Msikiti wa Mwembechai wakarabatiwa

Na Mwandishi Wetu

Baada ya kuvamiwa na kuvunjwa kwa milango na baadhi ya sehemu ya msikiti wa Mwembechai na Polisi, na kisha kuhakikishiwa kuwa watalipwa kwa kukarabatiwa, hatimaye ukarabati umeanza ndani ya msikiti huo.

Ahadi ya kuufanyia ukarabati msikiti huo, ilitolewa na serikali wakati walipokuwa wakiukabidhi msikiti huo, mikononi mwa wadhamini, mara baada ya vurugu za miezi Februari na Machi, ambazo zilipelekea watu kufa, magari kuchomwa moto na ofisi kadhaa za CCM kuchomwa moto, huku watu wapatao 280 wakitiwa nguvuni, kuhusishwa na vurugu hizo.

AN-NUUR , iliweza kuona ukarabati huo unaofanyika ndani ya msikiti huo ulioko Wilaya ya Kinondoni, kwa kupakwa rangi mpya,kutengeneza milango iliyovunjwa kwa kuchongea milango mipya, inayotokana na mbao zilizoletwa msikitini hapo wiki mbili zilizopita na mafundi huchonga humo humo ndani ya msikiti sehemu za kutilia Udhu.

Ukarabati mwingine ulioonwa na mwandishi wa gazeti hili ni kutengenezwa kwa vyoo,vilivyokuwa katika hali mbaya, na pia kutengenezwa upande wa wanawake ambao ndio ulioathirika na fujo za askari polisi walioingia ndani ya msikiti huo mwezi wa Februari.

Ingawa ukarabati huo umeshaanza kwa kasi ili kuufanya msikiti huo kuwa kama misikiti mingine, lakini bado hali ya waumini msikitini hapo ni ndogo, ukilinganisha na ukubwa wake na ilivyokuwa awali kabla ya fujo na vurugu msikitini hapo.

Hata hivyo, haikuweza kujulikana kama ukarabati huo, unatokana na ahadi za serikali au ni juhudi za wadhamini, kutokana na mzee mmoja aliye ndani ya kamati ya msikiti, huo, ambaye jina halikuweza kufahamika mara moja kushindwa kujibu mara alipoulizwa na mwandishi huyu, alipokuwa anatafuta ukweli juu ya ukarabati huo.

"We mbona unaulizauliza maswali mengi, kwani ni mwandishi wewe…mimi sijui kama ni Serikali au wadhamini, ninachojua msikiti unakarabatiwa kwa nguvu zetu na ukitaka kujua mengi mfuate Sheikh Songambele au Imamu Thabit….", alisema mzee huyo."