazeti lako nipate kueleza dukuduku langu kuhusu majibu ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani katika gazeti la Nipashe namba 01193 la Mei 32, 1998 lenye kichwa cha habari ‘Serikali yamjibu K.K.
Mosi ya yote nimefurahishwa na jinsi viongozi wetu wa Serikali ya awamu ya tatu wanavyotibu dalili za ugonjwa. Wanavyoangalia alikoangukia bila kuangalia alipojikwaa. Meja Nswima katika kueleza kwa nini vikundi vya dini lazima vishughulikiwe, ametoa mfano wa Kanisa la Kakobe juu ya mwanamke aliyechukuliwa dhahabu.
Katika hilo, serikali imeonyesha udhaifu, kwani tulitegemea wale wote waliohusika wangekamatwa kwa wizi Kanisani na wakaliacha Kanisa likaendelea na kazi zake, kwani kazi ya Kanisa zinaeleweka.
Je kama kila kosa likitendeka katika taasisi itakuwa ni kufuta, basi jeshi la polisi lingekuwa la kwanza kufutwa, kwani mauaji yaliyofanyika Arusha ya watu saba na polisi halafu kusingizia raia, mauaji ya Luteni Jenerali Kombe, mauaji ya kijana mzururaji kwa kukosa shilingi mia tano na kuamua kukimbia kumbe alikuwa anakabidhi maisha kwa askari.
Pili, Tume ya Jiji kujigawia viwanja wenyewe kule Buza na Boko badala ya waathiriwa wa mabondeni ni kielelezo cha kufanya kinyume na majukumu, lakini je tufute? Sikwambii mahakama ya Mwanzo kumhukumu mbwa Imigration kifo kinyume cha sheria wakati ndio taasisi ya kulinda haki. Je, mahakama zote za Mwanzo zifutwe?
Kuhusu kikundi kilichosajiliwa kwa ajili ya kuendeleza Qur’an badala yake kinapora Miskiti, hilo ndio ameonyesha dhahiri kwamba inafanya kazi zake kwa hisia au inaficha ukweli.
Vipi unaposema unaendeleza Qur’an una maana gani? Je, kuendeleza ni kuweka mashindano ya wasomaji na kutoa zawadi? Mungu anasema: "Na kwa hakika Misikiti (yote) ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuabudu yoyote pamoja na Mwenyezi Mungu". (Qur’an 72:18)
Mwenyezi Mungu anasema tena: "Wanaoamrisha Misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na kusimamisha sala na kutoa zaka na hawamuogopi yeyote ila Mwenyezi Mungu, basi hao ndio wanaotarajiwa kuwa miongoni mwa walioongoka." (Qur’an 9:18)
Ili kuendeleza Qur’an lazima uhakikishe kuwa Misikiti inayoabudiwa humo Mungu inasimama na wale wenye sifa. Kwa kifupi bado serikali haijajibu hoja za Mh. Kitwana Kondo (K.K.)
M. Masoud, Qiblatein Mosque, Box 16617, Dar es Salaam.
Lakini kwanza napenda nitoe shukrani na pongezi zangu za dhati kwa Mh. Kitwana Kondo kwa kutusaidia Waislamu kuthibitisha sisi wenyewe namna serikali hii ilivyo kwa Waislamu na Uislamu. Hebu Waislamu wote turejee kwenye hoja zilizotolewa na K.K. kisha tuliunganishe na tamko la serikali kama lililovyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani. Vipengele vilivyoelezwa na K.K. ni hivi vifuatavyo:
Kwanini Waislamu hawapati dhamana, matibabu na hata mtu akijitolea kupeleka dawa anakataliwa.
Kwanini serikali inawatisha wafanyabiashara wasitoe misaada kwa taasisi halali za Kiislamu.
Kwanini anayesema Yesu si Mungu anaswekwa ndani.
Kashfa ni nini, kwanini Muislamu akiandika kwenye baiskeli yake, Yesu si Mungu anakamatwa, ila yule anayeandika Yesu ni Mungu haulizwi? Je, hiyo haimaanishi kuwa serikali ina uhami Ukristo dhidi ya Uislamu?
Kwamba Serikali isivifute vikundi vya kidini, na iache tabia ya kuvitisha vikundi vinavyoikosoa.
Serikali iwafutie mashitaka wale wote waliokamatwa kwa kusema Yesu si Mungu na iwape dhamana Waislamu wa Kadhia ya Mwembechai.
Kwa muhutasari, hivyo ndivyo vipengele vilivyozungumzwa na Mh. K.K. lakini kwa mshangao wa Waislamu na wapenda amani wote, serikali hii ya ukweli na uwazi imeshindwa kabisa kutoa maelezo ya uwazi na ukweli wake kwa kipengele baada ya kipengele.
Abdallah H. Kapambala, Box 21094, Charambe.
MIMI ni Mkristo, lakini pia ni msomaji mzuri wa gazeti la Waislamu ANNUUR. Nasoma gazeti hili ili kuweza kujua upande wa pili unasemaje. Yesu Kristo pia alipenda mara kwa mara kujua watu wanasemaje kuhusu yeye, na je, wanafunzi wake nao wanasemaje (Matayo 16:13-15).
Pamoja na hayo, nimefurahishwa na hatua ya gazeti hili kuruhusu watu wa dini nyingine kutoa mawazo yao kuhsu maendeleo ya Waislamu.
Mimi nakubaliana kabisa na Bw. John Mtaki kuwa kwa muda mrefu Waislamu wamejengewa hisia kwamba wanaonewa na kudhulumiwa. Tabia hii imejengeka muda mrefu sana bila wao kuangalia wamejishughulisha vipi katika kuleta maendeleo yao wenyewe.
Miaka ya nyuma, Waislamu walijishughulisha sana na Elimu- Ahera kiasi cha kusoma madrasa tu na kuridhika kabisa. Hawakujishughulisha na kujenga shule wala hospitali, ni siku za hivi karibuni tu ndipo Waislamu wameona umuhimu wa kujenga shule zao wenyewe. Na hata shule walizojenga, haziendeshwi kwa ufanisi ikilinganishwa na wenzao Wakristo. Ukweli huu Waziri Kapuya ameubainisha, lakini wale wale waliojengea Waislamu hisia za kuonewa na kudhulumiwa walianza kupinga. (Angalia ANNUUR la tarehe 1-7 Mei, 1998 na Maalim Mwalimu) na kutolewa sababu za ovyo ovyo kuwa Waislamu shule zao hazifanyi vizuri kwa sababu zimejengwa mjini kwenye kelele za madisko!
Ni vyema Waislamu wakajengwa hisia zinazowachochea wafanye maendeleo yao kuliko kuwajenga hisia za kuonewa na kudhulumiwa hivyo kuwadumaza wasifikirie mambo mengine ya maendeleo.
Huko nyuma, Mwalimu Nyerere aliona mapema hatari ya Watanzania wa kundi moja kupata elimu na wengine kubaki na elimu duni hivyo akataifisha mashule ya Wakristo na kutoa mwanya kwa Waislamu kupata elimu. Hatua hii ya Baba wa Taifa ni ya kupongezwa lakini kama kawaida, watu waliojengewa hisia za kuonewa bado hawalioni hilo.
Makamu wa Rais, Dk. Omar Ali Juma majuzi alipogusia hisia za kuonewa, Gazeti hili lingefanya kazi kubwa ya kuwajenga Waislamu tabia ya kujiamini na kufuta hisia za kuonewa zilizojengeka.
Kwa upande wa imani, Wakristo na Waislamu wote ni watoto wa Ibrahimu (Mwanzo 21:9) na watoto hawa walicheza pamoja kwa amani.
Tofauti zetu za imani isiwe tabu. Taabu ambayo naiona mimi inaanzishwa na Waislamu wenyewe. Lakini kama Waislamu wangehubiri kama Qur’an tukufu inavyosema kusingekuwepo migongano. Qur’an tukufu inasema Issa siyo mwana wa Mungu (4:172) Issa hakufa msalabani (4:158) n.k.
Mimi nashauri Waislamu watamke Issa kama Qur’an inavyosema, lakini hakutakuwepo na migongano kwa sababu Wakristo hawamjui Issa ambaye hakufa, ambaye si mwana wa Mungu n.k. Hivyo kila upande utabaki na imani yake bila kuingiliwa.
Elia Batendi,
Box 538, Dar es Salaam.
NAMSHUKURU Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia nafasi hii adimu. Suala la Waislamu kuwa na Kadhi ni suala ambalo kwa sasa limefikishwa Bungeni ili liweze kujadiliwa na kufikia hatma. Mheshimiwa Mrema, Mbunge wa Temeke ndiye aliyeipeleka hoja hiyo. Haikupita muda mrefu Bakwata ilipeleka salamu zake Bungeni akiwaomba wapitishe hoja hiyo.
Yawezekana ya kuwa huu mpango wa Kadhi ni matayarisho ya kitu fulani ambacho kimejificha. Au ni matayarisho ya utekelezaji wa Dira 2025 ya serikali. Imeeleweka ya kuwa Waislamu hawaungi mkono Bakwata hivyo kinataka kutumika chombo ambacho Waislamu watakuwa na mawazo kuwa chetu, kumbe sio chetu.
Kadhi sio mahitaji ya haraka kwa Waislamu. Napenda kwa ufupi niorodheshe mahitaji ambayo Mrema pamoja na Sheikh wa Bakwata wangepeleka bungeni. Sio bungeni tu hata katika Dira ya 2025.
Waislamu wanataka wapatiwe nafasi sawa za elimu kuanzia darasa la kwanza mpaka vyuo vikuu.
Waislamu wanataka washiriki katika kazi mbalimbali nchini, pamoja na kushika madaraka ya uendeshaji wa nchi.
Waislamu wanataka kuchagua au kuchaguliwa kwenye Mabaraza ya Utungaji Sheria.
Waislamu wanataka wawe huru kuendesha mambo yao wenyewe kupitia katika vyombo vyao walivyochagua wenyewe na kujiunga na mashirika ya kimataifa kama OIC n.k.
Waislamu wanataka au ni amri kwao kutangaza dini yao bila kizuizi.
Muumini, Tanga.
BAKWATA imesema kwamba haijatoa msaada kwa sababu haijaombwa na Waislamu wala haijaelezwa kumetokea nini. Maana yake haijui kwamba kwa Waislamu waliouliwa wala walioko gerezani!
Waislamu ni juu yenu kuwaendea au la. Lakini binafsi naona Kadinali Pengo ana afadhali. Angalau anajua kilichotokea na kutoa maoni yake hadharani.
Huyu kwetu ni wa msaada mkubwa kwa sababu tunaujua msimamo wake.
Alihaq Msuya, Arusha.
NAPENDA kumjibu mzee wa Kamati ya wazee waliokabidhiwa Msikiti na serikali ambayo haina dini. Maelezo yake katika gazeti la Mfanyakazi la Mei 9, 1998 siku ya Jumamosi kuwa waumini wamehama Msikiti huo kwa hofu ya kukamatwa. Sio kweli wala si sahihi.
Napenda kumjulisha kuwa sisi waumini tumehama Msikiti si kwa kuogopa polisi au kukamatwa, kilichotufanya tuhame Msikiti ni haya yafuatayo:
Uongozi uliowekwa na serikali isiyo na dini haukubaliki na waumini.
Serikali ilisema imewakabidhi wadhamini Msikiti wao ikizingatiwa Misikiti yote ni ya Mwenyezi Mungu.
Waumini hawawezi kusali kwenye Msikiti wa Wadhamini au watu fulani, wanasali kwenye Msikiti wa Mwenyezi Mungu tu.
Hayo mambo ndio yamefanya sisi waumini kuhama Msikiti wao au nyumba yao hao wadhamini.
Tunachoomba wao wasali waache kutafuta waumini walichotaka ni Msikiti na Msikiti ndio huo wanao tumewaachia sasa wanaita waumini wa nini? Na wao wanatosha.
Naomba Waislamu msimamo ndio huo hamna kurudi nyuma kwani ukisali katika Msikiti wa Mwembechai nadhani utakuwa huna sala ukizingaita walio sababisha Waislamu kuuawa na Waislamu kuwekwa magerezani ni hao wanaosimamia (serikali) Msikiti huo.
Nasititiza umoja na mshikamano ili Uislamu uende juu kwani ndio dini ya haki Qur’an 3:19.
Maimuna Mtumwa, Dar es Salaam.
SASA imedhihiri kwamba kweli Bakwata chombo cha Serikali na adui wa Uislamu.
Toka Waislamu wauliwe limekaa kimya; lakini kuguswa tu serikali limetaharuki na kutoa shutuma kali dhidi ya mzee wetu K.K.
Lakini ukweli uko pale pale kwamba serikali imewadhulumu. Na dawa si kumkashifu K.K. bali kuiondoa hiyo dhulma.
Juma Kupela, Tandale, Sokoni.
BAKWATA imedai kwamba Mh. Kitwana Kondo kala fedha za Sheikh Kassim Foundation; hilo watathibitisha mahakamani.
Lakini tungependa kufahamu yafuatayo: Fedha za nyumba za Wakfu toka wamepora toka EAMWS ziko wapi? Au zimefanya nini? Nyumba hizo zilikuwa ngapi na leo ngapi? Zingine wamemuuzia nani?
Hamza H.S. Dar es Salaam.
Kutokana na kuzidi kwa matatizo ya uongozi mbaya wa BAKWATA katika Wilaya ya Misungwi,tumeonelea kukuandikia barua ya wazi ukiwa kama Sheikh wa Mkoa wa BAKWATA.
Kwanza kabisa tunapenda kukufahmisha kuwa hapa Misungwi hivi sasa kuna misikiti miwili mmoja uko chini ya baraza kuu na mwingine uko chini ya Bakwata.
Tunachukuwa nafasi hii kukufahamisha sababu zilizopelekea mpaka kupatikana msikiti wa pili hapa Misungwi, nadhani muheshimiwa Sheikh, kwa muda mrefu wewe ndie ulie kuwa mpatanishi wetu kutokana na matatizo yaliyokuwa yakitokea kwa Waislamu hapa Misungwi na wakati huo kulikuwa na Msikiti mmoja tu,ambao ulikuwa uko chini ya Bakwata na wewe mara nyingi ulikuwa ukiyatatua matatizo hayo kwa njia ya Qur’an na Sunnah.
Zaidi ya matatizo hayo ilikuwa ni waumini kuwaomba viongozi wa msikiti mapato na matumizi ya msikiti pia kutaka spika za msikiti zisitumike ila katika yanayouhusu Uislamu.
Spika zilikuwa zikitumika kutangaza kodi ya maendeleo ndani ya msikiti na mikutano ya kisiasa hivyo matatizo kama haya uliwahi kuyasikiliza na ukayatolea ufafanuzi kwa kuwasihi viongozi watowe mapato na matumizi ya msikiti kwa waumini na Spika isitumike kutangaza mambo ya kodi ila itumike kwa ajili ya mambo ya Kiislamu na ukaongeza kwa kusema ni makosa makubwa kutangaza katika msikiti habari za kodi.
Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’an suuratil jinni aya ya (18) hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu asiabudiwe yoyote pamoja na Mwenyezi Mungu.
Baada ya kutoa nasaha hizi pindi ulipoondoka mambo haya hayakukoma bali yaliendelea kama kawaida wakawa hawatoi mapato na matumizi ya msikiti pesa zinaliwa hovyo kwa maslahi yao.
Wakawa wanatangaza ndani ya msikiti mambo yasio kuwa ya Kiislamu pia wakawa wakiwazuiya wageni wa Kiislamu kutoa mawaidha msikitini kwa madai kuwa hawana kibali cha Bakwata.
Wageni wanapo haribikiwa safari hawana ruhusa ya kuomba msaada msikitini mpaka awe na kibali cha Bakwata, Waislamu walijitahidi kuyakemea mambo haya kwa juhudi zote. Lakini iliandikwa mhadhiri alie kuwa akikemea mambo hayo yasitendeke aliandikiwa barua nakala moja ya barua ikapelekwa katika kituo cha Polisi Wilaya ya Misungwi, barua hiyo ilikuwa ikisema kuwa msikiti ni mali ya Bakwata hivyo asiutumie yeyote kwa kuongea chochote labda atafute msikiti mwingine usiokuwa wa Bakwata kama atalazimisha atachukuliwa hatua za kisheria.
Je Qur’an na sunnah ndio vinatufundisha tukishindana katika jambo turejee katika kituo cha Polisi? Pia tunapenda kufahamu nakala ya barua hiyo waliopeleka katika kituo cha polisi na kwako ilifika? Kama haikufika basi utambuwe wazi kuwa wao wameona kituo cha polisi ni bora zaidi kuliko wewe ambaye unaweza kuturejesha katika Qur’an na sunnah.
Baada ya kuandikiwa barua hiyo na nakala moja kwenda polisi tukaona kuwa hapa hakuna tena utekelezaji wa maamrisho ya Mungu isipokuwa ni kutafuta mahala ambapo patakuwa msikiti na kutakuwa na uwezekano wa kutekeleza amri za Mungu.
Hizo ndizo sababu zilizopelekea kupatikana msikiti wa pili. Pia baada ya kuanzisha jumuiya ambayo mpaka hivi sasa iko chini ya Baraza Kuu la jumuiya na taasisi za Kiislamu Tanzania bado wanaendelea kuzua choko choko na kupeleka maneno ya uongo kila siku serikalini mara mahakamani kwa Mkuu wa Wilaya na hata kwa Afisa usalama wa Taifa wanadai kuwa hapa Missungwi yameanzishwa makao makuu ya siasa kali ya mkoa wa Mwanza na hivi sasa wanajiingiza katika vurugu ya Mwembechai, wanaweza kuhatarisha amani Misungwi na Mkoa wa Mwanza.
Hivyo Sheikh kwa kuwa tunazifahamu juhudi zako za kupambana na udhalimu tunategemea utafanya kama ulivyofanya kuwakemea viongozi wa Masjidi iliyopo Kirumba mjini Mwanza. Kama tulivyo soma katika gazeti la AN NUUR TOLEO NA 148 KUWA MAUAJI YA Mwembechai yanatuhusu Waislamu wote.
Kwani muda wanaoupoteza kutupiga vita sisi Waislamu wenzao ni bora wautumie katika kuleta maendeleo ya Uislamu,.
Tunatanguliza shukurani zetu za dhati kwako na ufanisi mwema katika jambo hilo.
Waumini, MISSUNGWI. Mwanza.