Bodi ya kusamehe wafungwa

Na Abu Kalam

JUMATATU Juni 1, 1998, Waziri Mkuu, Mh. Frederick Sumaye alizindua Bodi za mikoa na kitaifa zitakazosimamia utaratibu wa kusamehe wafungwa. Utaratibu huu, ambao kwa jina jingine unajulikana kama parole umeanzishwa nchini ili uweze kutumika kwa kuwaachia huru wafungwa ambao wameonyesha tabia na mwenendo mzuri wakati wakitumikia vifungo vyao.

Katika sherehe za uzinduzi, ilidaiwa kuwa mpango huu umeanzishwa kwa nia ya kuwasaidia wafungwa waweze kubadili mienendo yao ili hatimaye wawe raia wema katika jamii. Aidha ilidaiwa kuwa mpango huu unatumika na umefanikiwa katika nchi mbalimbali zikiwemo Uganda, Afrika Kusini na Canada.

Chini ya mpango huu, kila mkoa utakuwa na bodi yake ambayo itatathimini mwenendo wa wafungwa na kutoa maamuzi iwapo wanastahili msamaha au hapana. Walioteuliwa kuwa wenyeviti wa bodi za mikao ni:

Askofu Bruno Nyongani Lindi
Askofu Paul Ruzoka, Kigoma
Askofu Mario Mgulunde, Tabora
Askofu Justine Samba, Mara
Bw. Julius Matiko, Pwani
Bw. Angelo K. Mpuya, D'Salaam
Bw. Peter Feer, Tanga
Bw. Stephen Muna Jullah, Singida
Dk. M.A. Kipuya, Arusha
Balozi Job Lusinde, Dodoma
B. E. P. Siyovelwa, Iringa
Bw. Joseph Ndamugoba, Kagera
Bw. Chediel Mgonja, Kilimanjaro
Bw. David Mandanda Mtwara
Kanali Issac Mwisongo (Muislamu) Morogoro
Meja Jenerali James Luhanga, Mwanza
Chifu Edward Kasavila Kalavanda, Rukwa
Bw. Bruno Ndunguru, Ruvuma
Bw. Samwel Pundugu, Shinyanga

 
Kwa upande wa bodi ya kitaifa walioteuliwa kuwa wajumbe ni:

Julie Manning, Mwenyekiti
Askofu Elinaza Sendoro, Mjumbe
Simeon Mwanguku, Mjumbe
 

Imeripotiwa kuwa bodi ya kitaifa itakuwa na wajumbe tisa wakiwemo na Mwenyekiti. Hivyo basi wajumbe wengine sita bado hawajateuliwa.

Kutokana na wenyeviti wa bodi za mikoa na wajumbe wa bodi ya kitaifa imedhihirika kuwa walioteuliwa ukimuacha Kanali Issack Mwisongo, waliosalia wote ni wakristo. Katika orodha hiyo wamo pia Maaskofu watano.

Wananchi wengi wamehoji ni kwa vipi kwa muda wa miaka 37 sasa tokea kupata uhuru hakuna hata Muislamu mmoja (kati ya mamilioni waliopo) ambaye ana sifa ya kuchaguliwa ujumbe au uwenyekiti katika moja ya bodi hizi.

"Hivi kweli hata katika mikoa kama vile Tanga, Pwani, Kigoma, Lindi n.k. ambayo wakazi wake wengi ni Waislamu hakuna hata mmoja anayefaa kupata uteuzi huu", wamehoji wananchi kadhaa jijini Dar es Salaam

Aidha walidai kuwa kama hoja ni elimu, wapo Waislamu wengi sana ambao wana kiwango cha elimu ambacho ni kikubwa kupita wengi wa wenyeviti walioteuliwa.

Walitoa mfano kwa kuwataja Bwana Jumanne Mangara ambaye ana shahada ya pili ya Chuo Kikuu (sheria) na pia hadi hivi karibuni alikuwa Kamishna Mkuu wa Magereza Tanzania, pia yupo Bwana Hamza Aziz ambaye aliwahi kuwa Ispekta Jenerali wa Polisi na ana shahada mbili za Chuo Kikuu, vilevile wapo akina Profesa Issa Shivji, Bw. Othman Matata ambaye ana shahada ya sheria (Canada) na alishawahi kuwa Mwendesha Mashtaka, Juma Mwapachu na Mh. Kitwana Kondo ambaye aliwahi kuwa afisa Mwandamizi wa Jeshi la Polisi nchini.

Gazeti moja la Juni 4, limetaja kuwa yupo Sheikh Suleiman Kilemile katika Bodi ya Dar es Salaam. Pengine ingekuwa vyema basi serikali ikatutajia wajumbe wa Bodi za mikoa yote.

Kwa mujibu wa sheria namba 25 ya 1994 iliyotiwa sahihi na Rais tarehe 17 Januari 1995, sehemu ya pili ukurasa 236 kifungu cha 2(a) kinataja uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa.

"The National Parole Board shall consist of the Chairman who shall be a person vested with knowledge and xperience in legal matters or in administration of criminal justice, and who shall be appointed by the President".

Tafsiri:

Bodi ya Kitaifa ya Parole itajumuisha na Mwenyekiti ambaye atakuwa mtu mwenye ujuzi na uzoefu wa masuala ya kisheria au usimamiaji wa masuala ya jinai na atateuliwa na Rais.

Kifungu cha 3(a) kinazungumzia teuzi za Wenyeviti wa Bodi za Mikoa:

The Regional Parole Board shall consist of the Chairman who shall be appointed by the Minister and who is vested with knowledge and experience in legal matters or in administration or criminal justice.

Tafsiri:

Bodi ya Parole ya Mkoa itajumuisha na Mwenyekiti ambaye atateuliwa na Waziri na ambaye atakuwa mtu mwenye ujuzi na uzoefu wa masuala ya kisheria au usimamiaji wa masuala ya jinai.

Pamoja na kuwa tusingependa kuhoji utumiaji wa madaraka ya kisheria aliyopewa Rais na Waziri wa Mambo ya Ndani, lakini hivi kweli hawa Wakristo na Maaskofu wote walioteuliwa wamekidhi sifa zilizotajwa katika sheria hii? Je ni kweli kuwa Bwana Jumanne Mangara, Bwana Hamza Aziz, Bwana Said El-Maamry ambaye aliwahi kuwa Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (Senior Assistant Commissioner of Police) hawana sifa hizo? Je Waislamu wakijenga dhana kuwa serikali haiwathamini watakuwa wamekosea?

Linalotisha zaidi ni kuwa katika nchi yetu idadi kubwa ya wafungwa ni Waislamu. Aidha, idadi kubwa ya waendesha mashitaka ni Wakristo, idadi kubwa ya Mahakimu na Majaji ni Wakristo, idadi kubwa ya Maafisa Wandamizi wa Magereza ni Wakristo, na sasa hata Wenyeviti watakaoshughulikia misamaha wote ni Wakristo tena baadhi yao ni Maakofu. Je Waislamu watatendewa haki katika mfumo huu?

Kwa bahati mbaya uwiano huu mbaya umetawala katika taasisi zote muhimu katika nchi yetu. Baadhi tu ya mifano nikama ifuatavyo:
 
Taasisi  Waislamu   Wakristo 
Tume ya Jiji - Wakurugenzi 
0
9
Tume ya kurekebisha Sheria 
Tume ya Uchaguzi 
1
4
Makatibu Wakuu
5
22
Majaji wa Mahakama ya rufaa
0
7
Wakuu wa Mikoa
4
16
Makamanda Polisi wa Mikoa (RPC)
7
13
Maafisa Tawala wa mikoa (RAS)
1
19
 

Kwa upande mwingine, yawezekana kabisa hakuna Waislamu ambao wana sifa zinazohitajika kujaza baadhi ya nafasi hizo. Kama hivyo ndivyo, je serikali haioni hatari ya kuwa na kundi kubwa (mamilioni ya watu) katika jamii ambalo miaka 37 tokea tujitawale bado lipo nyuma kiasi hicho? Hata ukichukulia kiuchumi, nchi itakuwa inapata hasara kubwa iwapo kundi kubwa la raia wake lipo nyuma sana kiasi ambacho haliwezi kuchangia katika uongozi wa nchi yetu. Kwa vyovyote vile serikali inayojali raia wake itaiona hatari hii na kuchukua hatua  madhubuti kurekebisha dosari hii.

Kinyume chake, hapa nchini kwetu yeyote ambaye atazielezea dosari hizi na hatari zake, serikali imekuwa mstari wa mbele kuwabandika majina kama vile ‘wachochezi’, ‘siasa kali’, ‘Fundamentalists’, ‘wahuni’, ‘wakorofi wachache’, n.k. Hali hii ndiyo iliyowafikisha Waislamu kuchukua hatua kama zile za Mwembechai. Iwapo serikali ingekuwa inasikiliza kilio cha Waislamu yale ya Mwembechai yasingetokea. Wanaodai Waislamu si upendeleo bali wapewe fursa sawa kama raia wa nchi hii. Ipo siku tutakuja sema kuwa tulisema.