WAISLAMU hawana agenda ya siri bali wanachotaka ni haki zao kwa kulilia kuwepo na utawala wa haki, sheria, unatoa uhuru na usawa kwa wote bila ya ubaguzi.
Hayo yamesemwa na Sheikh wa Mkoa wa Morogoro (Bakwata) Sheikh Omar Mohamad Bafadhil katikati ya wiki hii. Akiongea na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwake Mji Mpya, Sheikh Bafadhil alisema kwamba kilio cha Waislamu juu ya haki zao na kuonewa kwao katika nyanja mbalimbali kimekuwa ni cha muda mrefu, lakini hakipati majibu.
Amesema Masheikh wamekuwa wakiwaelimisha wananchi wawe raia bora kwa kuwapa maadili bora, kupiga vita rushwa, wizi, uzinzi na ubadhilifu wa mali ya umma, lakini mchango wao hauonekani kuthaminiwa.
Tofauti na wao, amesema kwamba viongozi wa Makinsa wamekuwa wakipewa heshima kubwa na serikali na kila wanalolisema serikali hulichukulia kwa uzito mkubwa.
Amesema hali hiyo ni ya hatari, kwani itafika mahali wao Masheikh washindwe kuwa na kauli juu ya waumini wao na kuwaacha wapiganie haki zao kwa njia ambazo zaweza kuzua balaa katika nchi.
Akizungumzia suala la Mwembechai, Sheikh Omar Bafadhil amesema anasikitika kwamba imefikia mahali Waislamu wanauliwa, wanawekwa ndani na kunyimwa haki yao ya kikatiba hadi wengine wanafia ndani.
Alisema inamsikitisha zaidi kuona kwamba katika nchi hii ambayo serikali yake haina dini, Muislamu anashitakiwa na kuonekana mhalifu kwa kusema kwamba Yesu si Mungu.
Aidha, alimsifu na kumuombea kila la kheri Mheshimiwa Kitwana Kondo
kwa kujitokeza kwake kuwatetea Waislamu wanaoteseka gerezani kwa kunyimwa
dhamana, Sheikh Omar Bafadhil ambaye alimwita Mh. Kitwana Kondo kwamba
ni Ndugu na kipenzi cha Waislamu alisema bila ya kujali cheo na madaraka
yake,
Mh. Kondo amejitolea kutetea haki za wananchi na kwamba anastahiki
kuungwa mkono na Waislamu wote nchini.
Sheikh Bafadhil amesema kwamba amesikitishwa sana kwa kauli iliyotolewa na mmoja wa viongozi wa Bakwata ikimtuhumu Mh. Kitwana Kondo.
Alisema toka Waislamu wauliwe pale Mwembechai, Bakwata haijasema lolote. Haijawasaidia walio ndani ambao ni wagonjwa japo kwa dawa wala kuwaombea dhamana. Leo anajitokeza Mh. Kitwana Kondo kuwatetea Waislamu wale ndio Bakwata inapata sauti. Sauti yenyewe ya kumshutumu anayewatetea Waislamu!
Sheikh Omar alisema hoja hapa sio milioni 28, bali Waislamu wanaoteseka ndani na wale wanaoshitakiwa kwa kusema Yesu si Mungu. Aidha, alisema "Kama kulikuwa na tuhuma za milioni 28 kwanini zisitolewe kabla, iwe leo baada ya Mh. Kitwana Kondo kuwatetea Waislamu?" Alihoji Sheikh Omar.
Kuhusu nafasi ya Maimamu na Masheikh wa mikoa na wilaya, Sheikh Omar amesema kwamba hawa wamekuwa wakivishwa vilemba vya ukoka kwani wameshindwa kabisa kudai na kutetea haki za Waislamu nchini.
Kwa ajili hiyo, amesema hivi sasa kunahitajika mabadiliko katika Baraza ili wapatikane viongozi walio tayari kujitolea muhanga kwa ajili ya Waislamu. Amewakumbusha Masheikh wenzake kwamba wao ni wachunga na wataulizwa mbele ya Allah (s.w.) nini wamefanya kuwasaidia Waislamu.
Sambamba na hilo, amehimiza umoja na kutaka juhudi za pamoja zifanyike ili kuwaletea Waislamu maendeleo katika elimu, afya na huduma nyingine za jamii.
Amesema Waislamu vijijini hawajui hata udhu wao. Aidha, kunahitajika mashule ya awali, msingi, upili na vyuo vya ufundi kwa ajili ya vijana wa Kiislamu.
Yote hayo amesema kwamba yanahitaji nguvu za pamoja na ndiyo ya msingi kufanywa. Kwa ajili hiyo ametoa wito kwa Mabaraza na Taasisi mbalimbali kuunganisha juhudi zao katika kufanya mambo haya ya msingi badala ya kupoteza muda mwingi wakilumbana katika mambo yasiyowasaidia Waislamu. Na akaongeza kusema kwamba lau wataendelea kulumbana basi wafanye hivyo wakijua kwamba "vita vya panzi furaha ya kunguru".
Kuhusu kufadhiliwa shughuli za Kiislamu, Sheikh Omar aliungana na Mh. Kitwana Kondo kulaani hali inayojitokeza ya kuyatisha mashirika na watu binafsi wanaosaidia shughuli halali kwa mujibu wa sheria za nchi. Alisema inashangaza wafadhili wa shughuli za Waislamu wanatishwa wakati hilo halionekani kwa shughuli za Makanisa.
Katika jumla ya mambo yanayomsikitisha na kumtia huzuni, alisema Sheikh Omar ni vitisho vya mara kwa mara vya kutaka kulifungia gazeti la AN-NUUR. Alisema Wakristo wana vyombo vya habari chungu nzima, ikiwemo televisheni, redio na magazeti. Lakini gazeti moja na pekee la Waislamu limekuwa halipumui kwa kuandamwa.
Kuhusu hali ya Bakwata hivi sasa, Sheikh Omar amesema kwamba Sheikh Mkuu anahitaji msaada mkubwa toka kwa Masheikh ambao wapo karibu na waumini ili ajue nini Waislamu wanataka na wanasema nini juu ya Baraza.
Kwa ajili hiyo, ametoa wito kwa Kamati ya Ulamaa na Masheikh wengine kujitahidi kuwa karibu na Sheikh Mkuu ili kumsaidia katika kuyaweka mambo sawa.
Amesema hivi sasa ni jambo la kutia huzuni kwamba yale mambo yaliyokemewa waziwazi katika Qur’an kama ushirikina wa kupiga ramli hufanywa na viongozi wa ngazi za juu wa Baraza tena kwa fakhari na kwa kujinadi.