Damu ya Muislamu isiishie tu kufukiwa mchanga

Jumatano Juni 3, Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu lilitoa kauli kusisitiza madai ya Waislamu kwamba kuna dhulma nchini hapa dhidi ya Waislamu.

Baraza Kuu lilitaja suala la Waislamu kunyimwa dhamana kushitakiwa kwa kusema Yesu si Mungu na upogo uliopo katika teuzi za watendaji na viongozi katika sehemu mbali mbali kama mifano ya kudhihirisha dhulma iliyopo.

Katika kauli yao Baraza Kuu limesisitiza kwamba upo uwezekano kwa Waislamu kutokutendewa haki inapokuwa hawashirikishwi katika sehemu mbalimbali muhimu. Watasharehesha nukta hiyo kwa kueleza kwamba wanaendesha mashtaka walio wengi ni Wakristo, Mahakimu na Majaji wengi ni Wakristo hali kadhalika maofisa wa ngazi za juu ni Wakristo. Katika hali hiyo Baraza Kuu limesema upo wasiwasi mkubwa kama Waislamu watatendewa haki.

Na wasiwasi huo si wa bure bure kwani tayari upo mfano hai wa Waislamu kuuliwa, badala ya wauaji kushitakiwa wanakamatwa na kushitakiwa wafiwa; wanaouguza majeraha ya risasi na waliokoswakoswa risasi!

Tunaamini kwamba Baraza Kuu wanalikumbushia jambo hili kama Maprofesa wa Chuo Kikuu walivyojitokeza kuyalaani mauaji yale kwasababu kunyamaziwa jambo hili ni hatari.

Hisia za kudhulumiwa, kuteswa na kuangamizwa kwa namna yoyote ile hakuwezi kufifilishwa kwa udhalimu zaidi au propaganda.

Leo ni mwaka wa nne toka mauaji ya mwaka 1994 huko Ruanda lakini mpaka leo Mahakama zipo wazi na faili hazijafungwa. Wauaji wamesakwa na wanaopatikana wanafikishwa mahakamani na kuhukumiwa. Ni juzi tu Tanzania imepongezwa kwa kutoa ushirikiano mkubwa katika kufanikisha kazi ya kuwasaka na kuwashitaki wauaji hao. Vipi leo idhaniwe Waislamu wao watasahau ile damu yao iliyomwagwa opale Mwembechai ilihali wahusika hawajakamatwa.

Mtoto wa Kiyahudi anayezaliwa leo akianza tu kwenda chekechea anajua nani alihusika kuiangamiza familia yake mwaka 1936/48.

Vitabu vimeandikwa na filamu zimechezwa ili kuziweka kumbukumbu hizi za mateso na mauaji ya kutisha waliyofanyiwa Mayahudi na utawala wa Hitler. Na mpaka leo miaka takriban sitini baada ya tukio, bado mahakama zipo wazi na mafaili hayajafungwa. Kila ambapo anapatikana ushahidi wa kutosha, watuhumiwa wa udhalimu ule wanafikishwa mahakamani na mtuhumiwa. Tunao mfano hai wa juzi juzi tu huko Ufaransa. Na Waislamu wa Tanzania kama kurithishana , basi huu ndio urithi wetu. Hili la Mwembechai haliishi kwa hotuba wala kupita muda. Kama ambavyo watoto wa Kiyahudi leo hata yule wa chekechea anajua ni nani Hitler na aliwafanyia nini babu na nyanya zake.

Rodney King alipigwa na kuteswa sana na polisi Wazungu wa Marekani. Hiyoo ilikuwa mwaka 1992 wakati wa utawala wa Rais George Bush.

Rodney King alikuwa njiani polisi wakamhoji maswali ambayo yaliishia kwa yeye kupigwa na kuteswa sana.

Wakati anateswa na kupigwa pale barabarani mtu mmoja alikuwa na video Camera yake, inasemekana ndio kwanza alikuwa ametoka kuinunua dukani, akajibanza mahali akaeikodi tukio lote lile.

Rodney King ni Mmarekani mwema baada ya kuteswa na kupigwa kesi iligunduliwa mahakamani jopo la majaji likawaona polisi wale hawana hatia.

Yule Bwana aliyelipiga picha lile tukio lote uchungu ukampata.

Hakuweza kuuvumilia ule udhalimu kwamba mtu anapigwa na kuteswa bila ya kisa halafu mtesaji anaachiwa huru na mahakama!

Yule Bwana akautoa ule "Mkanda". Athari yake baada ya "Filamu" ile kuonekana Los Angeles hapakukalika mji uliwaka moto. Hakula mtu wala kunywa maji mtu.

Mahakama za Marekani ni katika mahakama zinazosifika duniani kwa kuwa huru. Lakini Rais Bush ililazimika kusimama na kuwatuliza wananchi kwa kuwaahidi kwamba kesi hiyo itatizamiwa upya. Kwa mara ya kwanza Serikali iliingilia mahakama na Jopo jipya la majaji likateuliwa.

Rodney King hakuuwawa; alipigwa tu. Hapa mtu kauliwa kwa kulengwa shabaha. "Piga yule"; "mwongeze", Rodney King alikuwa peke yake. Hapa si mmoja tu aliyeuliwa! Rodney King wakufungwa pingu kitandani kama Chuki Athumani!

Filamu ya Rodney King ilionyeshwa siku nyingi tu baada ya tukio. Hapa tukio la piga yule limeonyeshwa pengine hata Muislamu yule kuingizwa chumba cha maiti!

Tofauti na Rodney King watu wameonyeshwa masaini kijana yule alitupwa ndani ya gari la polisi baada ya kuuliwa! Watu wanaonyeshwa poli9si wakifukia damu ya Ustaadh Isa Saleh kwa mchanga baada ya kudunguliwa risasi na kuongezwa nyingine ili kuhakikisha kwamba kafa!

Katika tukio la Rodney King polisi hawakujua kwamba yupo mtu kajificha mahali anapiga picha. Hapa kamanda mwenye cheo chake ametoa amri "pig yule". "Muongeze", alijua kwamba camera za picha za kawaida na za video zimemwelekea kuchukua picha yake pamoja na sauti yake!

Si hivyo tu na wakuu wake wa kazi wamemzunguka wakishuhudia nao wakipigwa picha!

Kwa Rodlney King Rais George Bush aliteua jopo jipywa la majiji baada ya lile la kwanza kutowatia hatiani watesaji. Hapa wauaji wanapongezwa; wafiwa wanashitakiwa na kutishwa zaidi na wale waliojeruhiwa kwa risasi wakafungwa pingu!

Hatukuwasikia wanasheria wala majaji kulizungumzia hili. Tunachojiuliza ni kwamba je; hawakulisikia au kulishuhudia tukio lile! Pengine hawana hisia za uchungu au tuseme nyoyo zao hazishuki wakiona dhulma.

Dhana zote hizo tunaamini si sahihi. Haiwezekani wawe hawakushuhudi tukio lile wakatileo wakati tunayaandika haya "Kaseti ile inatizamwa sehemu nyingi duniani. Wala haiwezekani ikawa hawanahisia za kuvionea huruma viumbe vya Mwenyezi Mungu kwani hawakuweza kustahimili walipoona kiumbe cha Mwenyezi Mungu kinadhulumiwa huko Sumbawanga.

Tena kile kiumbe cha Mwenyezi Mungu cha Sumbawanga hawakuona wakati kinauliwa wala hawakuona mazishi yake.

Kukaa kwao kimya katika hili kunatufanya tujiulize wenzetu hawa ni ujumbe gani wanatupa?

Katika kuhitimisha kauli yake Baraza Kuu lilisema kwamba kufumbia macho udhalimundiko kunakofanya wananchi wachukue hatua kama zile za Mwembecahi.

Tusingependa ifike siku Waislamu wasema "tulisema" kwama Baraza Kuu lilivyotahadharisha. Hata hivyo hilo litaepukika tu endapo dhulma itakomwa na kuondolewa.

Damu ya mtu isiishie tu kufukiwa kwa mchanga. Waliotoa amri "piga yule" wanajulikana na waliopiga wanajulikana. Hawa wakamatwe wafunguliwe mashtaka. Waeleze Waislamu wale walikuwa na kosa gani la kustahiki walengwe shabaha.

Kama lilivyosema Baraza Kuu kunajengeka utamaduni hapa mtu akidai haki au kuepeza dosari zilizopo huitwa mchochezi.

Lakini tunaamini kwamba hakuna namna ya kuinusuru nchi yetu zaidi ya hii ya kuzielezea na kuzikemea dosari zilizopo hasa zile zenye kujenga hisia miongoni mwa wananchi kwamba wao wanaonewa, wao wanadhulumiwa.

Uchungu wetu na uzalendo wetu juu ya nchi yetu hii ndio unaotufanya tuyasema, yote haya, tukiamini kwamba kila mmoja akidhaminiwa na akipewa haki yake na kile mmoja akitekeleza wajibu wake kwa uadilifu; nchi yetu itabaki katika salama na amani.