Wezi wa Fadhila!, hiyo fadhila yenyewe iwapi?

Mapema wiki hii vyombo vya habari vimemnukuu Mhe. Rais Benjamin William Mkapa akilipongeza kanisa kwa huduma zake kwa jamii ya Watanzania.

Katika pongezi hizo Mheshimiwa Rais amekaririwa akisema kwamba kwa kazi nzuri ya Kanisa, wapo viongozi leo (katika serikali) ambao si Wakristo walipata elimu yao katika mashule ambayo yalijengwa na makanisa.

Pongezi hizo Mheshimiwa Rais alizitoa katika hafla ya ufunguzi wa kituo cha elimu na Maendeleo Matemanga (Matemanga Centre for Education and Development) kilichopo katika kijiji cha Milonde, wilayani Tunduru.

Tunaamini kwamba pongezi hizi za Mhe. Rais zimetolewa kwa nia nzuri kabisa zikilenga kuzipongeza Jumuiya na Taasisi za kidini zinazotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii. Na pongezi hizo zimekuwa zikitolewa hata kwa taasisi binafsi.

Kwa bahati mbaya kuna watu wameijadili vibaya hotuba hiyo ya Rais na kudai kwamba Waislamu ni wezi wa fadhila.

Kufuatia malalamiko ya muda mrefu ya Waislamu juu ya kudhulumiwa katika elimu na kufuatia makala ya Mohamed Said katika gazeti hili juu ya maisha ya Almaruhumu Said Tewa, tumekuwa tukipokea barua nyingi zinazotoa maelezo na tafsiri tofauti juu ya malalamiko ya Waislamu.

Kufuatia kauli hiyo ya Mhe. Rais watu wengine wanaona kana kwamba ndio majibu ya serikali kwa Waislamu. Kwa ajili hiyo wanaitumia kuwasimanga Waislamu kuwa hawana shukrani kwani walisomeshwa katika shule za Misheni na bado wakabaki na dini zao, lakini bado wanalalamika.

Kama vile ambavyo tumesema kwamba pongezi hizi za Rais zimetolewa kwa nia nzuri ni vivyo hivyo tunaamini kwamba hazikuwa na lengo la kuwajibu Waislamu. Na kwa hiyo hatuthubuti wala hatuwezi kuthubutu kuijadili kinyuma na lengo lake zuri.

Lakini kwa hawa walioibuka na kuipa tafsiri potofu kauli ya Rais na kuanza kuwasimanga Waislamu mitaani, hawa ni lazima tuwajibu.

Awali ya yote ni lazima tusema kwamba Waislamu si wezi wa fadhila. Kwanza ili mtu awe mwizi wa fadhila ni lazima kwanza hiyo fadhila yenyewe iwepo.

Dhana iliyojengeka kwa wengi ni kwamba kanisa lilikuja na fedha zake kutoka huko litokako iwe ni Ujerumani au Uingereza n.k. likajenga mashule.

Pengine tuanze kwa kusema kwamba hakuna anayeweza kuleta hoja kupinga ukweli kwamba Kanisa lilitangulia kusafisha njia ya wakoloni kuja kututawala. Na lengo la Wakoloni halikuwa lingine ila kuchuma kupitia ardhi yetu raslimali zetu na kwa kuwafanyisha kazi kitumwa babu zetu.

Katika watu walioteseka ni pamoja na Wamatumbi waliofanyishwa kazi katika mashamba ya pamba toka alfajiri hadi magharibi wakiambulia dona na mijeledi kwa anayeonyesha kulegea hata kama anaumwa.

Ndio maana tunawakuta Wamatumbi wakiungana na Kinjekitile kupambana na dhulma ile ya mkoloni. Lakini wakati Wamatumbi wanaendesha harakati zile Wakuu wa Makanisa waliwatahadharisha watu wao wasishiriki.

Pamba hii na mazao mengine kama katani walipeleka kwao. Japo sote Waislamu kwa Wakristo tulidhulumiwa na Wakoloni,lakini wenzetu walijengewa Makanisa mazuri na shule. Leo fedha zile zile zilizotokana na raslimali zetu zikatajirisha Wazungu zinaletwa tena kuboresha makanisa, mashule na huduma nyingine za jamii.

Sisi tumedhulumiwa 100%. Vipi tusimangwe! Nani kamfadhili mwenzake! Sisi au wakoloni waliopora raslimali zetu na kututumikisha kitumwa kuwatajirisha!

Katika vitu ambavyo mkoloni alikuwa hana mchezo ni kukusanya kodi. Alikusanya kodi za kila aina mpaka ya kichwa. Sehemu ya pato la kodi hizo aliyakatia makanisa yajenge na kuendesha mashule. Kwa mfano mwaka 1957 shule ya Wakatoliki ya Minaki ilipewa kutoka mfuko wa Serikali paundi 40,000 kwa ajili ya majenzi na ununuzi wa vifaa. Kwa viwango vya leo fedha hizo ni sawa na shilingi milioni 40. Na hiyo ni kwa shule moja tu wakati ule mfuko wa saruji ukiwa bado pengine shilingi tatu.

Aidha, hii ni mbali na ile iliyokuwa inaitwa Grant-in Aid ya kusaidia gharama za uendeshaji. Fedha hizi zilitolewa kama "Capital Grant".

Kinachojitokeza hapa ni kuwa Wakoloni walichukua kodi zetu nusu na robo wakachukua kwao robo wakagawana na makanisa.

Tunaposimangwa leo kosa letu nini! Kusoma na kubaki na dini zetu! Kumbe hatukutakiwa tubaki na dini zetu! Au ni kwa kule kukaa kwetu kimya na kutokufungua kesi ya madai ya kodi zetu tulizodhulumiwa?

Lakini tunashukuru pia kwamba kuna kukiri kwamba tumesoma. Pengine sasa tuulize kubaki na dini zetu ndio kunatufanya tusipewe ukuu wa Wilaya na Mikoa. Maofisa Tawala Mikoa (RAS); Makatibu Wakuu, Ukurugenzi na Wenyeviti kuu "Parole".